KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Wednesday, 22 August 2012

Posho ya sensa yazua balaa tupu Malampaka

Mikutano inayoendelea ya kuhamasisha zoezi la sensa kwa viongozi wa ngazi ya kijiji hadi tarafa katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imeingia dosari kufuatia kuzuka kwa vurugu katika vituo vya Malampaka na Lalago kutokana na madai ya posho.

Hali hiyo imebainika wilayani hapa katika maeneo hayo  na kuwepo kwa vurugu hizo zinatokana na viongozi kuelezwa kuwa hakuna posho ya kuwalipa.

Kitendo hicho kimepingwa na kusababisha karatasi ya mahudhurio waliojiorodhesha kuchanwa chanwa mbele ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Maswa, Danford Peter.

Tukio hilo lilitokea katika kituo cha Lalago ambapo mkutano pamoja uliopangwa ufanyike katika uwanja wa ofisi ya mtendaji wa kata ya Lalago, ulishindwa kufanyika baada ya wajumbe kuwataka maafisa wa timu ya sensa wa wilaya hiyo kuwapatia kwanza posho yao.

Wakizungumza kwa jazba, walisema serikali imeshindwa kuwathamini kwa kipindi kirefu lakini yanapotokea mambo ya msingi, huamua kuwashirikisha lakini bila kuwalipa stahili zao huku wenyewe wakijilipa posho ya kufanya mikutano hiyo.

"Serikali kwa muda mrefu imeshindwa kututhamini sisi wenyeviti wa vitongoji, sasa leo ndiyo wanaona umuhimu wetu.
Hatuwezi kutumika kama dodoki kuwasafishia wengine halafu siye tubaki hivi hivi huku wao wakijilipa posho," alilalamika Masanja Nungwa, mkazi wa kijiji cha Mwadila.

Walisema viongozi hao ndiyo watakaoharibu  zoezi la sensa wilayani humu kwani malalamiko ni mengi na kwa asilimia kubwa zoezi hilo limegubikwa na vitendo mbalimbali vikiwemo vya rushwa, ubinafsi na uchakachuaji.

Walisema hawaamini kuwa serikali haina fedha za kuwalipa isipokuwa ni mwendelezo wa vitendo vya ufisadi ambao umekuwa kila mara ukifanyika kwa viongozi waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi.

Akizungumzia hali hiyo iliyojitokeza katika kituo cha Lalago, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Danford Peter, alisema zoezi hilo linachanganywa na mambo ya kisiasa.

Na katika mkutano mwingine wa tarafa ya Sengelema uliofanyika katika mji mdogo wa Malampaka, kulizuka vurugu baada ya wajumbe hao kuelezwa kuwa hakuna posho ya kuwalipa.

Hali hiyo ilimlazimu Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Luteni mstaafu Abdallah Kihato, kuwaomba radhi wajumbe kwa kitendo hicho.

Mikutano hiyo inawashirikisha wenyeviti wa vitongoji, watendaji wa kata na vijiji,viongozi wa sungusungu na wazee maarufu.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment