KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Saturday 30 July 2011

HATMA YA WALIOSALIA KUJIVUA GAMBA NI LEO


 
Sunday, 31 July 2011 06:41

KAMATI KUU CCM YAKUTANA DODOMA, KUTOA UAMUZI MZITO
Neville Meena, Dodoma
 KAMATI Kuu ya CCM inafanya kikao chake cha kawaida mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete leo, huku wachunguzi wa mambo wakitabiri kuwa itatoa uamuzi wa mambo mazito yanayoweza kuwaacha wengi midomo wazi.

Miongoni mwa mambo hayo itakuwa ni thatmini ya azimio la chama hicho kujivua gamba lililofikiwa miezi mitatu iliyopita.

Mpaka sasa mchakato wa kujivua gamba ndani ya chama hicho kwa watuhumiwa wa ufisadi haujapiga hatua kubwa, ingawa siku tisini zilizowekwa zilishapita.

Kutokana na hali hiyo, wachunguzi wa mambo wanabashiri kuwa kamati hiyo itafanya uamuzi wa kushtukiza juu ya hatima ya watuhumiwa hao wa ufisadi Ili kukamilisha mkakati wake wa kujisafisha.

Kikao hicho kinafanyika siku chache baada ya mmoja wa makada wa CCM ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, kuamua kujiuzulu huku akiilaumu sekretarieti ya chama hicho kwa alichokiita kuwa ni kuendesha siasa chafu dhidi yake.

Rostam alijiengua katika mazingira ya mkakati wa CCM wa kujivua gamba, ambao umelenga kuwaondoa kwenye nyadhifa zao watuhumiwa wote wanaohusishwa na madai ya ufisadi.

Kujiuzulu kwa Rostam ambako kumelifanya Bunge kutangaza Jimbo la Igunga mkoani Tabora kuwa, ni miongoni mwa mambo ambayo yanatarajiwa kuchukua nafasi kubwa katika Kamati Kuu itakayokuwa chini Mwenyekiti wake, Rais Kikwete.

Tayari vyama kadhaa vya siasa vya upinzani vikiwemo, Chadema na CUF vimeanza kupiga jaramba kwa ajili ya kusimamisha wagombea wao.

Katika mazingira hayo, uchaguzi wa Igunga pia ni sehemu ya ajenda ambazo huenda CC itazijadili katika kikao chake cha leo.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye, aliliambia Mwananchi Jumapili jana kuwa kikao cha Kamati Kuu kitafanyika leo na kwamba, muda wake wa kuanza utategemea kumalizika kwa vikao vya kamati nyingine za maandalizi ambavyo vilifanyika jana.

"Leo (jana) vikao mbalimbali vya kamati za chama vinaendelea hapa na ni sehemu ya maandalizi ya kikao cha Kamati Kuu. Taarifa zaidi nadhani tusubiri kesho baada ya kikao kumalizika," alisema Nape.

Hata hivyo, Nape hakuwa tayari kutaja kamati ambazo zilikuwa zikiendelea na vikao vyake jana, lakini taarifa ambazo Mwananchi Jumapili lilizipata jana mchana zilidai kwamba, kamati moja wapo ambayo ilifanya kikao jana ni ya maadili.

Kikao hicho pia kinafanyika wakati ambao kumekuwa na misigano miongoni mwa makada wa chama hicho tawala nchini, hasa kuhusu jinsi Sekretarieti mpya inayoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Willson Mukama inavyofanya kazi.

Shutuma hizo ni jinsi inavyotekeleza maazimio ya kikao cha mwisho kilichoridhia mabadiliko makubwa ndani ya chama hicho, chini ya mpango wa kujivua gamba.

Nape na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Tanzania Bara Kapten John Chiligati, walitajwa na Rostam katika hotuba yake ya kujiuzulu aliyoitoa jimboni Igunga, kwamba ni miongoni mwa waliopotosha nia njema ya kuivusha CCM katika matatizo yanayokikabili.

Kujiuzulu kwa Rostam kulitafsiriwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya NEC la kujivua gamba.

Nape aliwataja Rostamu, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kuwa ni miongoni mwa wanaotakiwa kujivua gamba.

Pia Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Pius Msekwa, lithibitsha baadaya liwa alikutana na Chenge, Lowassa na Rostam na kwamba taarifa ya matokeo ya mazungumzo itawasilishwa katika vikao vikuu vya chama.

Tangu kutolewa kwa taarifa hiyo, hiki ni kikao cha kwanza cha juu cha CCM kufanya mkutano na taarifa hiyo ya Msekwa ambayo inachagizwa na kujiuzulu kwa Rostam huenda ikawasilishwa na kujadiliwa na leo kabla ya kufikishwa rasmi kwenye Halmashauri Kuu ta Taifa.

Hata hivyo kuna dalili za wazi kuwa kuna mvutano mkali wa kimakundi ndani ya CCM, ambao unakifanya chama hicho kugawanyika na kutofikia utulivu unaokusudiwa, licha ya mabadiliko makubwa ya uongozi yaliyofanyika hivi karibuni.

Katika kile kinachothibitisha kuwepo kwa misigano miongoni mwa makada wa CCM, mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu, wiki hii aliliambia Mwananchi Jumapili mjini hapa kuwa "Wanachama wengi wa CCM hawafurahishwi na ziara za Nape na washirika wake mikoani."

Zira hizo za Nape ambazo zinawahusisha makada wa CCM wanaojipambanua kuwa wanapinga ufisadi, zinaelezewa kuwa zinachochea chuki badala ya kujenga umoja.


"Kwa mfano unapowataja watu watatu tu kwamba ndio wanaopaswa kujivua gamba una maanisha nini? Mtu kama Rajab Maranda, Nazir Karamagi na wengine ndani ya CCM tunawaweka wapi? Mimi nadhani si haki kabisa, hawa jamaa wanataka kutupeleka mahali ambako siko," alisema mjumbe huyo wa CC.

Maranda ni Mtunza Hazina wa CCM, mkoa wa Kigoma ambaye anatumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kutiwa hatiani kwa wizi wa fedha zilizotoka katika akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kwa upande wake, Karamagi ni Kada wa CCM ambaye kama ilivyo kwa Lowassa alilazimika kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Nishati na Madini mwaka 2002 kutokana na kashfa ya Kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond.

Pia baadhi ya makada wa CCM, wamekuwa wakimtupia lawama Mwenyekiti wa CCM kuwa ndiye
kikwazo, kwa vile hataki kuonekana mbaya katika makundi yote yanayosigana ndani ya chama.

Hivyo, wanasema huenda wakasimama kusema ukweli mbele yake bila ya woga wakati kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM itakayofanyika wakati wowote kuazia sasa ili wajue mbichi na mbivu.

Wiki iliyopita Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kupitia kwa Kaimu Mwenyekiti wake, Benno Malisa na Katibu wa Umoja huo Taifa, Martin Shigella, ulitoa tamko la maazimio ya Baraza la Kuu la Umoja huo, ambalo pamoja na mambo mengine walipongeza mabadiliko mengi yaliyofanywa kupitia NEC.

Hata hivyo, viongozi hao hawakuwa tayari kuweka bayana msimamo wa jumuiya wanayoiongoza kuhusu malalamiko yanayokosoa utekelezaji wa falsafa ya kujivua gamba kwa maelezo kwamba, hayo ni mambo yanayohusu Sekretarieti na sio kazi yao.

"Sisi tunapongeza uamuzi wa NEC na tunaposema uamuzi wa tunamaanisha mabadiliko mengi ya kimfumo ambayo yanatuelekeza kukidhi matakwa ya sasa ya kisiasa nchini dhidi ya washindani wetu na kuwatumikia wananchi," alisema Malisa na kuongeza:

"Mabadiliko haya ni pamoja na utaratibu unaowataka wanachama wetu kutokuwa na madaraka au nafasi nyingi ndani ya chama na serikali kiasi cha kushindwa kuwajibika".

No comments:

Post a Comment