KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Sunday 3 July 2011

Hatimaye Nahodha apata nyumba

Wengine waendelea kutesa hotelini







Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamshi Vuai Nahodha
Hatimaye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamshi Vuai Nahodha ambaye amekuwa akiishi hotelini kwa miezi nane sasa atahamia kwenye nyumba yake kuanzia wiki ijayo.
Habari tulizo nazo ni kwamba nyumba hiyo ambayo ilielezwa kuwa haikidhi, hivi sasa imekamilika kwa kiwango alichokuwa anataka yeye mwenyewe.
Awali, chanzo cha kuaminika kililiambia gazeti hili kwamba Nahodha alikataa kuhamia kwenye nyumba yake kwa maelezo kuwa haikuwa na hadhi ya Waziri Kiongozi mstaafu.
Kutokana na hali hiyo, serikali ililazimika kutumia mamilioni ya shililingi, kumlipia Nahodha chumba katika hoteli ya New Afrika, jijini Dar es Salaam.
Taarifa zilieleza kwamba Nahodha ameendelea kuishi hotelini kwa sababu nyumba haikuwa na samani za kutosha.
Chanzo hicho kikalidokeza gazeti hili kwamba pamoja na mambo mengine, Nahodha alikosa nyumba ya serikali kwa kuwa aliyekuwa anashikilia wadhifa huo, Laurence Masha, alikuwa akiishi nyumbani kwake.
Kutokana na hali hiyo, Wakala wa Ujenzi (TBA), ililazimika kumjengea Nahodha nyumba ambayo imekamilika lakini samani hazikutosheleza ukubwa wake.
Nahodha ambaye anaishi hotelini tangu Novemba mwaka jana baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, inaelezwa kwamba ameshindwa kukaa kwenye nyumba za mawaziri wa kawaida kwa kuwa alihitaji nyumba kubwa inayoendana na hadhi ya Waziri Kiongozi mstaafu.
Nahodha anaishi kwenye hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam, ambayo gharama ya chumba kwa siku ni kati ya dola za Marekani 140 na dola 160, kwa vyumba vyenye hadhi ya kawaida (standard) wakati vyumba vyenye hadhi ya juu (executive suite), ni dola za Marekani 280 kwa usiku mmoja.
Imedaiwa kuwa kutokana na nyumba aliyojengewa kutokuwa na samani za kutosha, Nahodha alilazimika kukaa hotelini mpaka mahitaji ya nyumba hiyo yatakapokamilika.
Msemaji wa Wizara hiyo, Isaac Nantanga, alipoulizwa na alisema kuna uwezekano wa Nahodha kuhamia kwenye nyumba yake, alisema yupo nje ya ofisi na kwamba hana taarifa za kina kuhusiana na suala hilo.
“Tuwasiliane Jumatatu ijayo ili niwe na taarifa za uhakika za kukupa…nipo nje ya ofisi kwa sasa,” alisema Nantanga.
Hata hivyo, pamoja na kwamba Waziri Nahodha anahamia kwenye nyumba yake wiki ijayo, uchunguzi unaonyesha kwamba bado Mawaziri kadhaa wataendelea kuishi hotelini.
Baadhi yao ni Naibu Waziri wa Maji, Gerson Lwenge anayeishi Abla Hotel apartments, zilizopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini pasi na shaka kwamba, Naibu Waziri huyo tangu ateuliwe kushika wadhifa huo hajapewa nyumba ya serikali.
Kutokana na hali hiyo, kiongozi huyo anaishi Abla ambako analipiwa dola 3,000 (sawa na Sh. 4,800,000), kila mwezi kama gharama ya pango la nyumba.
Utafiti umebaini kwamba Naibu Waziri huyo, ameishi Abla kwa takribani miezi mitano na hivyo amekwishatumia zaidi ya Sh. 60 milioni mpaka sasa. Kabla ya Abla, alikuwa anaishi kwenye moja ya hoteli ya kifahari jijini hapa.
Kwa mujibu Abla, gharama za apartment kwa mwezi zinatofautiana kulingana na siku ambazo mpangaji ataishi.
Inaelezwa kwamba ikiwa mgeni atakaa kwa siku moja ni dola za Marekani 250, kwa mwezi ni dola 3,000 wakati mgeni atakayeishi kwa miezi mitatu anapatiwa punguzo la dola 900 hivyo atalipa dola 8,100.

No comments:

Post a Comment