CHAMA cha Wananchi (CUF), kimedai kushangazwa na kauli iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye kwa vyombo vya habari kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeingia mikataba ya kifisadi na wafadhili wa nje ili kupora rasilimali za nchi.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaama jana na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Bw. Abdul Kambaya, alisema Bw. Nnauye hakupaswa kuishtaki CHADEMA kwa wananchi bali kupitia Serikali yao walipaswa kuzuia fedha hizo na kuwataja wafadhili hao, “CUF kimeshangazwa na kauli hii ambayo imetolewa na msemaji wa CCM, ambacho ndio chama kinachoongoza nchi, tulitarajia Bw. Nnauye angewataja hao wafadhili wa CHADEMA ambao dhamira yao ni kupora rasilimali za nchi,” alisema Bw. Kambaya.
Aliongeza kuwa, chama hicho kinaamini CCM na CHADEMA ni watoto wa familia moja ambapo wafadhili wao ndani na nje ya nchi pia wa aina moja, “Kama CHADEMA imeingia mikataba ya kupewa mabilioni ili baadae wataposhika madaraka waweze kulipa mabilioni hayo kupitia rasilimali za nchi basi watakuwa wanaendeleza utaratibu wa CCM kuingia mikataba mibovu isiyo na tija kwa Watanzania,” alisema.
Alisema CUF inaamini kuwa, tatizo lililopo nchini ni mifumo mibovu inayoendesha Serikali, nchi, kukithiri kwa wizi, matumizi mabaya ya fedha za umma na ukiukwaji wa haki za binaadamu.
Bw. Kambaya alisema, sababu ya Watanzania wengi kuwa maskini wa kutupwa, ukosefu wa huduma bora kwa jamii, kudumaa kwa maendeleo ya nchi na ukosefu wa ajira ni matokeo ya muda mrefu yanayosababishwa na mfumo mbovu uliopo.
Alisema njia sahihi ya kulinda rasilimali zilizopo na zinazoendelea kugunduliwa nchini Serikali ya Umoja wa Kitafa ambayo itashirikisha vyama vyote vyenye wabunge.
Aliongeza kuwa, kwa kuzingatia utaratibu huo hakuna chama ambacho kitakuwa na maamuzi yake katika matumizi ya rasilimali na Maliasili za nchi, “Sisi tunataka Watanzania waelewe kuwa, mazingira yanaonesha CHADEMA kimeizidi kete chama tawala kwa kuwa na wafadhili wa nje ndio maana CCM Inapiga kelele,” alisema.
---
No comments:
Post a Comment