KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Tuesday, 21 August 2012

Lowassa:     Sijaugua kiharusi

  Aeleza kinachomsumbua

  Atoboa kisa cha kukaa kimya

Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa
Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, amesema afya yake ni nzuri na kwamba, hajapata ugonjwa wa kiharusi, kinyume cha inavyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari, ambavyo amesema vimekuwa vikitumiwa na baadhi ya wanasiasa kueneza uwongo dhidi yake kwa misingi ya chuki za kisiasa na upotoshaji.


Pia alisema ameamua kukaa kimya kwa kuwa ukimya ni hekima kutoka kwa Mwenyezi Mungu.


Lowassa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Mbunge wa Monduli (CCM), alisema hayo wakati akihojiwa katika kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa na Televisheni ya ITV jana.


Alisema hajapata ugonjwa wa kiharusi isipokuwa matatizo ya jicho yaliyosababisha afanyiwe upasuaji miaka mitatu iliyopita.

“Lakini afya yangu namshukuru Mungu. Kama nilivyotoka Ujerumani, niliwaeleza waandishi wa habari kwamba, afya yangu ni nzuri, inaendelea vizuri. Sikupata stroke (kiharusi) yoyote.

Nimekuwa nikiwaambia niko check up kama kawaida,” alisema Lowassa na kuongeza:


“Niliwaeleza nina matatizo ya jicho kidogo. Nilifanyiwa operesheni miaka mitatu iliyopita. Kwa hiyo, huwa nakwenda kwa check up mara kwa mara. Lakini afya yangu ni nzuri.”


Hata hivyo, alisema kinachomshangaza ni kasi ya kuandika uwongo inayofanywa na baadhi ya vyombo vya habari juu ya afya za watu.

Alisema tabia ya Watanzania kutakiana mabaya, kama vile kumtakia mtu awe mgonjwa wakati hayuko mgonjwa, huku akijua kuwa anachokiandika ni uwongo ni tabia inayomsikitisha, kwani nchi haijawahi kuwa na utaratibu wa namna hiyo.

“Lakini nawashangaa sana wanaoandika that (hivyo). Lakini nataka kuwahakikishia Watanzania na wanaonitazama, afya yangu ni nzuri, namshukuru Mwenyezi Mungu, niko ‘fiti’ kwa jambo lolote,” alisema Lowassa.

Alipotakiwa kueleza uzoefu wake juu ya msingi wa Watanzania kutakiana mambo mabaya, kama vile magonjwa na vifo, badala ya kutakiana afya njema, Lowassa alisema:

“Mimi nadhani ni siasa za chuki tu. Chuki na upotoshaji. Kuna watu katika vyombo vya habari wanatumika na wanasiasa wenye nia zao na malengo yao. Kwa hiyo, wanaandika vitu ambavyo ni vya uwongo.”

Alisema kwa mfano, kama Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, aliwahi kuzungumza kuhusu kamati yake kuunga mkono kauli ya serikali kuhusu mgogoro wa Malawi.

Hata hivyo, alisema kauli yake ilipotoshwa na baadhi ya vyombo vya habari kwa kuandika kwamba, ametangaza vita na amekuwa Amiri Jeshi Mkuu, wakati madai hayo ni uwongo mtupu.

“Nilisema na napenda kurudia. Nilisema Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inaunga mkono kauli ya serikali kuhusu suala la mgogoro wa Malawi. Hatukutangaza kauli sisi. Kama wabunge hatuna kauli. Yenye kauli ni serikali. Na mwenye kauli ya mwisho ya kutangaza vita ni Amiri Jeshi Mkuu, ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano,” alisema Lowassa na kuongeza:

“Tunajua mipaka yetu. Lakini tumetangaza tu. Kwamba, sisi kama wabunge wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Tumeita vyombo vya dola. Tumeviuliza hali ikoje.


Wametueleza maelezo mazuri kabisa ya kuridhisha, ambayo tumewaambia Watanzania, tukazane sana, tuombee jambo hili, kadiri inavyowezekana tusifike kwenye vita.”


Alisema Watanzania wana historia ya vita, bado wanakumbuka namna walivyovamiwa na Nduli Idd Amin wa Uganda mwaka 1978.

Lowassa alisema kitendo hicho kiliilazimu Tanzania kuingia vitani, baada ya vita iliyomalizika mwaka 1979 kwa kutimuliwa kwa Amin nchini mwake, wananchi waliambiwa watafunga mikanda kwa miezi 18, lakini badala ya kuwa hivyo, ikawa miaka 18 ya tabu na adha tupu.

“Najua Watanzania wengi hawapendi vita. Lakini tuliwatahadharisha wenzetu wa Malawi kwamba, tuzungumze, tuzungumze, tuzungumze, tuelewane. Tusifike mahali, ambapo tukafika kwenye vita,” alisema Lowassa na kuongeza:

“Tukatumia mfano wa Wakatoliki. Wakatoliki wanapokuwa wanamchagua Papa .... hukaa ndani, wakaomba, wakasali mpaka moshi (mweupe) utoke. Na sisi tukataka mawaziri hawa wanaozungumza juu ya amani kati yetu na Malawi, wazungumze, wazungumze mpaka amani ipatikane.”

“Ila tulisema tunawatahadharisha Wamalawi, wasitufikishe mahali ambapo tukajaribu kutumia nguvu zetu za kijeshi. Tukasema tukifika hapo Watanzania watakuwa tayari kutetea mipaka yao kwa nguvu zote.”

“Kwa hiyo njia za kidiplomasia zizungumzwe, zizungumzwe. Tukishindwana sisi wenyewe kwa wenyewe, tutafute mtu wa kati wa kutusaidia. Lakini tusifikirie vita. Tukawataka Watanzania tuombee, tusifike kwenye vita, tufike mahali tuelewane.”

Alisema hata kama mgogoro huo utapelekwa ngazi za kimataifa,   Tanzania imejipanga vizuri katika kudai mipaka yake halali.

Lowassa alisema ni vigumu kuuhusisha mgogoro huo na rasilimali zinazoelezwa kuwamo kwenye Ziwa Nyasa lenye mgogoro.

Alisema Malawi ndiyo iliyoanzisha mgogoro huo baada ya kugawa vitalu vitano kwenye ziwa hilo kwa ajili ya kutafuta mafuta na gesi yanayosemekana kuwamo kwenye ziwa hilo.

Hata hivyo, alisema katika kugombea rasilimali hizo, mazungumzo yanawezekana, kwani nchi zote mbili ni maskini, hivyo wataelewana.

Machi, mwaka huu, Lowassa aliondoka nchini kwenda Ujerumani kwa matibabu, ambapo suala la afya yake lilizua mijadala kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, huku baadhi ikidai ana hali ni mbaya.

Aliporejea nchini, alizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, na kusema alikwenda Ujerumani kuchunguzwa tatizo la macho, lililokuwa likimsumbua.

Alisema kumekuwa na maneno mengi kuwa anaumwa, huku wengine wakisema ni mgonjwa sana, lakini akasema yote hayo ni uwongo.

Katika kuthibitisha kwamba hana tatizo lolote, Lowassa alikunja ngumi mbele ya waandishi wa habari na kunyoosha mikono yake huku akicheka, kuthibitisha kuwa yu bukheri wa afya.

Alifanya hivyo baada ya kuombwa na mmoja wa waandishi wa habari athibitishe kama yuko mzima wa afya.

“Niko vizuri, niko tayari kwa mapambano yaliyoko mbele yetu,” alisema Lowassa bila kufafanua ni mapambano gani.

AAMUA KUKAA KIMYA

Awali, katika kipindi cha Dakika 45 akijibu swali kuhusu kukaa kwake kimya muda mrefu, Lowassa alisema ukimya ni hekima kutoka kwa Mungu.

“Kwa hiyo, natumia nafasi hii kukaa kimya, kutojihusisha na masuala mengine, kunyamazia, kuangalia wenzangu waendelee na kazi bila kuwasumbua na kusema mambo ambayo yanaweza kuwakatisha tamaa,” alisema Lowassa.

TATIZO LA WAHAMIAJI HARAMU

Kuhusu wahamiaji haramu, alisema limekuwa ni tatizo kubwa nchini, hivyo akataka vyombo vinavyohusika na Watanzania kwa jumla kutoigeuza Tanzania kuwa shamba la bibi kwa kuacha kila mtu kuingia na kuishi nchini kienyeji na kuhoji sababu za Watanzania kuwa wakarimu kupindukia kwa watu wa aina hiyo.

Hata hivyo, alisema hapaswi kulaumiwa mtu, badala yake akasema ni jukumu la kila Mtanzania kuvisaidia vyombo vya dola ili viweze kuwabaini wahamiaji haramu, kwani wananchi ndiyo wanaowajua na kama binadamu hushirikiana na watu hao.
Chanzo gazeti Nipashe.

No comments:

Post a Comment