Mwanasheria kizimbani kumiliki bastola bila kibali
20th August 2012
Mwanasheria wa kujitegemea Howard Msechu (25), mkazi wa Mbezi Beach, Dar es Salaam amefikishwa katika Mahakama ya Kinondoni kwa kukabiliwa na mashitaka mawili likiwemo la kumiliki bastola aina ya Wallter bila kibali.
Mwendesha Mashitaka Mratibu wa Polisi Mkimbu Ramadhani, alimsomea mshitakiwa shitaka la kwaza mbele ya Hakimu Amaria Mushi, kuwa Mei 29, mwaka huu katika maeneo ya Kimara, mshitakiwa alikutwa na silaha hiyo yenye namba za siri 141223 bila kuwa na kibali.
Katika shitaka la pili, alidai kuwa mshitakiwa alikutwa risasi tatu za silaha hiyo. Mshitakiwa alikiri makosa yote yaliyokuwa yanamkabili.
Hakimu Mushi alitoa hukumu ya kosa la kwanza kwa mshitakiwa huyo kuwa achague moja kati ya kufungwa jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh. 150,000.
Katika kosa la pili, Hakimu Mushi alimtaka mshitakiwa huyo achague kufungwa miezi sita au kulipa faini ya Sh. 20,000. Hata hivyo, mwanasheria huyo alikubali kulipa faini za makosa yote mawili.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment