KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday 7 July 2011

Njaa yakabili robo tatu ya nchi

Mikoa 16 (sawa na asilimia 76) ya nchi inakabiliwa na njaa na inahitaji msaada wa chakula cha dharura.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, aliliambia Bunge jana kwamba, kutokana na hali hiyo, serikali imefuta vibali vyote vya kusafirisha mazao ya chakula nje ya nchi kuanzia Julai mosi, mwaka huu.
Maghembe alisema serikali pia imepiga marufuku uuzaji wa mazao ya chakula nje ya nchi kwa kipindi cha miezi sita, kuanzia Julai Mosi hadi Desemba 31, mwaka huu.
"Madhumuni ya hatua hizi ni pamoja na kuipa serikali nafasi ya kufuatilia mwenendo mzima wa upatikanaji wa chakula nchini kwa lengo la kujihakikishia usalama wetu wa chakula katika kipindi hicho na baada ya hapo," alisema.
Alifafanua kwamba pamoja na tatizo la njaa linaloikabili sehemu kubwa ya nchi, baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiwarubuni wakulima na kununua mazao yao moja kwa moja yakiwa shambani, jambo linalowanyonya wakulima.
Alisema ili kukomesha unyonyaji huo, serikali inakusudia kujenga masoko na maghala ya chakula katika maeneo mengi ili kuwawezesha wakulima kutumia utaratibu wa stakabadhi ghalani kuuza mazao yao.
Maghembe alikiri kwamba lipo tatizo la mazao ya chakula kusafirishwa kwa njia za magendo kwenda nje ya nchi, lakini alisema biashara hiyo inafanywa kwa vibali vya kughushi.
Aiitaja mikoa inayokabiliwa na njaa na idadi ya wilaya zake kwenye mabano kuwa ni Arusha (7), Dar es Salaam (3), Dodoma (1), Iringa (2), Kagera (2), Kilimanjaro (5), Manyara (2), Mara (4), Mbeya (1), Mtwara (1), Mwanza (5) na Pwani (2).
Mngine ni Shinyanga (7), Singida (2), Tabora (3) na Tanga (1). Hata hivyo, alisema wilaya 56 zinakabiliwa na hali tete ya ukosefu wa chakula.
Alisema kutokana na hali hiyo, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), inahamisha tani 115,000 za chakula cha ziada kilichopo kwenye maghala yake ya Sumbawanga, Makambako na Songea kwenda kwenye maeneo yanayokabiliwa na njaa katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Shinyanga.
"Hatua hii itawezesha serikali kukabiliana na upungufu wa chakula na mahitaji mengine ya soko kwa haraka zaidi…serikali inawahimiza wakulima wajiwekee akiba ya chakula katika msimu huu kwa ajili ya mahitaji ya kaya zao mpaka msimu ujao," alisema.
Waziri Maghembe alisema hali ya uzalishaji wa chakula nchini msimu wa mwaka 2010/11 haikuridhisha kwa kuwa kuna upungufu wa tani 413,740 za chakula.
Alisema chakula kinachovunwa sasa kinatazamiwa kuwa tani 6,786,600 wakati mahitaji ni tani 7,200,340.

No comments:

Post a Comment