KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday, 30 August 2012


 
Kutoka kwenye gazeti la MTANZANIA  -- BAADA ya kufanyika kwa uchunguzi wa kitabibu kuhusu kifo cha mfuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ally Zona, matokeo ya madaktari yamebaini jeraha lililosababisha kifo chake limetokana na kugongwa na kitu kizito na si risasi kama ilivyokuwa inadaiwa.

Tukio hilo lilitokea Agosti 27, mwaka huu mjini Morogoro, wakati polisi wakitawanya maandamano ya wanachama wa chama hicho wakitokea eneo la Msamvu Lupila kuelekea Viwanja vya Fire kulikofanyika mkutano huo ambapo awali yalikatazwa na jeshi hilo.

Akieleza matokeo ya uchunguzi huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alisema jeraha hilo la marehemu lililokuwa kichwani lilitokana na kugongwa na kitu kizito kilichorushwa na si risasi kama ambavyo watu walikuwa wakidhani.

Alisema uchunguzi huo ulifanywa na madaktari wawili wa mkoani hapa pamoja na Dkt. Ahmed Makata kutoka Dar es Salaam na kushuhudiwa na mwanasheria wa CHADEMA, Amani Mwaipaja, pamoja na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi.

Alisema baada ya matokeo hayo ya daktari, polisi sasa wanaendelea na uchunguzi wa kubaini kitu hicho kilichorushwa na kusababisha kifo cha mfuasi huyo.

Alisema baadaye watachukua hatua za kisheria kwa askari ama mtu mwingine atakayebainika kuhusika kurusha kitu hicho, ikiwa ni pamoja na kumkamata mtu ama kiongozi wa chama hicho aliyechochea ama kuandaa maandamano hayo yaliyozua vurugu.

Alisema katika kubaini mwenendo mzima wa tukio hilo, Serikali imeunda tume ya kuchunguza ambayo inahusisha askari polisi na watu wengine watakaosaidia kukamilisha uchunguzi huo.

Hata hivyo, alisema tume hiyo ambayo tayari imeshafika mkoani hapa, itatafuta maelezo na ushahidi kutoka kwa watu mbalimbali walioshuhudia tukio hilo, wakiwamo wanahabari na kuwaomba wote watakaohitajika kutoa ushirikiano.

Akielezea kuhusu majeruhi, Hashimu Seiph, aliyejeruhiwa mguu katika vurugu hizo, alisema uchunguzi umebaini kuwa alijeruhiwa na bomu lililomuangukia mguuni na anaendelea vizuri na bado yuko Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa ajili ya matibabu zaidi.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa CHADEMA, Aman Mwaipaja, ulikiri kupokea taarifa ya matokeo ya uchunguzi wa madaktari hao na kusema wanafanya mawasiliano na viongozi wakuu wa chama hicho kuona hatua gani zitachukuliwa.

Alisema kwa sasa anafanya mawasiliano na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Wilbroad Slaa, aweze kumpatia taarifa hiyo na hatua zozote zitakazochukuliwa zitatolewa taarifa kwa vyombo vya habari.

Alisema mwili wa marehemu huyo unatarajia kusafirishwa baada ya familia kukaa na kupanga siku ya mazishi mkoani Tanga na mazishi hayo yatahudhuriwa na baadhi ya viongozi wa CHADEMA mkoani Tanga na wengine.


No comments:

Post a Comment