Madudu ya TANESCO haya
• Mbunge aiuzia matairi mabovu
na Mwandishi wetu, Dodoma
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, jana aliibua madudu
mengine ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambapo ilinunua misumari kwa
pauni 50,000 badala ya spea.
Muhongo aliongeza kuwa baadhi ya wabunge wakiwamo wale wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wanafanya biashara na TANESCO, ambapo
kampuni ya mbunge mmoja ililiuzia shirika hilo mataili mabovu.
Waziri huyo aliibua madudu hayo alipokuwa akijibu hoja za wabunge
waliochangia hotuba ya bajeti yake kwa mwaka 2012/2013 ambapo alisema serikali
haitasita kuiingilia TANESCO pindi inapobaini mambo hayaendi sawa.
Alisema kuna taarifa za siri kutoka kwa wabunge watatu kuwa biashara ya nguzo
imekuwa ikifanyiwa mchezo mchafu kwa kuchukuliwa mkoani Iringa na kupelekwa
Afrika Kusini na kisha kurejeshwa hapa nchini na kuuzwa bei kubwa.
Aliongeza kuwa TANESCO ina madudu mengi na wamemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi ndani ya shirika hilo.
“Waheshimiwa wabunge naomba tumwachie CAG afanye uchunguzi kama
tulivyomuagiza na habari za kamati teule tuachane nazo na kufunga mjadala huu
hata kwenye vyombo vya habari tuchape kazi,” alisema.
Waziri Muhongo alianza kujenga hoja zake akinukuu kauli mbili za mwanafalsafa
na mwandishi wa habari mkongwe kuwa; “Ukweli ni tochi au kurunzi ndani, hivyo
kadiri unavyoitingisha ndivyo inavyowaka” na “Ukitaka kujua mafanikio ya
kiongozi yeyote aliyefanikiwa ni kutazama yale
ya wenzake waliyoyaacha.”
Katika hilo aliweka bayana kuwa mtu yeyote anayeitetea TANESCO au wale wote
wanaowaumiza wananchi ni mpuuzi, kwa vile shirika hilo limekuwa likifanya kazi
tangu mwaka 1930 lakini kwa miaka yote hiyo wameshindwa kusambaza umeme kwa
asilimia 20.
“Anayedhani TANESCO haitaingiliwa anajidanganya tu. Hii ni ajabu, maana
hatuwezi kuchukua vyanzo vya mapato ya serikali kwenye bia kila mwaka badala ya
TANESCO,” alisema.
Kuhusu kuunda tume kwa mambo ambayo yanakuwa yametokea ndani ya wizara yake,
Waziri Muhongo alisema utaratibu mpya anaoupendekeza sasa ni ule wa watendaji
pamoja na yeye kwenda eneo husika na kukutana na wananchi kusikiliza (public hearing).
Tuhuma za Mhando
Kuhusu tuhuma zinazomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, William
Mhando, alisema kuwa amesimamishwa kupisha uchunguzi wa matumizi mabaya ya fedha
na madaraka.
Alizitaja tuhuma zinazomkabili Mhando kuwa ni pamoja na kukiuka sheria ya
maadili ya umma kwa kuingia mkataba wa kutoa mkopo wa sh milioni 884.5 kwa
kampuni ambayo ana masilahi nayo, kwani mkewe Eva ndiye mkurugenzi, na watoto
wao wawili (Veronica na Fredy).
Kuhusu hofu ya kuwapo kwa mgawo wa umeme, Waziri Muhongo alisema kuwa
ilikuzwa tu na mafaisadi kwa kupitia mawakala wao lakini akabainisha kuwa
shirika linao uwezo wa kutosha kuzalisha umeme.
Ni katika mlolongo wa hujuma hizo, waziri alibainisha kuwa madai ya kwamba
wizara ilikiuka kanuni ya manunuzi ya umma kwa kuipa mkataba Kampuni ya PUMA
Energy wa kusambaza mafuta kwa Kampuni ya IPTL kwamba si za kweli.
“TANESCO haikuwa na fedha, vile vile mafuta, lakini ilitaka iweke masharti
kwa kampuni ya kuisambazia mafuta. Siku wanapoweka mgawo hawakunipa taaarifa
wala wasaidizi wangu. Watu hao
hao waliokata umeme kwa kusingizia kukosa mafuta nilikwenda ofisini kwao kesho
yake nikitokea Dodoma, lakini nikakuta bado hawajanunua mafuta,” alisema.
Prof. Muhongo alifafanua kuwa fedha walizowapatia TANESCO hazijaingilia
utaratibu kwani hawakuingia huko kuwashawishi waipe zabuni PUMA Energy.
Alisema kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na serikali kwa asilimia 50, hivyo
kununua mafuta kwake wanapata unafuu na gawiwo la hisa, lakini pia walibaini
ujanja kwamba hata kampuni iliyokuwa ipewe zabuni ya kuuzia mafuta TANESCO kwa
sh 1,800
kwa lita, nayo inayanunua kwa PUMA Energy kwa bei ndogo ya sh 1,460.
“Tumepata barua ambayo tungeitumia kama nondo ya kutuokoa humu ndani kama
wabunge msingeshutukia mchezo uliokuwa ukifanyika dhidi yetu. Hii ndiyo
ingetuokoa maana inaonesha kuwa kwa vile IPTL ipo chini ya mufilisi, mkataba
unabainisha wazi kuwa Wizara ya Nishati na Madini ndiyo yenye mamlaka ya
kuinunulia TANESCO mafuta,” alisema.
Kuhusu Bodi ya TANESCO nayo kuvunjwa kutokana na kukosa uhalali wa kimaadili,
waziri alisema wanaelekea huko na hivyo kubainisha kuwa hata wajumbe wake
kuanzia sasa
watapaswa kuomba kazi na kusailiwa kwa kulingana na sifa zao.
Katika hatua nyingine, Waziri Muhongo amaeanza kutekeleza maagizo ya
kupunguza matumizi ya serikali kwa vitendo ambapo amepiga marufuku watendaji
wake kutumia magari ya anasa, maarufu kama mashangingi na kwamba viongozi wakuu
watatumia magari yasiyozidi CC 3000, ambayo watakopeshwa.
Alisema kwa kufanya hivyo, wizara yake itaokoa kiasa cha sh bilioni 1.4 kila
mwaka, fedha ambazo zitaelekezwa kwenye matumizi mengine ya maendeleo.
Pia alikubaliana na hoja ya msemaji wa kambi ya upinzani, John Mnyika, ya
kuitaka serikali kuweka akiba ya dhahabu, akisema jambo hilo ni la msingi na
kama kuna mchumi atalikataa itabidi wamtilie shaka.
“Kwa mfano, unaweza kuona wenzetu wa mataifa makubwa walivyojizatiti katika
hilo, mathalani Marekani inaongoza kwa kuweka akiba ya tani 8,133.5, ikifuatiwa
na Ujerumani 3,396.3, IMF tani 2,811.1, Italia 2,451.8, Ufaransa 2,435.1, China
1,054 wakati Afrika Kusini inashika nafasi ya 29 ikiwa na tani 125,”
alisema.
Wezi wa umeme waanikwa
Waziri Muhongo pia aliwataja wezi sugu wa umeme ambao wamekuwa wakitumia
nishati hiyo kwa kutumia luku za wizi ambazo hazijasajiliwa na TANESCO ambapo
katika orodha hiyo imo shule maarufu ya kimataifa ya St. Mary’s inayomilikiwa na
mmoja wa wabunge wa Viti Maalumu, Mchungaji Gertrude Rwakatare.
Alisema kuwa shule hiyo imetumia umeme wa sh milioni 10.5 huku wezi wengine
wa Dar es Salaam wakitajwa kuwa ni Access Benki ya Tabata sh milioni 13.8, Shree
Shalim sh milioni 8.1 na Hoteli ya Akubu Paradise mali ya Philip Ngunda iliyoko
eneo la Kariakoo.
No comments:
Post a Comment