Kipaumbele cha Mvomero si jezi
Mb. Amos Makalla
Abdallah Khamis
JUZI nikiwa ninaangalia taarifa ya habari ya kituo kimoja cha televisheni, nilimshuhudia Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, ambaye pia ni Mbunge wa Mvomero, mkoani Morogoro, akigawa vifaa vya michezo kwa vijana katika mji mdogo wa Dakawa.
Hatua ya Makalla kurejea katika jimbo lake imechangiwa kwa kiasi kikubwa na moto wa Operesheni Sangara unaowashwa na CHADEMA katika Mkoa wa Morogoro huku kaulimbiu ikiwa ni Vuguvugu la Mabadiliko (M4C).
Kwa tafsiri yangu, Makalla amefanya tendo lile la kuwakusanya vijana wa mji wa Dakawa na kuwapatia vifaa vya michezo, akijaribu kuwahadaa vijana wale kwa vifaa hivyo kuiua ari ya kuzungumzia matatizo ya msingi yanayowakabili.
Aidha, hatua ya Makalla imekuja kipindi hiki ambacho CHADEMA inazidi kuwafumbua macho ikiwaonesha wakazi wa Morogoro namna wabunge wao wasivyowajibika kwao.
Nasema, Makalla ameshindwa kuwajibika katika jimbo lake kwa kudhani hitaji la kwanza la wananchi wa Jimbo la Mvomero, ni mipira na jezi ambavyo amewagawia.
Ameshindwa kuwajibika kwa kuwa, hakuweza kufika katika Kata ya Luale ambapo wananchi wake wanalazimika kuchimba miamba kwa ajili kutafuta barabara ya kuwawezesha punda wanaobeba wagonjwa kupita.
Makalla anadhani kipaumbele cha wakazi wa Mvomero ni jezi na mipira wakati hata hao vijana ikitokea wakiumia uwanjani watashindwa kupata huduma bora kutokana na kutokuwepo kwa wahudumu wa afya wa uhakika katika jimbo hilo.
Mfano hai ni katika Kijiji cha Kododo ambapo wanakijiji zaidi ya 3,000 wanalazimika kuhudumiwa na muuguzi mmoja wa zahanati ya hapo ambaye ndiye anayebeba jukumu la kuwa mwandishi wa vyeti vya wagonjwa, mpimaji, mtoa dawa na mshauri kulingana na wakati.
Mbunge huyu anasahau kuwa, katika jimbo lake kuna wananchi waliolazimika kuchimba miamba (magema) kwa zaidi ya kilometa 20 kwa ajili ya kutafuta barabara kwa ahadi ya kulipwa sh 5,000 kwa siku, huku fedha za maendeleo ya mfuko wa jimbo zikiwa hazijulikani zinafanya kazi gani.
Tatizo la Mvomero, si mipira, kwa kuwa hata vijana wa Kata ya Kichangani hawatakuwa na amani ya kucheza ikiwa hawajui hatima ya siku inayofuata kwa kuwa nyumba za wazazi wao zimeshawekwa alama ya kubomolewa, tena wakiwa hawajui watalipwa vipi licha ya barabara kuwakuta katika eneo hilo.
Makalla anatakiwa ajue tatizo la wakazi wa Kata ya Hembeti ambalo lipo jirani na eneo alilogawa mipira kuwa ni suala la ardhi baina ya wafugaji na wakulima, huku watendaji wakitumia fursa hiyo kujinufaisha kwa matatizo ya pande hizo mbili.
Watakuwa na raha gani wakazi wa Kitongoji cha Kododo waende kucheza mpira wakati wadogo zao wapatao 600 kuanzia elimu ya awali hadi darasa la saba wanafundishwa na mwalimu mmoja?
Kwa hakika wanamuona mbunge huyu hawezi kutimiza jukumu la kuwapatia elimu bora bali bora elimu kutokana na walimu kushindwa kwenda katika kijiji hicho kwa kukosekana miundombinu bora.
Kwa sababu ya kukata tamaa ya maisha, wakazi wa Kododo sasa hawajui jambo jingine lolote zaidi ya kulewa muda wote.
Makalla angetimiza wajibu wake ipasavyo, leo watoto wa watu wenye ulemavu wa ngozi katika Kata ya Luale, Kijiji cha Kekeo wasingefukuzwa shule kwa kukosa shilingi 70,000, wakati kuna mfuko wa kusaidia jamii ya watu wasiojiweza katika jimbo hilo inayopokea ruzuku serikalini, huku mbunge wao akiwa kimya.
Makalla hajui hatari inayowakabili ndugu zetu hao kwa kufanya kazi katika mazingira hatarishi, ikiwamo juani wanapolazimika kuchimba na kutengeneza barabara kwa mikono yao huku mfuko wa jimbo ukiwa haujulikani unatumikaje.
Kwa mtazamo wangu, kipaumbele cha Mvomero ni matatizo yao kutatuliwa na si naibu waziri na mbunge wao waliyedai kumuona kwa mara ya mwisho wakati wa kuomba kura, akiwaendea na jezi ambazo hata zikichafuka hawatakuwa na uwezo wa kuzifua kwa kushindwa fedha ya kununua sabuni kwa hali ngumu ya maisha
No comments:
Post a Comment