KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Wednesday 24 August 2011

Mwili wa marehemu Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mussa Khamis Silima waagwa Zanzibar


ZANZIBAR- MSIBA -MBUNGE
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi leo jioni wameuaga mwili wa marehemu Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mussa Khamis Silima baada ya kufikishwa katika ukumbi wa Baraza hilo Visiwani Zanzibar.
Kwa mujibu wa kanuni za Baraza la Wawakilishi kuanzia sasa Mjumbe yoyote atakayefariki atalazimika kufikishwa katika Baraza hilo kwa kuombewa dua na jeneza kufunikwa Bendera ya Baraza la Wawakilishi.
Mwili wa marehemu uliwasili uwanja wa ndege wa zamani saa 11:30 jioni kwa ndege ya kukodi ya Shirika la TANZAIR ambapo katika uwanja huo viongozi mbalimbali wa Serikali walikuwepo pamoja na wananchi.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho alishughulikia taratibu za kuusafisha mwili wa marehemu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dar es Salaam.
Mbunge wa viti Maalum(CCM), Maua Abeid Daftari alikuwa miongoni mwa viongozi walioleta mwili wa marehemu Visiwani hapa.
Katika taarifa ya Serikali ya Mapinnduzi Zanzibar kwa vyombo vya habari iliyotolewa jioni hii na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed ilisema marehemu anatarajiwa kuzikwa kesho Kijijini kwao Kiboje Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika taarifa hiyo, Waziri Aboud alimtaja marehemu Mussa kuwa ni miongoni mwa watu waliotoa mchango katika shughuli za kisiasa pamoja na utumishi wa muda mrefu Serikalini akiwa mwalimu ambaye amechangia maendeleo ya vijana wengi Visiwani Zanzibar.
Kabla ya kifo chake, marehemu Silima alipata ajali ya gari ambapo katika ajali hiyo, mke wa marehemu alifariki papo hapo na hali ya dereva wake bado anaendelea kutibiwa hospitalini.
Mwakilishi huyo aliumia ya sehemu ya miguu pamoja na kiuno kutokana na ajali iliyotokea eneo la Nzuguni Dodoma juzi na kulazimika kupelekwa Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Viongozi mbalimbali wa Serikali wanatarajiwa kuhudhuria katika mazishi hayo.

No comments:

Post a Comment