KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Sunday 3 July 2011

CHADEMA YAISHINDA CCM KUHUSU SWALA LA POSHO

 
Sunday, 03 July 2011 .
PINDA ASEMA SERIKALI INAANDAA UTARATIBU WA KUFUTA
kutoka,  Dodoma
CHADEMA imeibuka mshindi dhidi ya Serikali kuhusu suala la posho baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutangaza bungeni kuwa Serikali imekubali pendekezo la kutafakari na kuziangalia upya posho mbalimbali wanazolipwa wabunge na watumishi wote umma.Ushindi huo wa Chadema katika hoja ya posho dhidi ya Serikali, umekuja baada ya malumbano yaliyozuka mwanzoni mwa mkutano wa nne wa Bunge la Kumi unaoendelea mjini Dodoma, huku ukiacha makovu ya kutupiana maneno na tuhuma miongoni mwa wabunge na mvutano na ofisi ya Bunge.

Ikiwa siku ya pili jana tangu Pinda kukubalika kwa pendekezo la kutafakari na kuangalia upya posho za watumishi wa Serikali na wabunge Ijumaa usiku, Naibu Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni, Zitto Kabwe, alisema Jumapili kuwa ajenda yao inaonekana kushinda.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini,  alisema lazima Chadema isimamie hilo hadi ushindi upatikane, kwa sababu nia yao ni kufika walipokusudia ambako ni kufutwa kwa posho hizo.

Juni 7, mwaka huu Zitto aliwasilisha barua ofisi ya bunge kukataa posho akisema watumishi wa Serikali na wabunge, hawastahili kulipwa posho wanapohudhuria vikao rasmi vya uwajibikaji wao wa kawaida.

Zitto alisema posho hiyo haistahili kulipwa kwake, wabunge wengine wala watumishi wa umma kwa kuwa kuhudhuria vikao ni sehemu ya kazi zao. Wabunge wanalipwa posho za vikao sh 70,000 kwa siku.

Alisema kitendo cha Waziri Mkuu kueleza kuwa watatafakari na kuangalia upya na kwamba suala la posho ni sera ya taifa na Ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni ishara ya kiongozi huyo wa juu kukubali wazo la Chadema na safari ya kufuta posho hizo.

Awali, mara baada ya Chadema kutangaza msimamo huo, Spika Anna Makinda alipinga uamuzi wa kususia posho akisema suala hilo lipo kisheria na kwamba hakuna mtu ambaye anaweza kuamua kuliondoa.

Alisema Wabunge wa Chadema wataendelea kulipwa posho za vikao kupitia akaunti zao za benki na watatakiwa kusaini fomu ya mahudhuriao ya Bunge, vinginevyo watajiweka katika wakati mbaya.

Hata hivyo, akihitimisha hoja za wabunge katika hotuba yake ya makadirio ya matumizi ya ofisi yake na zilizo chini yake juzi, Pinda alisema suala la posho lipo kwenye mchakato wa kuzingatia upya na kutekeleza mpango wa maendeleo kwa kufuta posho za vikao (sitting allowance).

Waziri Mkuu ambaye awali alionekana kupigana na Chadema, alisema Katiba inakataza suala la posho zisizo za msingi na kwamba utaratibu huo umeandaliwa kwa kufuata utaratibu mzuri bila ya kuathiri mazingira na mfumo uliopo ndani ya Serikali kwa watumishi wake.

hata hivyo, Ziito alisema jana kuwa Pinda amejipinga mwenyewe kwa kukubaliana na hoja yao ya kupinga posho, hasa aliposema kwamba, Katiba inapinga masuala ya posho zisizo za msingi na kwamba.

Zitto alisema chama chake (Chadema) kitalisimamia kwa nguvu zao suala hilo hadi mafanikio yatakapopatikana.

“Mimi nimepokea majibu ya Waziri Mkuu kwamba utaratibu wa posho unafanyika ili kuziangalia upya na kutekeleza mpango wa maendeleo kwa kufuta posho za vikao, kwa hiyo nasema Waziri Mkuu amekubaliana na hoja yetu ya kufuta posho zisizo na msingi ili kuijenga Tanzania, lakini lazima mfahamu kuwa Waziri Mkuu amejipinga mwenyewe,’’ alisema Zitto.

Mbunge huyo alisema baada ya majibu ya Pinda, kazi iliyopo mbele yao kwa sasa ni kuhakikisha kuwa mpango wa maendeleo unatekelezwa kwa nguvu zote kwa vitendo, bila ya kuweka nadharia na siasa ndani yake.

Zitto alisema Chadema itaendelea kushikilia msimamo wake wa kutosaini posho za vikao katika kipindi chote cha uhai wa Bunge ikiwa ni pamoja na kutokusaini fomu za vikao hivyo.

Alisema yeye kama Naibu Kiongozi wa Upinzani, aliamua kuwa mfano mwema wa kuigwa posho yake, alipoamua kuachia posho zake zote na kuapa kuwa hatazichukua kabisa.

“Mimi ni Naibu kiongozi wa upinzani bungeni, niliamua tangu Juni 8, mwaka huu kutokuchukua posho na napenda kuwahakikishia Watanzania kuwa, sijachukua posho hizo na sitapokea hata nikipewa,’’ alisema na kuongeza:

“Tangu wakati huo sijasaini fomu za mahudhurio na mkakati wa wabunge wote wa Chadema ni kuhakikisha kuwa zinatengenezwa fomu nyingine kwa ajili ya wabunge wa Chadema ili kusaini pindi wanapohudhuria vikao hivyo,’’ alisema Zitto.

Mbunge huyo ndiye alikuwa wa kwanza kuibua hoja hiyo, kabla ya Mwenyekiti wa Chadema ambaye ndiye Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, kuiwasilisha rasmi bungeni kama hoja ya chama.

Hata hivyo, taarifa zinaonyesha kuwa kabla ya hoja hiyo kuwasilishwa bungeni rasmi na Mbowe, mvutano mkubwa ulizuka miongoni mwa wabunge wa Chadema wakati wa kujadili hoja hiyo.

Inadaiwa kwamba baadhi ya wabunge wa Chadema walipinga hatua ya kususia poshondani ya vikao vya chama, huku Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda alipinga msimamo huo wa chama chake.

Shibuda wiki hii alikaririwa akisema hawezi kususia posho za vikoa kwa sababu uamuzi huo umechukuliwa kwa kuzingatia misingi ya ubinafsi.

Alisema kuwa wanaongoza hoja ya kukataa posho ndani ya chama hicho inaonekana hawana majukumu mengi katika majimbo yao.

Bajeti ya posho kwa walimu
Uamuzi huo wa Chadema, umekuja huku taarifa za utafiti wa taasisi ya Policy Forum inayojihusisha na tafiti mbalimbali za sera zikionyesha kuwa, katika mwaka 2008/2009, Serikali katika bajeti yake ilitenga Sh506 bilioni kwa ajili ya malipo ya posho.
 Kwa mujibu wa utafiti huo, ambao taarifa yake ilitolewa mwaka uliopita, fedha hizo ni sawa na mishahara ya mwaka mzima kwa walimu 109,000 ambao ni robo tatu ya walimu wote nchini.Kwa mujibu wa utafiti huo mwaka 2009/10 kiasi cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya posho za watumishi wa umma kilikuwa sawa na asilimia 59 ya malipo ya wafanyakazi wa ngazi ya chini.
Katika hatua nyingine, juzi Mbowe, aliitaka Serikali ndani ya mwaka mmoja kutengeneza sera ya kubana matumizi.Mbowe alisema hayo alipokuwa akiuliza swali Bunge lilipoketi kama kamati kwa ajili ya kupitisha bajeti hiyo.Baada ya kupewa nafasi ya kuomba ufafanuzi, Mbowe alisema ni vyema Serikali ikatoa muda maalum ambapo itatoa sera ya kubana matumizi ya Serikali.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, alisema serikali haiwezi kueleza muda maalum wa kufanya hivyo, badala yake muda uliotolewa katika Mpango wa Maendeleo wa Serikali wa Miaka mitano, utatumika pia kutengeneza sera hiyo.
Baada ya jibu hilo Mbowe alisimama tena na kusema ni vyema suala hilo likafanyanyika ndani ya mwaka mmoja, au katika bajeti ijayo kwa vile miaka mitano ni mingi kulingana na unyeti wa suala hilo.

No comments:

Post a Comment