KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday 22 December 2011

CHADEMA WATOA TAMKO KUHUSU MAFURIKO JIJINI DAR ES SALAA



CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

SALAAM ZA RAMBIRAMBI NA POLE KWA WANAFAMILIA NA WANANCHI KUHUSIANA NA
JANGA LA MAFURIKO YALIYOKUMBA JIJI LA DAR ES SALAAM, MBEYA NA DODOMA .
Usiku wa kuamkia tarehe 20.12.2011 Maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es
Salaam, Mbeya na Dodoma yamekumbwa na maafa makubwa ya mafuriko ambayo
yamesababishwa na mvua kubwa ambazo zimeendelea kunyesha mfululizo
katika maeneo hayo.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapenda kutoa pole za
dhati kwa wanafamilia na wananchi wote ambao wamekumbwa na janga hili
kubwa , kwani limesababisha maafa makubwa sana ya vifo, kupoteza mali
na miundombinu mbalimbali kuharibiwa vibaya kwenye maeneo husika.
Tunapenda kuwahakikishia wananchi hawa kuwa tutakuwa nao pamoja katika
kipindi hiki kigumu katika maisha yao kutokana na madhara waliyopata
yaliyosababishwa na maafa haya.

Kutokana na janga hili limetukumbusha jambo moja kuwa kama Taifa
hatujajiandaa kikamilifu kuweza kukabiliana na majanga kama haya pindi
yanapotokea na hata vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeonyesha
dhahiri kuwa havijaandaliwa kimfumo na kinyenzo katika kuweza
kukabiliana na majanga kama haya na huu ni udhaifu mkubwa sana kwa
taifa lenye miaka 50 baada ya uhuru wake .

Mathalani mpaka sasa hatujaona jitihada zozote ambazo zimechukuliwa na
Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa katika kuonyesha juhudi za
kukabiliana na janga hili kubwa kwa taifa letu,hii inaonyesha wazi
kuwa kitengo hiki hakijaandaliwa kuweza kukabiliana na maafa kama
ambavyo majukumu yake yanavyopaswa kuwa . Na hii ni hatari kwani kama
chombo cha kukabiliana na maafa hakiwezi kufanya hivyo kwa wakati ni
kuendelea kuwaacha wananchi waendelee kupata madhara makubwa zaidi. Na
haswa ikizingatiwa kuwa idara ya hali ya hewa ilishatahadharisha
kuhusiana na mvua hizi.

CHADEMA tunapenda kuikumbusha serikali kuhusiana na ilani yetu ya
uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo ilieleza wazi kuhusiana na kukosekana
kwa mifumo thabiti ya kujulisha umma kuhusiana na majanga mbalimbali
katika miji yetu (Early Warning Systems) kama ambavyo ipo katika nchi
nyingi , mfumo huu ni muhimu sana katika kuweza kuufanya umma uwe na
elimu ya jinsi ya kuweza kujikinga na majanga haya kwa lengo la
kupunguza madhara yasiwe makubwa kama ambavyo taifa hivi sasa
linashuhudia.

CHADEMA inapendekeza hatua zifuatazo ziweze kuchukuliwa haraka na
serikali ili kuweza kukabiliana na majanga/maafa mbalimbali hapa
nchini yanapojitokeza;

I) Kuandaa mfumo wa awali wa kutahadharisha umma juu ya ujio wa
majanga (Early Warning Systems) kwa kutumia vyombo na nyenzo
mbalimbali ili kuepusha madhara makubwa kwa watu na mali zao.

II) Kutunga sheria mpya ya ujenzi na kuweka viwango vya ujenzi viwe
vyenye hadhi ya kimataifa na haswa ujenzi wa kuta mbalimbali na
majengo marefu na kuhakikisha kuwa ujenzi holela haujitokezi kwenye
miji na majiji yetu hapa nchini.

III) Kuhakikisha kuwa kwenye miji yote mikubwa mtandao wa mabomba ya
maji ya dharura unawekwa ili kuweza kukabiliana na majanga ya moto
pindi yanapotokea.

IV) Serikali ijiandae mara moja kukabiliana na magonjwa ya milipuko
kama vile kuhara ,kipindupindu na mengineyo ambayo yatajitokeza
kutokana na mafuriko haya kuharibu miundombinu ya kusambaza maji,
makazi ya watu n.k.

V) Kitengo cha maafa kiwe na vifaa wakati wote , na haswa vifaa kwa
ajili ya uokoaji na wawe na utaratibu wa kutoa elimu kwa umma jinsi ya
kuweza kutumia vifaa hivyo kuweza kujiokoa na sio kuacha hali iwe kama
ambavyo imejionyesha Dar Es Salaam jana baada ya baadhi ya majaketi
okozi kufikishwa kwa wahanga na kushindwa kuyatumia kikamilifu.

VI) Serikali itoe elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa ya milipuko
kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko haya ili kuepusha wananchi wengi
kukumbwa na magonjwa hayo pindi yakijitokeza.

Mwisho tunapenda kuendelea kutoa pole kwa wanafamilia wote na wananchi
kwa ujumla kutokana na madhara makubwa waliyoyapata , Mungu awajaze
nguvu katika kipindi hiki kigumu.
Tamko hili limetolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu CHADEMA .

……………….

DR. Willbroad P. Slaa.

Katibu Mkuu –CHADEMA.


22/12/2011.

WAZIRI MAGUFULI ATAKA KUTENGENEZA BARABARA ZIPITIKE



NA MAGRETH KINABO – MAELEZO
22/12/2011
WAZIRI wa Ujenzi ,Dk. John Magufuli amewataka mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS) wa mikoa nchini kutengeneza barabara ili ziweze kupitika na kuacha kisingizio cha sababu ya mvua.

Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri Magufuli katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa usafiri wa haraka wa mabasi jijini Dares Salaam wa awamu ya kwanza wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo alitolea mfano wa mkoa wa Iringa. “Sitaki kuona barabara inayosimama kwa sababu ya kusingizio cha mvua. Ni wajibu wao kuona barabara zote zinapitika,” alisema Waziri Magufuli huku akisema fedha za mfuko wa barabara zipo wakandarasi na mainjia wapo. Waziri Magufuli alitolea mfano pia barabara ya Mwenge hadi Tegeta, Mandela eneo la Kitunda zilizopo katika jiji la Dares Salaam ambapo alisema alitaka wakandarasi husika wapewe maelekezo ili waweze kutengeneza barabara hizo kwa kuwa ni jukumu lao.

Wakati huohuo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Patrick Mfugale ambaye alitia saini katika mkataba huo na Meneja Mkazi wa kampuni ya Strabag kutoka Ujerumani, Heribert Schippers, ambayo ndiyo mkandarasi mradi huo alisema ujenzi wa awamu ya kwanza utagharimu sh. 240. 87 unahusisha ujenzi wa barabara wa kilometa 20.9 katika barabara ya Morogoro , kutoka Kimara hadi Kivukoni Feri. Eneo jingine ni barabara ya Kawawa kutoka Magomeni hadi Morocco na barabara ya Msimbazi kutoka Fire hadi Makutano ya barabara ya Nyerere. Aliongeza kuwa ujenzi huo utachukua kipindi cha miaka mitatu.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usafiri wa Haraka(DART) , Cosmas Takule alizitaja changamoto zinazoukabili mradi huo kuwa ni kesi ya wakazi wa Gerezani ya tangu mwaka 2008 ambayo imekwamisha ujenzi wa fungu la tano na ujenzi wa miundombinu, hivyo kukwama wa eneo hilo kunatishia uhai wa mradi kwa kuwa linakutanisha awamu tatu muhimu. Alizitaja Changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wananchi kufungua kesi kwa madai ya kutaka nyongeza ya fidia na ufinyu wa bajeti ya wakala ambao unakwamisha utekelezaji wa masuala mengine ya msingi katika kufanikisha mradi huo.

Katika hatua nyingine Waziri wa Uchukuzi ,Omari Nundu , Waziri wa Miundombinu wa Uganda Dk. Chebrot Stephen na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya China Civil Engineering Constraction Corporation (CCECC EAST AFRICA LIMITED), Wang Xiang dog leo(jana) wametia saini mkataba ya utafiti wa kina wa mradi wa ujenzi wa reli na bandari mpya.

Utafiti huo utakagharimu dola za marekani milioni 450 utafanywa na kampuni hiyo,ambapo. Mradi huo utahusisha ujengaji wa reli kutoka Tanga- Musoma- Arusha zikiwemo bandari mpya.Fedha za utafiti huo zimetolewa na Tanzania, ambapo utafiti huo utafanyika kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita

JAJI (MSTAAFU) DAMIAN LUBUVA ATEULIWA KUWA MWENYEKITI WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI


I nytt fönster
Skriv ut alla










 




















 Jaji(Mtaafu) Damian Lubuva kushoto akiwa na Jaji Mkuu mstaafu Augustino Ramadhani


PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete amemteua Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Damian Lubuva kuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Aidha, Rais Kikwete amemteua Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Hamid Mahmoud
Hamid kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Bwana
Julius Benedicto Mallaba kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi.

Taarifa iliyotolewa leo, Alhamisi, Desemba 22, 2011 na Katibu Mkuu
Kiongozi, Bwana Phillemon L Luhanjo mjini Dar es Salaam imesema kuwa
uteuzi huo umeanza tokea Jumatatu, Desemba 19, mwaka huu, 2011.

Kabla ya uteuzi wake, Mheshimiwa Lubuva alikuwa Jaji katika Mahakama
ya Rufani Tanzania na baada ya kustaafu aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa
Baraza la Maadili ya Viongozi.

Mheshimiwa Lubuva anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mheshimiwa Jaji
Lewis Makame ambaye mkataba wake wa utumishi wa umma ulifikia mwisho
Julai, mwaka huu, 2011.

Naye Mheshimiwa Hamid alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kabla
ya kustaafu kwake na anachukua nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Mhe
Jaji Omari O. Makungu. Mheshimiwa Jaji Makungu aliteuliwa na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baadaye
akateuliwa kuwa Jaji Mkuu.

Naye Bw. Mallaba, kabla ya uteuzi wake, alikuwa Mkurugenzi wa Sehemu
ya Mikataba (Contracts and Treaties) katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali. **Bw. Mallaba anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Bwana
Rajabu Kiravu ambaye amemaliza mkataba wake wa utumishi Septemba,
mwaka huu, 2011.

Imetolewa na:

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

22 Desemba, 2011