STARS YAWASILI GABORONE KUIKABILI ZEBRAS
Wachezaji
wa Taifa stars wakiwasili Gaborone
Kikosi
cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kikiwa na wachezaji 17 kimewasili
leo asubuhi jijini Gaborone tayari kwa mechi ya kirafiki ya kalenda ya
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya wenyeji Botswana
'Zebras' itakayochezwa kesho (Agosti 15 mwaka huu).
Stars imetua kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Sir Seretse Khama saa 5.45 leo asubuhi kwa saa za hapa
ambapo nyumbani ni 6.45 na kupokewa na
viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Botswana (BFA) na Watanzania wanaoishi hapa
Botswana.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa
Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura baadhi ya
wachezaji walioko kwenye kikosi hicho ni Frank Domayo, Ramadhan Singano na Simon
Msuva
ambao walijiunga na Stars saa chache baada
ya kurejea kutoka Nigeria ambapo walikuwa na timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro
Heroes) ambayo Jumapili ilicheza mechi ya mashindano ya Afrika dhidi ya Nigeria (Flying
Eagles).
Wachezaji wengine kwenye kikosi kilichoko
Botswana ni Aggrey Morris, Amir Maftah, Athuman Idd, Erasto
Nyoni, Haruna Moshi, Juma Kaseja, Kelvin
Yondani, Mrisho Ngassa, Mwadini Ally, Mwinyi Kazimoto,
Ramadhan Chombo, Salum Abubakar, Said
Bahanuzi na Shabani Nditi.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager imefikia kwenye hoteli ya Oasis ambayo pia ndipo
Zebras imepiga kambi kwa ajili ya mechi
hiyo. Mechi itaanza kesho saa 1 kamili usiku kwa saa za hapa na
itafanyika kwenye Uwanja wa Molepolole Sports
Complex. Uwanja wa Taifa wa Botswana hivi sasa uko kwenye matengenezo.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen
amesema mechi hiyo ni muhimu kwa vile timu yake bado
inakabiliwa na mechi za Kombe la Dunia Kanda
ya Afrika, na michuano ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji
wa Ndani
(CHAN) inayotarajia kuanza baadaye mwaka huu.
No comments:
Post a Comment