Chadema chatumia kitabu cha Makamba mikutano ya M4C
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanza kutumia katika mikutano yake kitabu kilichotungwa na Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba, kinachoeleza sababu za Tanzania kuwa masikini licha ya kuwa na utajiri mwingi wa rasilimali.
Kitabu hicho kiitwacho Makatazo ya Rushwa kwa Mujibu wa Biblia na Quran tukufu, kimekuwa kikitumiwa na Chadema katika operesheni yake za Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) mkoani hapa, kunukuu baadhi ya vipengere vinavyo kataza rushwa tendo ambalo limekuwa likipigiwa kelele na viongozi wa chama hicho kwa madai kuwa nchi imefika hapa ilipo kwa sababu ya rushwa.
Akizungumza katika mikutano ya M4C iliyofanyika katika vijiji mbalimbali vya majimbo ya Morogoro Mashariki na Morogoro Kusini mkoani hapa, mmoja wa makamanda Chadema ambaye aliwahi kushika nyadhifa za uwaziri na naibu waziri kwa miaka 15 na mbunge kwa zaidi ya miaka 25, Arcado Ntagazwa, alisema kitabu cha Makamba kimeeleza vizuri juu ya tatizo la rushwa lakini anashangazwa na kitendo cha serikali ya CCM kushindwa kuendesha nchi kwa uadilifu.
Alidai kuwa aliamua kuihama CCM kutokana na kushindwa kukomesha rushwa na kushindwa kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.
Alisema Yusuph Makamba amekuwa kada na kiongozi wa CCM kwa miaka mingi na alitunga kitabu hicho mwaka 2008 akiwa bado na nyadhifa kubwa ndani ya chama hicho ikiwa ni pamoja na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa, Katibu Mkuu na mjumbe wa Kamati Kuu, lakini bado chama chake kinanyooshewa kidole kwa baadhi ya viongozi wake kushiriki katika rushwa.
Ntagazwa alidai kuwa, serikali ya CCM imeshindwa kudhibiti rushwa nchini na hicho ni kielelezo kuwa imeshindwa kuwahudumia wananchi kwa uadilifu.
Alisema kuwa licha ya kitabu hicho kutengenezwa na kada wa CCM, lakini wana-CCM wameshindwa kuyatatua.
No comments:
Post a Comment