Tiketi Precision kwa M-Pesa |
Patricia Kimelemeta
KAMPUNI ya Ndege ya Precision air imeingia ubia na Kampuni ya Vodacom ili kuwawezesha abiria kuanza kununua tiketi za ndege za shirika hilo kwa kutumia M-Pesa.
Akizungumza na waandisi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kifedha cha Vodacom Tanzania, Innocent Ephraim, alisema kuwa ushirikiano huo ni mwendelezo wa uboreshaji wa huduma kwa wateja wao, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kupata wateja zaidi.
“Mteja atakayekata tiketi kwa kutumia njia ya M-Pesa, fedha zake zitakuwa salama, kwa sababu mteja ataweza kuweka na kutoa fedha zake bila ya matatizo yoyote, jambo ambalo litaweza kurahisisha shughuli zake,” alisema Ephraem.
Aliongeza ushirikiano huo utaweza kutoa njia mbadala ya malipo ya tiketi kwa muda mfupi na haraka, lengo ni kuleta mapinduzi katika huduma mbalimbali za kifedha tangu kuanzishwa kwake miaka minne iliyopita.
Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara cha Precision Air, Patrick Ndekana alisema kuwa makubaliano hayo ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi.
Alisema kutokana na hali hiyo wateja wa Vodacom kupitia huduma ya M-Pesa watawasiliana na kitengo cha huduma kwa wateja cha kampuni ya Precision Air ili waweze kununua tiketi hizo bila ya kufika kwenye ofisi zao, jambo ambalo linaweza kuwarahisishia upatikanaji wa tiketi hizo.
“Tumeingia ubia na Vodacom kwa ajili ya kununua tiketi za ndege kwenye mtandao wao, jambo ambalo tunaamini linaweza kurahisisha huduma za mawasiliano na kwamba wateja wenye haraka wataweza kupatiwa namba za tiketi zao kupitia simu zao za mikononi,” alisema Ndekana.
Aliongeza kutokana na hali hiyo anaamini kuwa, wateja wenye haraka ambao wanahitaji kusafiri huku wakiwa na muda mfupi watapata tiketi zao hata kama wanaishi kwenye maeneo ya mbali.
Alisema mpaka sasa kampuni hiyo ina wateja zaidi ya 900,000 ndani na nje ya nchi, hii inatokana na huduma bora ambazo zimesaidia wananchi wengi kutumia usafiri wa anga wa kampuni yao.
Alisema mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa, wanawafikia wateja wengi zaidi kwa kipindi kifupi ili waweze kuboresha utendaji wa shughuli zao, jambo ambalo litawasaidia kuongeza mapato.
|
No comments:
Post a Comment