Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe akichangia kwa hisia katika semina ya wabunge juu ya fao la kujitoa, kwenye ofisi za bunge mjini  Dodoma  leo.
Na. Mwandishi wetu-Dodoma.
 Wabunge  wa bunge la Tanzania wamegawanyika katika semina yao juu  ya fao la kujitoa  katika mifuko  ya hifadhi ya jamii  ambapo wabunge wengi vijana wanataka mifuko hiyo irudishe sheria ya kujitoa wakati mawaziri na baadhi ya wabunge wengine wanakataa kurudishwa kwa fao hilo.
 Kuna hoja zingine za wabunge zinazotaka  sheria ya fao la kujitoa lisiwepo na  badala yake kuwepo fao lingine la kujikimu kwa wanachama wanaoachishwa kazi wakati wakisubiri umri wao wa kupata fao la kujitioa.
 Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zito Kabwe (Chadema)  amesema kuwa kwa sasa  fedha nyingi za mifuko ya hifadhi ya jamii zinatumika vibaya kwa kisingizio cha uwekezaji na masuala mengine  yanayofanana na hayo na kusababisha hofu kubwa  ya uwezo wa mifuko hiyo  kuwalipa wanachama wake hapo baadaye.
 Amesema kuwa yeye hatakuwa tayari kuona kuwa mifuko hiyo haina fedha ya kuwalipa wanachama wanaofikisha umri wa kupata fao la kujitoa, endapo kama atakuwa Rais wa nchi  yetu ya Tanzania .
 Zito amesema kuwa hata kama siye yeye atakuwa Rais wa Tanzania miaka ijayo,  laikini hatapenda kuona mtu yeyote atakayekuwa Rais akishindwa kuwalipa mafao wanachama wa mifuko hiyo.
 Usemi wa Zitto ulileta minong’ono kutoka kwa wabunge na Spika aliyekuwa anahudhuria semina hiyo katika ukumbi wa zamani wa Bunge kwa sasa unaitwa ukumbi wa Pius Msekwa.