KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday 11 August 2011

Chadema yatikitisa Arusha

 
Wakazi wa Kata ya Kimandolu Mkoani Arusha, wakimsikiliza mbunge wa Arusha Mjini kupitia Chadema, Godbless Lema alipohutubia mkutano wa hadhara kulaani kuadimika kwa mafuta ya petroli na mgao wa umeme unaondelea nchini, mkutano ulioambatana na ufunguaji wa matawi ya Chama hicho. Picha na Silvan Kiwale
Peter Saramba, Arusha
SHUGHULI mbalimbali zikiwamo za kiuchumi na kijamii katika baadhi ya mitaa ya jiji la Arusha, jana zilisimama kwa muda wakati misafara mirefu iliyojaa mbwembwe za kila aina ya magari, pikipiki, baiskeli na mikokoteni iliyofungwa bendera za Chadema, ilipopita kwenye kata nne ambazo zilikuwa zikiongozwa na madiwani kiliowatimua uanachama hivi karibuni.

Ziara hiyo ya kwanza ya viongozi wa juu wa Chadema imekuja siku chache baada ya Kamati Kuu (CC) ya chama iliyokutana Mjini Dodoma kati ya Agosti 5 na 6, kuamua kuwafukuza uanachama madiwani wake watano kutokana na madai ya kuingia muafaka na CCM na TLP katika nafasi ya umeya wa jiji hilo Juni 20, mwaka huu bila ridhaa ya uongozi wa taifa.

Katika kile kilichoonekana kuwa ni kupunguza joto hilo na kuweka mambo sawa katika jiji hilo ambalo ni moja ya ngome muhimu za kisiasa za Chadema, viongozi hao wa kitaifa wakiongozwa Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na baadhi ya wabunge, waliingia jijini hapa wakiwa wamegawanyika katika makundi manne.

Misafara ya makundi hayo manne tofauti, ilianzia katika Viwanja vya Soweto, eneo la Kaloleni mjini hapa kuelekea katika Kata za Kimandolu, Themi, Elerai na Kaloleni kwenyewe.

Kutokana na msururu wa magari ya misafara hiyo, jiji la Arusha lilikuwa na msongamano mkubwa wa magari. Baadhi ya madereva walilazimika kujifanya kuwa ni sehemu ya msafara huo kwa kupiga honi kushangilia alimradi wapate mwanya wa kujipenyeza pembezoni mwa barabara kuendelea na safari zao.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Gulugwa alisema pamoja na kufanya maandalizi ya mkutano mkubwa wa hadhara unaotarajiwa kufanyika leo katika Viwanja vya NMC, Unga Ltd, ambao tayari umeruhusiwa na polisi, hatua ya jana ililenga kuimarisha uhai wa chama hicho kwa kufungua matawi na kuzungumza na wananchi.

Gulugwa alisema Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa wa Chadema, John Heche aliongoza kundi la viongozi katika Kata ya Elerai, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa aliongoza kundi la Sokon wakati Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alikuwa Kata ya Kimandolu.

Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje pamoja na Meya wa Manispaa ya Musoma, Alex Kasurura walikuwa Kata ya Kati.“Kwa upande wa Kata ya Themi, viongozi wote wataungana pamoja kutembelea eneo hilo kulingana na muda utakavyoruhusu. Kilele cha kampeni yetu ni kesho (leo) pale NMC,” alisema Gulugwa.

Aidha, viongozi hao wanatarajiwa kurejea tena katika kata hizo leo kuendelea na uhamasishaji wao kabla ya kwenda Unga Ltd katika mkutano wa hadhara.

Msimamo wa Polisi kuhusu mkutano leo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa, Thobias Andengenye alithibitisha ofisi yake kuruhusu shughuli za kutembelea kata, mitaa na vitongoji kwa viongozi wa Chadema pamoja na mkutano wa hadhara leo katika Viwanja vya NMC.

“Tumeruhusu shughuli zao za kisiasa kama walivyoomba kwa kutoa taarifa kulingana na sheria. Leo wanatembelea kata kufungua matawi na kuzungumza na wanachama na wananchi na kesho watafanya mkutano wa hadhara pale NMC, Unga Ltd,” alisema Andengenye kwa simu jana.

Katika mkutano huo viongozi hao, wakiongozwa na Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa pamoja na mambo mengine, watafafanua uamuzi wa kuwatimua madiwani hao.

Madiwani hao waliofukuzwa baada ya mvutano wa muda mrefu na uongozi wa makao makuu ni Estomih Mallah (Kimandolu), John Bayo (Elerai), Charles Mpanda (Kaloleni), Reuben Ngowi (Themi) na Rehema Mohamed (Viti Maalumu).

Mgogoro huo ulianza Juni 20, mwaka huu wakati madiwani wa Chadema Manispaa ya Arusha walipoingia muafaka wa kumtambua, Diwani wa Kata ya Olorien, Gaudance Lyimo kuwa Meya.

Awali, madiwani hao pamoja na chama chao walipinga kuchaguliwa kwake kwa madai ya kukiukwa kwa kanuni za uchaguzi za halmashauri. Kupinga huko kulifuatiwa na maandamano yaliyofanywa kwa nguvu na chama hicho licha ya kupigwa marufuku na polisi na kusababisha vifo vya watu watatu Januari 5, mwaka huu.

1 comment:

  1. USIKU MWEMA KAKA AMA KWELI TAARIFA ZAKO ZINAIAMSHA JAMII YA WATUMIA MTANDAO.

    ReplyDelete