KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday 15 September 2011

Wakuu wapya wa mikoa watangazwa

15th September 2011
  Wakuu wa wilaya 11 wapanda
  Sura mpya nne nazo zateuliwa
  Saba wastaafu, wanne kiporo
Rais Jakaya Kikwete, ameteua wakuu wa mikoa wapya 15, kati yao 11 wakiwa waliokuwa wakuu wa wilaya, wanne kutoka nje ya nafasi hizo, huku saba wakistaafu na wanne wakiachwa kwa maelezo kwamba, watabadilishwa vituo vya kazi.
Pia wakuu wa mikoa mipya minne ya Simiyu, Geita, Katavi na Njombe itakayoundwa baada ya taratibu kukamilika, watatangazwa baadaye.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, walioachwa, ambao watapangiwa vituo vingine vya kazi, ni Amina Mrisho aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani; Dk. James Msekela (Dodoma); Abeid Mwinyimusa (Tabora) na Daniel Ole Njoolay (Rukwa).
Waliostaafu ni Mohammed Babu (Kagera); Isidore Shirima (Arusha); Kanali Mstaafu Anatory Tarimo (Mtwara); John Mwakipesilem (Mbeya); Kanali Enos Mfuru (Mara); Brigedia Jenerali Dk. Yohana Balele (Shinyanga) na Meja Jenerali Mstaafu Said Kalembo (Tanga).
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Singida amebaki kwenye kituo chake cha kazi wakati wakuu wa mikoa wengine wanne watapangiwa kazi nyingine.
Wakuu wa wilaya 11 waliopandishwa vyeo na kuwa wakuu wa mikoa, ni John Tupa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara; Saidi Mwambungu (Ruvuma); Chiku Gallawa (Tanga); na Leonidas Gama (Kilimanjaro).
Wengine ni Dk. Rehema Nchimbi (Dodoma); Elaston Mbwillo (Manyara); Kanali Fabian Massawe (Kagera); na Fatma Mwassa (Tabora); Ali Nassoro Rufunga (Lindi); Mhandisi Ernest Welle Ndikillo (Mwanza) na Magesa Stanslaus Mulongo (Arusha).
Walioteuliwa nje ya nafasi hizo, ni Mhandisi Stella Manyanya (Rukwa) na aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza (Pwani).
Wengine ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera (Morogoro) na aliyekuwa Mbunge wa Kalambo (CCM-2005-2010), Ludovick Mwananzila (Shinyanga).
Waliobadilishwa vituo vya kazi, ni Abbas Kandoro anayekwenda Mbeya akitokea Mwanza; Said Mecki Sadiki anayekwenda Dar es Salaam akitokea Lindi na Dk. Christine Ishengoma anayekwenda Iringa akitokea Ruvuma.
Wengine ni Luteni Kanali Issa Machibya anayekwenda Kigoma akitokea Morogoro na Kanali Joseph Simbakalia anayekwenda Mtwara akitokea Kigoma.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa wakuu wote wa mikoa waliopo sasa, wameagizwa kuandaa Hati za Makabidhiano (Handing Over Notes) katika muda wa siku 14 kuanzia siku ya kuapishwa kwa wakuu wapya wa mikoa.
Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa wakuu wa wilaya, ambao wamepandishwa vyeo kuwa wakuu wa mikoa, nao wanapaswa kufanya hivyo hivyo kwa ajili ya wakuu wa wilaya watakaopangiwa vituo vitakavyokuwa vimeachwa wazi kutokana na uteuzi wao.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa wakuu wa mikoa minne mipya na wakuu wa wilaya watakaoteuliwa baadaye, nao watatakiwa kuandaa Hati za Makabidhiano ndani ya siku 14 tangu kuapishwa.
“Makabidhiano hayo lazima yahusishe pia kutembelea kwa pamoja baadhi ya maeneo na miradi, ambayo ni muhimu kama sehemu ya makabidhiano yao,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliwataka wakuu wote wa mikoa walioteuliwa na wakuu wa mikoa minne mipya wakaoteuliwa pamoja na wakuu wote wa wilaya watakaoteuliwa baada ya zoezi kukamilika kuhudhuria mafunzo ya wiki tatu.
Mafunzo hayo yatatolewa kwenye Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi wa kiuongozi na kiutendaji.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa wakuu hao wapya wa mikoa wataapishwa kesho saa 4.00 asubuhi kwenye viwanja vya Ikulu, jijini Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment