KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Monday 15 August 2011

IGP aonja makali ya wabunge

15th August 2011
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema (kulia), akibadilishana mawazo na wabunge baada ya kuwasilisha mada juu ya Uzalendo, Haki na Utii bila kushurutishwa kwa wabunge kwenye ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma jana.
Wabunge wamelishambilia Jeshi la Polisi na kulitaka kujisafisha kwanza kabla ya kuanza kampeni ya haki na utii wa sheria bila shuruti.
Waliyasema hayo wakati wakichangia katika semina kuhusu haki na utii wa sheria bila shuruti iliyofanyika bungeni mjini Dodoma jana. Mada hiyo iliwasilishwa na Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema.
LISSU: POLISI WANANUKA RUSHWA
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisema Jeshi la Polisi linanuka rushwa na watu wamekuwa wakibambikiwa kesi.
Alilitaka jeshi hilo kuanza kujisafisha lenyewe kabla ya kutekeleza kampeni hiyo ya utii wa sheria bila kushurutishwa.
AKUNAAY: POLISI KUWENI BINADAMU
Mbunge wa Mbulu (Chadema), Mustafa Akunaay, aliwataka polisi wanapowakamata watu kuwaadabisha baada ya kuwafikisha kwenye sehemu inayostahili.
“Polisi kuweni binadamu, polisi wetu ni wakatili sana,” alisema na kuongeza kuwa katika kitabu kinachoelezea dhana hiyo ya haki na utii wa sheria bila shuruti, ukurasa wa 48 askari wanamshikilia raia ambaye hana hatia.
Alisema utii wa sheria uanze kwanza kwa polisi kuwa binadamu wakati wanavyokuwa katika majukumu yao ya kazi.
Alisema suluhisho si kutawanya askari kila eneo, bali ni kufuata mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali na kwamba sheria inayounda Jeshi la Polisi ni sheria ya wakoloni.
KOMBO: POLISI WANADHALILISHA WAPINZANI
Mbunge wa Mgogoni (CUF), Kombo Hamis Kombo, alisema kama hakuna umoja na mshikamano katika kujengeana heshima baina ya viongozi na Jeshi la Polisi, uwasilishaji wa maudhui ya dhana hiyo kwa watu wa kada ya chini utakuwa ni mgumu.
“Kwanza tujenge kuaminiana baina ya viongozi tulioletewa mada hii na Jeshi la Polisi…utii Mheshimiwa Mwenyekiti utapatikana kama utii wa Jeshi la Polisi na utii wa viongozi utakwenda sambamba. Jeshi la Polisi liheshimu viongozi wote wa vyama vyote bila kujenga ubaguzi kwamba walio na haki ni viongozi wa chama tawala,” alisema na kuongeza:
“Leo ikitokea kwamba kiongozi wa chama cha upinzani anafanya mkutano anatoa maoni yake kwa watu inaonekana kuwa na uadui badala ya kumwita kistaarabu, anakwenda kuchukuliwa mbele ya hadhara ya waliomchagua anavunjiwa heshima. Tujenge kuaminiana baina ya polisi walioleta mada hiyo na wabunge.”
MACHALI: POLISI WANATUMIA AKILI KIDOGO
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, alisema kuwa Jeshi la Polisi limekuwa ni mabingwa wa kutumia nguvu katika maeneo mbalimbali nchini na hutumia akili kwa kiasi kidogo sana.
Alisema mara nyingi wakimkamata mtu hufikiri kuwa kile wanachokiamini wao ndicho alichokifanya mtuhumiwa na hawataki kumpa nafasi na yeye kuzungumza.
MNYIKA: UTII WA SHERIA UFANYIKE POLISI
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alitaka maeneo yote yanayokizana na tafsri ya kisheria, kikatiba na kisiasa yafanyiwe marekebisho.
“Ni vizuri pia kampeni hii ya utii wa sheria bila shuruti ikafanyika pia ndani ya Jeshi la Polisi lenyewe, mimi nafahamu Mheshimiwa Waziri na ni vyema ukalitolea kauli bungeni. Ulisema bungeni kuwa askari wanapewa posho ya Shilingi 150,000, askari wakaichukua ile kauli na kuanza kuulizia ndani ya Jeshi la Polisi,” alisema na kuongeza:
“Tunaomba posho ya Sh. 150,000 iliyotangazwa ndani ya Bunge kilichotokea, hawa ni askari watii hawajaandamana, hawajashika bunduki, kilichotokea askari akisema posho ya Shilingi 150,000 anawekwa ndani na wengine wamefukuzwa kazi.”
MNYAA: KASI YA MWEMA POVU LA SODA
Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habib Mohamed Mnyaa, alisema kasi aliyoingia nayo Mwema siyo kama ilivyo hivi sasa na kuifananisha na povu la soda.
Alisema ili kutii sheria ni lazima sheria zote za kutumia mabavu zibadilishwe kwanza na baada ya hapo ndipo serikali ije na kampeni hiyo kitaifa kama vile wanavyofanya katika kupambana na gonjwa la Ukimwi.
KAFULILA: TATIZO NI UTAWALA
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema majeshi yote yanapata kazi ngumu sana katika kipindi ambacho utawala umeporomoka.
“Ninachokiona wewe na jeshi lako pengine mngeanza training (mafunzo), kuwa polisi kwenye mazingira ambayo utawala umeporomoka,” alisema na kuongeza:
“Unaposikia watu wanashiriki maandamano pengine kama hoja ipo ama haipo ujue kwamba tafsiri yake ni kwamba kuna hali fulani kama ya wananchi kuasi, mnawezaje kuimanage (kuimudu) peke yenu kama Jeshi la Polisi hamuewezi, lakini mnaweza kama mnaweza kuwaambia ukweli watawala.”
SENDEKA: HAKI ZA KUANDAMANA ZIFUATWE
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema haki za kuandamana ni vema zikafuata taratibu ili kuepusha ugomvi baina ya raia na askari polisi.
“Mimi naamini kuwa jeshi liloandaliwa kistaarabu halitaingilia mjumuiko uliofuata taratibu za kistaarabu, lakini kuwa na jeshi liloandaliwa vyema likinyamaza pale maandamano yanapokuwepo ambayo hayakufuata utaratibu litajitwalia sifa ya kuwa jeshi dhaifu. Ni imani yangu kuwa tuna wajibu kama raia kutii na jeshi lina wajibu wa kuhakikisha kuwa wananchi wanatii sheria,” alisema.
KAGASHEKI: JAZBA IMETAWALA MJADALA
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Khamis Kagasheki, alisema shabaha ya semina hiyo sio jazba na kwamba Wabunge waliochangia walionyesha jazba sana.
Alisema madhumuni ya kuwapa semina hiyo wabunge ni kuona ushirikiano gani watakaoupata kutoka kwao. Alisema kumekuwa na dhana kuwa madhumuni ya semina hiyo imelenga chama Fulani, lakini ukweli ni kwamba IGP Mwema aliitwa na Spika baada ya kupeleka kitabu chake na kumuomba akigawe kwa Wabunge.
Akizungumzia kuhusiana na utendaji wa polisi alisema: “Tukitaka tuwape likizo ya saa 24 wasifanye kitu chochote, kweli nchi hii itakalika… yote mliyoyasema tutayachukulia kwa umakini wake na kuyafanyia kazi.”
Kwa upande wa posho zilizodaiwa kuwafukuzisha kazi baadhi ya polisi, Kagasheki alisema hakuna askari aliyefukuzwa kazi kutokana na kudai posho na kuwataka Wabunge kufanya utafiti wa kina kabla ya kuzungumza.
MWEMA: TUMEWASIKIA
Naye Mwema alisema michango yote waliyochangia Wabunge jana na wakati wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, yamechukuliwa na timu maalum waliyoiunda wizarani.
Alisema hayo yanalenga katika kutengeneza jeshi la kisasa, weledi na linaloshirikiana na wananchi.

No comments:

Post a Comment