KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Friday, 17 August 2012


 
Picture
George Kayala na Haruni Sanchawa

TUKIO la mwanamke Rehema Nungu kukutwa ameteketea kwa moto ndani ya gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T 883 BLA katika msitu wa Mabwepande, jijini Dar Agosti 1, 2012 linazidi kugusa akili za wengi hasa kutokana na utata wa tukio lenyewe na hii ndiyo ripoti kamili.

Taarifa zilizopenyezwa na ndugu mmoja wa Simon Sakilu ambaye ni mume wa marehemu, zinadai kuwa kabla ya tukio hilo, Rehema na mumewe walikuwa kwenye ugomvi mzito usiokuwa na dalili ya kumalizika.

MAELEZO YA UPANDE WA MWANAUME

Habari zinadai kwamba marehemu alikuwa akidaiwa fedha na mfanyabiashara mmoja (hakutajwa jina) lakini mumewe hakulijua deni hilo mpaka siku za mwisho za uhai wa Rehema ambapo hata hivyo hakumuuliza.

Aidha, ikadaiwa kwamba mfanyabiashara huyo alikuwa akimdai marehemu kwa vitisho kwamba asipolipa atamwambia mumewe, jambo ambalo mwanamke huyo hakutaka litokee.

Siku ya tukio, habari zinadai kuwa marehemu aliamka mapema na kufanya shughuli za nyumbani na baada ya muda inadaiwa alikunywa sumu ambayo haikujulikana ni ya aina gani.

Ikazidi kudaiwa kuwa baada ya kitendo hicho, mumewe alifanya juhudi za kumnywesha  maziwa ili kuokoa uhai wake lakini ilishindikana kufuatia mke kumzidi nguvu mumewe na kukimbilia kwenye gari na kuondoka nyumbani kwenda kusikojulikana.
 “Mwanamke alipokunywa sumu, mumewe (Simon) alifanya juhudi za kumpa maziwa ili kuokoa maisha yake lakini alizidiwa nguvu, mke akatoka na gari na kwenda kusikojulikana.

“Simon alikwenda kukutana na mdai wa mkewe na kumlipa fedha zake akiamini mkewe alikunywa sumu kwa sababu ya deni, baada ya malipo akampigia simu mkewe ili kumtaarifu lakini simu hiyo ilikuwa inaita na kukatika, baadaye haikupatikana kabisa,” alisema ndugu huyo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake gazetini.

Kuanzia hapo, ndugu walianza kumsaka Rehema mpaka Agosti 2 mwaka huu habari zilipopatikana habari  kwamba kuna gari limekutwa limeteketea kwa moto kwenye msitu wa Mabwepande. Mtu aliyedaiwa ndiye alikuwa dereva naye alikuwa ameungua na kubaki majivu na fuvu likiwa sehemu ya kiti.

Hata hivyo, ndugu hawakutaka kuweka msiba wakiamini aliyefariki dunia kwa moto huo anaweza asiwe Rehema. Ili kujiridhisha na hilo, walichukua mabaki hayo na kuyapeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa vipimo vya DNA.

MUME ANA SIRI NZITO?

Habari zaidi kutoka ndani ya familia hiyo zinadai kuwa huenda Simon ana siri nzito juu ya kifo cha mkewe Rehema kwani haingii akilini mume kuzidiwa nguvu na mkewe wakati wa kumsaidia kumnywesha maziwa.

Aidha, mpenyesha habari huyo aliendelea kufunguka kwamba ilikuwa ni kawaida kwa wanandoa hao kutibuana na mke kwenda anakojua hata kwa siku tatu bila mwanaume kujishughulisha kumtafuta.

MAELEZO UPANDE WA MWANAMKE

Agosti 6, 2012  mapaparazi wetu walifika nyumbani kwa marehemu Rehema, Mbezi Beach, Dar na kukuta watu wachache ikidaiwa hali hiyo ilitokana na wengi kutoamini kama Rehema alifariki dunia. Mume wa marehemu hakuwepo msibani hapo bila kujulikana alikokwenda.

Alipotafutwa ndugu wa marehemu kuzungumzia suala hilo, kila mmoja aliruka na kudai mwenye uwezo wa kuzungumzia jambo hilo ni mama mzazi ambaye naye aligoma kusema lolote.

“Mwenye uwezo wa kuzungumzia suala hilo ni mama mzazi lakini amegoma kwa madai kuwa hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa vile  anahisi kuna mchezo mchafu umefanyika,” alisema ndugu mmoja.

Hata hivyo, mtu mmoja wa karibu na familia ya marehemu alisema kuwa habari kamili juu ya msiba huo zitapatikana mara baada ya kupata vipimo kutoka kwa mkemia mkuu kubaini kama kweli aliyekutwa ameteketea kwa moto ndani ya gari ni Rehema.

“Ni vigumu kulizungumzia suala hili kwani linatatanisha, unaweza kusema aliyekufa ni Rehema na matokeo ya mkemia mkuu yakitoka yakaonesha tofauti, inaweza kuleta shida, tusubiri majibu kwanza,” alisema mtu huyo bila kutaja jina lake.

MAJIBU YA MKEMIA MKUU YATOKA

Agosti 10, 2012 mmoja wa ndugu wa marehemu alimpigia simu mwanahabari wetu na kumweleza kuwa majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali yametoka na kubaini kwamba aliyekufa ni Rehema Nungu.

“Kama unavyosikia vilio hivyo, nipo msibani, majibu ya mkemia mkuu yamebaini aliyekufa ni Rehema Nungu, taratibu za mazishi zinafanywa sasa ila naomba muende nyumbani kwa Simon mtapata habari kamili,” alisema ndugu huyo na kusisitiza kuwa kama msiba utafanyika kwa mume wa marehemu, hawatakwenda ila watakwenda makaburini tu.

NYUMBANI KWA SIMON

Baada ya kupata taarifa hizo, waandishi wetu walifika nyumbani kwa Simon, Tegeta Nyuki, Dar na kumkuta msemaji wa familia hiyo aliyejulikana kwa jina moja la Dedu.

Dedu alipopewa pole ya msiba na kutakiwa kueleza sababu za kifo cha marehemu, alisema waulizwe polisi yeye hawezi kusema chochote licha ya kukutwa na picha ya marehemu mkononi.

“Siwezi kusema chochote, kamuoneni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ana habari zote za msiba huu, naomba mniache niendelee na taratibu za hapa,” alisema Dedu.

KAMANDA WA MKOA WA PWANI

Agosti 10, 2012 mwandishi wetu alitinga katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu kwa lengo la kujua chochote kuhusu kifo cha mwanamke huyo lakini hakuwepo, ikabidi apigiwe simu yake ya kiganjani ambapo alikuwa na haya ya kusema:

“Ni kweli majibu ya tukio hilo yametoka, mtu aliyeteketea kwa moto ndani ya gari ni Rehema lakini sipo katika nafasi nzuri ya kuongea kwani niko Muhimbili nashughulikia majeruhi wa ajali ya wanakwaya wa kutoka Kenya.

“Hata kesho (Agosti 11) sitakuwa ofisini kwani nitakuwa bado nashughulikia suala hilo, waliofariki ni raia wa nje hivyo ni vyema nikahakikisha wanasafirishwa kurudi kwao,” alisema Kamanda Mangu.

UTATA

Asubuhi ya Agosti 11, 2012, wanahabari wetu walidamkia nyumbani kwa Simon ili kutaka kujua taratibu za mazishi.

Nje ya nyumba alikuwepo Dedu na mzee mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake, akasema yeye ni makamu mwenyekiti wa kamati ya mazishi. Wawili hao waligoma kuongea chochote kwa madai yaleyale, suala liko polisi.

Hata hivyo, muda huohuo simu ya Dedu iliita, alipopokea ilionekana kupigwa na ndugu mmoja wa marehemu ambaye alisema mazishi ya mabaki ya mwili wa Rehema (fuvu na majivu) yangefanyika Jumamosi au Jumapili iliyopita lakini baada ya kupata kibali kutoka kwa mkemia mkuu.

Baadaye habari kutoka ndani ya familia ya Rehema zilisema kibali cha kuzika masalia ya mwili wa marehemu kilikuwa kipatikane jana Jumatatu.

Marehemu Rehema ameacha watoto wawili, Ngimba na Muheri.

---
via globalpublishers.info 
Picture
Marehemu, Rehema Nungu enzi za uhai wake (picha: GlobalPublishers.info)


No comments:

Post a Comment