KATIBU WA NEC, ITIKADI NA UENEZI CCM, Bw Nape Nnauye
--
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imemaliza kikao chake cha siku moja usiku wa tarehe 31/07/2011 mjini Dodoma chini ya uenyekiti wa  Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.
Pamoja na mambo mengine Kamati Kuu imeamua yafuatayo;
1.    Imefanya uteuzi wa makatibu  ishirini  na saba (27) kujaza nafasi zilizokuwa wazi katika wilaya hizo. (majina  na wilaya zao yameambatanishwa). Pamoja na uteuzi huo, Kamati Kuu  imetengua uteuzi wa Makatibu wa Wilaya watatu (3) katika kuboresha  ufanisi wa kazi katika wilaya hizo.(majina na wilaya zao  yameambatanishwa).
2.    Kamati Kuu imepokea na kuridhia taarifa ya kujiuzulu kwa       aliyekuwa  Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuwakilisha Mkoa wa Tabora,  Ndugu Rostam Aziz. Aidha imempongeza kwa uamuzi huo uliozingatia maslahi  mapana ya chama chake. 
3.    Kamati  Kuu imepokea pia taarifa ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wa Igunga,  Ndugu Rostam Aziz na kuagiza chama kupanga ratiba ya mchakato wa kumpata  mgombea ubunge wa Jimbo la Igunga itakayozingatia ratiba ya Tume ya  Taifa ya Uchaguzi juu ya uteuzi wa mgombea.
Aidha  Kamati Kuu imeagiza shughuli zote za kampeni kutafanywa na CCM Mkoa,  Wilaya na ngazi zote za chama wilayani Igunga. CCM Taifa watashiriki  kuongeza nguvu. Chama kinatoa wito kwa wana CCM, wapenzi na wakereketwa wa chama chetu kushiriki kwa pamoja kuhakikisha jimbo linabaki kwa CCM.
4.    Kamati  Kuu haijaridhishwa na kiwango cha bei ya mafuta ya taa nchini kwa kuwa  ndio nishati inayotumiwa na wananchi wengi wenye kipato cha chini. Aidha  Kamati Kuu haikuridhishwa na maelezo ya kupandishwa kwa bei ya mafuta  hayo kwa kisingizo cha kuzuia uchakachuaji wa mafuta mengine. 
Hivyo basi,  Kamati Kuu imeiagiza Serikali kutafuta njia za kushusha bei ya mafuta  ya taa na kuvitaka vyombo vya Serikali vinavyohusika na usimamiaji wa  ubora wa mafuta, vihakikishe vinatimiza wajibu wake kuzuia kabisa mtindo  wa uchakachuaji wa mafuta nchini na si kupandisha bei ya mafuta ya taa  kama suluhisho.
5.    Kamati  Kuu inasikitishwa na tatizo la umeme nchini kwani athari zake kwa  uchumi wa Taifa na mtu mmoja mmoja ni kubwa. Hivyo basi imeitaka  Serikali kutumia muda iliyopewa wa kurekebisha Bajeti ya Wizara ya  Nishati na Madini kuja na mpango wa dharura wa kunusuru hali hii na  kisha kulimaliza kabisa tatizo la umeme nchini. 
6.    Aidha  Kamati Kuu imejadili masuala mengine kama; migogoro ya ardhi, tatizo la  bei ya pamba, tatizo la uuzaji wa mahindi, migogoro migodini, masuala  yanayohusu kero za Muungano na kuagiza Serikali kuyashughulikia kwani  yanatatulika.
7.    Kamati Kuu imeipongeza Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa  kwa  kazi nzuri ya kutekeleza maamuzi ya NEC na kuitaka iongeze kasi katika  utekelezaji huo, ili kuhakikisha mageuzi yaliyokusudiwa yanatekelezwa  kwa wakati. Aidha imejadili na kupitisha miundo mipya ya Idara ya  Itikadi na Uenezi na Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
8.    Kuhusu  suala la maadili ndani ya Chama, Chama kinaendelea kusimamia maadili,  na kuwataka wale waliotakiwa kujipima na kuwajibika watumie muda huo,  kujipima na kuwajibika kwa masilahi mapana ya chama.
Aidha  Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inatarajiwa kukutana wakati wowote mwezi  Septemba, ambapo pamoja na mambo mengine itatathimini utekelezaji wa  maamuzi yake. 
Imetolewa na:-
 Nape M. Nnauye (MNEC)
KATIBU WA NEC, ITIKADI NA UENEZI
DODOMA
1/8/2011
No comments:
Post a Comment