Lowassa: Siungi mkono Kilimo Kwanza |
ASEMA HATA CCM INAJUA MSIMAMO WAKE, WAZIRI KABAKA ASISITIZA KILIMO NI LAZIMA, PROFESA LIPUMBA, MBATIA WAMSHANGAA
Peter Edson
WAKATI Serikali ikielekeza nguvu nyingi kutekeleza mkakati wa kuendeleza sekta ya kilimo nchini uliopewa jina la Kilimo Kwanza, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ameibuka na kusema haungi mkono mkakati huo.Alisema mkakati huo wa Kilimo Kwanza umekosa mashiko hivyo ili auunge mkono, kuna haja ya kubadili dhana yake na kuwa, elimu kabla ya kilimo kwanza.
“Ni vyema nikaeleweka hapa. Ninachomaanisha ni kuongeza elimu katika Kilimo Kwanza ili wananchi wawe na elimu kwanza ndipo waweze kuboresha kilimo,” alisema Lowassa.
Akizungumza katika Kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV juzi usiku, Lowassa alisema pamoja na Serikali kuwa na nia nzuri ya kumkomboa mwananchi kwa kuboresha mazingira ya kilimo, jambo hilo litakuwa si chochote kama hatapatiwa elimu itakayomwongoza kwenye mapinduzi hayo ya kijani.
“Mpango huu wa Kilimo Kwanza umekosa nguvu kwa sababu kuanzishwa kwake hakukuzingatia dhana ya ukombozi wa mwananchi wa kawaida. Tangu awali ndani ya chama (CCM) nilieleza kuwa sitaunga mkono hoja hiyo mpaka kuongezwe mashiko na kuwa Elimu Kabla ya Kilimo Kwanza,” alisema Lowasa na kuongeza:
“Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alitoa uamuzi mgumu na wenye busara, ndiyo maana kilimo cha pamba, kahawa, mkonge na mazao mengine vikaanzishwa. Hivyo ipo haja ya kufanyika mchakato wa kuona mbali zaidi ili viongozi wetu waweze kutoa uamuzi sahihi katika hoja hii ya Kilimo Kwanza, kwani nguvu nyingi pasipo elimu inaweza kuligharimu taifa.”
Alisema kuwa ili mwananchi wa kawaida aweze kunufaika na Kilimo Kwanza, anahitaji kupatiwa elimu ya kutosha ya namna ya kuandaa mazingira ya kilimo na uelewa wa vifaa na pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea na dawa.
Alisema pamoja na kuwa na mabwana shamba wachache, wananchi wamejikuta wakitumia mawazo yao kufanikisha miradi ya kilimo katika maeneo yao na matokeo yake wanapata mazao kidogo ambayo hayawakwamui kiuchumi.
Alitoa mfano wa nchi ya Indonesia akisema inaendesha uchumi wake kwa kilimo cha michikichi, ambayo mbegu zake zimetoka Tanzania... “Lakini Tanzania iliyotoa michikichi hiyo sasa ni moja ya wateja wa mafuta hayo yanayotoka Indonesia.”
Alishauri Serikali kuanzisha mashamba ya michikichi maeneo mbalimbali nchini kwa kuwa ardhi ipo ya kutosha hivyo kujitosheleza kwa mafuta hata ya kuuza nje.
“Ningelikuwa na uwezo wa kutoa uamuzi, vijana wetu wa JKT (Jeshi la Kujenga Taifa), ningewapa kazi ya kuanzisha mashamba ya michikichi nchi nzima kwani nchi yetu imejaliwa kuwa na ardhi kubwa na yenye rutuba, mapori yapo mengi,” alisema Lowassa.
Alisema wananchi wanaweza kupewa matrekta na pembejeo mbalimbali za kilimo, lakini bila kupewa elimu elekezi ya namna ya kuzitumia pembejeo hizo kuzalisha mazao bora, itakuwa kazi bure kwa kuwa ongezeko la mazao litakuwa dogo kama ilivyo kwa kilimo cha jembe la mkono.
Alitoa wito kwa Serikali kutumia fursa zilizopo za miradi ya kilimo kuwaelimisha Watanzania ili baadaye waweze kupewa au kukopeshwa zana za kilimo, akieleza kuwa nguvu kazi na elimu, ndivyo vitakavyomkomboa mwananchi katika umaskini wa kipato.
Kabaka: Kilimo lazima
Alipotakiwa kuzungumzia kauli hiyo, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka alisema kilimo ni lazima na Lowassa lazima akubaliane na mpango wa Serikali wa kutekeleza Kilimo Kwanza.
“Lowassa lazima akubaliane na msimamo wa Serikali wa kutekeleza Kilimo Kwanza. Kilimo ni lazima,” alisema Kabaka na kuongeza kuwa sekta hiyo ndiyo inayotoa ajira kwa watu wengi kuliko nyingine.
Alisema Tanzania ina wahitimu zaidi ya 800,000 wa elimu ya juu wa fani mbalimbali ambao moja ya ajira ambazo wanapaswa kujiunga nazo ni kilimo na hakuna ambaye anaweza kutafuta elimu akiwa na njaa... “Serikali itaendelea kusimamia Kilimo Kwanza na tunamtaka Lowassa atuunge mkono.”
Waziri huyo alisema Serikali haipuuzi elimu, lakini ukweli unabaki kuwa sekta ya kilimo ilisahaulika kitambo hivyo kupitia Kilimo Kwanza ukiacha ajira za wakulima wa kawaida, pia maofisa ugani wa kada mbalimbali wanaajiriwa.
“Hata huko kijijini huwezi kusema unampelekea elimu mtu ambaye ana njaa. Huwezi kueleweka, lakini tunajua watu wakishiba wataweza kufanya mambo mengine hivyo kauli yake kuwa kwanza ingetolewa elimu haina tija,” alisema.
Profesa Lipumba, Mbatia wamshangaa
Kauli hiyo ya Lowassa imeonekana kumkera mchumi maarufu nchini na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia. Kwa nyakati tofauti jana, viongozi hao wa vyama vya upinzani walihoji mamlaka ya kimaadili aliyonayo Lowassa ya kusema hayo.
Profesa Ibrahim Lipumba alimponda akisema anachofanya kada huyo wa CCM ni kujipapatua kisiasa kwani Kilimo Kwanza ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Profesa Lipumba alisema kauli hiyo ya Lowassa inaonyesha kana kwamba hafahamu vizuri mkakati huo wa Kilimo Kwanza hivyo ni bora akachukua muda kujifunza kabla ya kutoa kauli hizo.
Profesa Lipumba alisema katika kutekeleza Kilimo Kwanza, elimu pia hutolewa hivyo haiwezekani kusema kuwa itolewe kwanza elimu kabla ya kutekeleza mpango huo, kwa kuwa vyote vinakwenda pamoja.
“Huwezi kusema kuwa eti utoe elimu kwanza kisha ndiyo uanze utekelezaji. Hivi vyote vinatakiwa kwenda pamoja labda kasoro zilizopo ni kuwa Kilimo Kwanza kimewalenga wakulima wakubwa wakitarajiwa wawainue wadogo jambo ambalo haliwezekani,” alisema.
Alisema utekelezaji wa Sera ya Kilimo ni jambo jema kutokana na ukweli kuwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 10 iliyopita, wakulima wamesahaulika na kufanya ukuaji wa kilimo kuwa asilimia nne, kiwango ambacho ni cha chini kwa mahitaji ya ongezeko la watu ambalo ni wastani wa asilimia moja kwa mwaka.
“Kilimo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa lolote duniani na kitendo
cha kuwategemea wakulima wakubwa ni kasoro ambayo inapaswa kufanyiwa kazi katika utekelezaji wa mpango huu wa Kilimo Kwanza,” alisema Profesa Lipumba.
Mbatia alisema anamshangaa Lowassa kupingana na uamuzi wa chama chake kwa kuwa mkakati wa Kilimo Kwanza ulipitishwa na chama chake... “Lowassa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, hivyo Kilimo Kwanza ni uamuzi wa CCM. Anapingaje wakati hata alipojiuzulu alisema anafanya hivyo kulinda masilahi ya chama, leo anapinga mipango ya chama hichohicho?”
Alisema kama anaona haendani na mambo yanayofanywa na CCM ni vyema ajiondoe na kujiunga na chama kingine au kuanzisha chake ili awe na fursa nzuri ya kupinga kazi za chama tawala.
Ajira
Lowassa pia alizungumzia suala la ajira akisema viwanda vikifufuliwa vitanufaisha Watanzania wengi kwa kupata ajira na hivyo kuondoa dhana ya kuwepo kwa wahitimu wengi wa vyuo vikuu wasiokuwa na ajira.
“Unapotangaza kazi ya watu 20, barua za maombi ya kazi zinakuja 2,000, tusisubiri maandamano, tutatue tatizo hili sasa,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Hili suala linahitaji ufumbuzi wa haraka ingawa tumechelewa. Nilimshangaa sana yule waziri niliposema kuna shida ya ajira, akasema hakuna tatizo hilo.”
Tangu mwaka jana, Lowassa amenukuliwa na vyombo vya habari mara kadhaa akisema ukosefu wa ajira kwa vijana ni tatizo kubwa nchini, akilifananisha na bomu linalosubiri kulipuka ikiwa halitatafutiwa ufumbuzi.
Hata hivyo, Machi 21 mwaka huu, Kabaka katika mkutano na wanahabari alipinga kauli hiyo ya Lowassa akisema:
“Hali halisi ya ukuaji wa uchumi nchini ni nzuri lakini, haiwezi kuonekana kama wananchi wake ni maskini na hawana ajira. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kushughulikia suala hilo ikiwamo la kuhimiza uwekezaji nchini,” alisema Kabaka na kuongeza:
“Kitendo cha wanasiasa kuendelea kusema tatizo la ajira kwa vijana ni bomu linalosubiri kulipuka, siyo kweli na kudai Serikali haijafanya kitu wanakuwa hawaitendei haki. Tatizo limepungua kutoka asilimia 12.9 mwaka 2000/01 hadi asilimia 11.7, mwaka 2006.
Mbio za urais 2015
Alipotakiwa kueleza iwapo ana mpango wa kuwania urais mwaka 2015, Lowassa alisema suala hilo halipaswi kuzungumzwa sasa kwani linaweza kufungua uwanja wa malumbano.
“Waingereza wana msemo mmoja unaosema, ‘tutavuka daraja tutakapolifikia.’ 2015 bado ni mbali ukisema chochote sasa utafungua uwanja wa malumbano, tusubiri 2015 bado ni mbali,” alisema Lowassa.
|
No comments:
Post a Comment