KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Friday 19 August 2011

Shibuda alipuka bungeni

 
Thursday, 18 August 2011 22:21

Fidelis Butahe
MBUNGE wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda jana alilishangaza Bunge baada ya kutumia sehemu ya dakika zake za kuchangia Hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuzungumzia zaidi hatma yake kisiasa  na chama chake.

Akizungumza wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2011/12, Shibuda alisema hata siku moja hakuwahi kuvunja msimamo wa kikao cha Kamati Kuu(CC) ya chama hicho, bali anatofautiana na viongozi wa Chadema kwa dhamana zao binafsi huku akisisitiza, “Ni haki katika hili”.
Shibuda amewahi kuhojiwa baada ya kupingana na msimamo wa chama hicho wa kumsusia Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akizindua Bunge Desemba mwaka jana kwa kuhudhuria dhifa katika Ikulu ya Chamwino huku akiweka bayana kupingana na msimamo huo.Lakini, jana  akizungumza kwa msisitizo na kutoa mifano mingi ya maneno ya Kiswahili, Shibuda alisema, “Ninaulizwa maswali mengi juu ya hatma yangu ndani ya Chadema na hili vilevile nimeona ni bora kulizungumza,”.

Kauli hiyo ya Shibuda ilimshtua Spika wa Bunge, Anna Makinda ambaye aliuliza iwapo suala hilo linahusu masuala ya Utalii, “Hilo nalo ni utalii,”

Baada ya kujibu kuwa suala hilo pia linahusu masuala ya maliasili na utalii, Shibuda alisema “Maliasili ya nchi yetu ni siasa bora na utawala bora, nimeona hilo nilizungumze”.Alisema viongozi wa dini kazi yao kubwa ni kumng’arisha binadamu ili aweze kwenda ahera na viongozi wa siasa kazi yao ni kuwa madobi wa kuing’arisha Serikali.

“Nimeamua kulisema kwa kuwa kila mtu (hata wabunge) wananiuliza kama kamati kuu ya Chadema imeniita na kwamba, nitafukuzwa,” alisema Shibuda.

Atuhumu baadhi ya vyombo vya habari
Licha ya kutotaja majina ya magazeti aliyoyatuhumu, Shibuda alisema  kwamba kauli  zinazoandikwa  na kunukuliwa na baadhi ya magazeti ni kauli hatarishi , huku akisisitiza kuwa  kauli hizo za vyombo vya habari zinaacha vikwazo kwa wanasiasa.
Alisema kuwa hata Jukwaa la vyombo vya habari nchini lina mazuri na mabaya yake na kwamba  apendaye kutumia jukwaa la siasa ni sawa na mtu mpenda fitina.

“Maneno yaliyonukuliwa na viongozi wa Chadema katika vyombo vya habari kwamba mimi ni msaliti si kweli na wala sijavunja msimamo wa uongozi wa kikao cha kamati, nimetofautiana na watu kwa dhamana zao binafsi,” alisema Shibuda.Alisema kuwa hawezi  kugandishwa na kukosa demokrasia ya kikatiba ya  kutoa maoni yake, na kwamba  yoyote anayegeuza au kutumia cheo chake kwa maslahi binafsi hatakuwa na tofauti na Pius Msekwa.

Msekwa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara anatuhumiwa  kuingilia  watendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA), kwa kujihusisha na utoaji wa ofa kwa wafanyabiashara wanaotaka kujenga hoteli za kitalii.

“Mazuri huwa ya baba na mabaya huwa ya mama…,  bahari ikichafuka nahodha hupimwa kwa ujasiri wake, nakiri kuchafua hali ya hewa ila napenda kuwaambia kuwa Shibuda ni jasiri,” alisema.

Aliongeza, “Maswa sio Pundapori ina wenyewe na wananchi wa Maswa wamekataa kuporwa mbunge wao kama wanyamapori, CCM ni demokrasia pana na Chadema ni kwa maslahi ya jamii, lakini kila kizuri hakikosi kasoro heshima na busara ndio itatuongoza kufika salama,”.

 “Vyama vya siasa vipo kama 12 hivi, vipo vyama maslahi binafsi, jamii, ushirika na Saccos…, mimi kudhalilishwa na kupuuzwa sijali  sana kwa kuwa ninaongozwa na ukweli na siwezi kusema uongo,” alisema  Shibuda.

No comments:

Post a Comment