Mbowe: Tupeni madaraka kwa masharti
na Abdallah Khamis, Mvomero
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amewataka Watanzania kukiweka kando Chama cha Mapinduzi (CCM) na badala yake wakichague CHADEMA kwa masharti kwamba kikishindwa kusimamia masilahi yao nacho kiondolewe.
Alisema ni makosa makubwa kwa wananchi kufikiria kuwa CCM ndicho baba na mama yao, hivyo kuwataka wakinyime kura katika chaguzi mbalimbali kwa kuwa kimeshindwa kuwaondolea kero zao.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, alitoa kauli hiyo juzi jioni katika Kata ya Hembeti, jimboni Mvomero, mkoani Morogoro, alipozuiliwa kwa muda na wananchi wakitaka awahutubie.
Alisema kuwa kwa sasa wananchi wanapaswa kuachana na CCM badala yake wakichague CHADEMA lakini akaweka bayana kuwa endapo nacho kitashindwa kusimamia masilahi yao, kiwekwe pembeni.
“Mimi Mbowe leo nikiona CHADEMA haiendani na mahitaji ya wananchi na kushindwa kuongoza, sitakuwa na sababu ya kuendelea kuwa mwana-CHADEMA, sasa ninyi mnang’anga’nia CCM kwa nini?” alihoji huku akishangiliwa na wakazi hao.
Mbowe alipita eneo hilo akitokea mjini Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao vya Bunge, akielekea Kata ya Mtibwa mkoani humo, kuungana na viongozi wenzake katika operesheni ya vuguvugu la mabadiliko ( M4C) ndipo akazuiliwa kwa muda katika Kata ya Hembeti ambako kulikuwa na mkutano wa chama hicho.
Mkutano huo ambao ulikuwa ukihutubiwa na Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar, Hamad Yusuph, ulisimama kwa muda huku wananchi wakizuia gari la Mbowe lisiendelee na safari wakitaka awahutubie.
Hali hiyo ilimlazimu kada wa chama hicho, Arcado Ntagazwa, aliyekuwa akihutubia kumpa kipaza sauti Mbowe kwa ajili ya kusalimia umati huo.
Akihutubia mkutano huo, Mbowe alisema kuwa dhamira ya CHADEMA kuwapo mkoani Morogoro ni kuwaondoa wananachi wa mkoa huo katika wimbi la usingizi wa kuishabikia serikali ya CCM aliyodai imeshindwa kutatua matatizo ya msingi ya nchi.
“Tunapita kila kata ya Mkoa wa Morogoro kujenga mtandao wa chama bila kujali dini, kabila wala rangi, ujumbe wangu kwa wana-Hembeti ni kujua wajibu wa chama cha siasa ni kupata viongozi na sera mbadala zitakazowezesha nchi kusonga mbele,” alisema Mbowe.
Mbowe aliongeza kuwa serikali ya CCM imeshindwa kuwatoa watu katika matatizo na kuwapeleka katika neema huku akiwataka wakazi hao kutafakari miaka 50 ya Uhuru imewafikisha wapi.
Alisema kuwa Mkoa wa Morogoro umefunga ndoa na CCM, hali inayowafanya wasiwe na sauti ya moja kwa moja hadi matatizo yao yaongelewe na wabunge wa vyama vya upinzani kutoka maeneo mengine.
“Tunawaunganisha wana CCM, CUF na vyama vingine na wengine katika kuikomboa Tanzania, tunawaomba msiwacheleweshe wakazi wa mikoa mingine katika kusonga mbele kwa kuwa ninyi mmefunga ndoa na Chama cha Mapinduzi,” aliongeza.
Naye Ntagazwa, akihutubia katika vijiji vya Kambala, Hembeti na Mkindo kunakokaliwa na jamii ya wafugaji na wakulima, alisema migogoro ya ardhi nchini inakuzwa kwa makusudi na watawala kwa vile wana masilahi nayo.
Alisema watendaji na watawala wa serikali ya CCM badala ya kuwakutanisha wakulima na wafugaji kwa ajili ya kuondoa tofauti zao wao hutumia fursa hiyo kuchukua fedha kwa mmoja wao na kisha kuacha uhasama miongoni mwa wafugaji na wakulima.
“Msidhani matatizo yenu yanashindwa kutatuliwa ila huo ni mradi wa watu kwa maana leo ng’ombe wa mfugaji akiingia katika shamba la mkulima na akapelekwa kwa mtendaji kwa ajili ya kulipwa fidia, mtendaji anachukua fedha kwa mfugaji na mkulima, hali inayomfanya mfugaji aendelee kuwa na kiburi cha fedha na mkulima awe na uchungu wa kuharibiwa mali yake,” alisema Ntagazwa.
No comments:
Post a Comment