KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Saturday, 28 July 2012

Wapinzani waanika uozo wa Tanesco  
Kizitto Noya na Boniface Meena, Dodoma
KAMBI ya Upinzani Bungeni imeanika kile ilichokiita uozo ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), huku wakiitaka Serikali ielekeze kufanyika kwa uchunguzi wa kijinai dhidi ya tuhuma zinazomkabili Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, William Mhando.

Katika maoni yake kuhusu hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini, bungeni jana, kambi hiyo ilisema Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), aamuru uchunguzi wa kijinai dhidi ya Mhando kuhusu tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika katika hotuba yake, pia alipendekeza kuundwa kwa kamati maalumu ya Bunge kwa ajili ya kuchunguza masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na tuhuma za ufisadi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta. Mnyika alilieleza Bunge kuwa uchunguzi huo pia uhusishe Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi wa kiuchunguzi (forensic audit) kwa malipo yaliyofanywa kwa Kampuni za Mafuta za Puma Energy, Oryx na Camel Oil ili kubaini iwapo kuna vigogo zaidi wa Serikali walioshiriki katika malipo tata.

“Izingatiwe kwamba masharti ya Ibara ya 27 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inamtaka kila mtu.. kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi pamoja na kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu,” alinukuu.

Uozo Tanesco
Kambi hiyo imetaka Mhando achunguzwe kijinai kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi. Alisema katika mchakato wa kununua mafuta ya kuzalisha umeme wa dharura, licha ya ukweli kwamba mafuta ya BP yanauzwa kwa bei ndogo ikilinganishwa na Kampuni ya Oryx, Mhando alisaini mkataba wa kununua mafuta kutoka Oryx kwa bei ya Sh1,501,707.60 kwa tani.

“Aidha, wiki moja kabla ya hapo mkurugenzi huyo alikwishasaini mkataba mwingine na Kampuni ya Camel Oil kwa bei ya Dola za Marekani 905.24 au Sh1,444,488.80 kwa tani... Mikataba yote miwili ilikuwa na gharama kubwa zaidi kuliko gharama za BP. Hata hivyo, mkataba wa BP ulikatishwa na Tanesco ikaanza kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kwa Kampuni za Oryx na Camel Oil.

” Mnyika aliendelea: “Cha ajabu zaidi ni kwamba licha ya mikataba ya Kampuni za Oryx na Camel Oil kuonyesha bei ya Sh1,501.70 na Sh1,466.49 kwa lita, Tanesco ilinunua mafuta hayo kwa Sh1,850. Kwa ulinganisho, mafuta yaliyouzwa na BP kwa mkataba na Rita yaliigharimu Serikali Sh13,140,000,000 kwa bei ya Sh1,460 kwa lita.

“Hii ndiyo kusema kwamba kama Tanesco ingeendeleza mkataba na BP badala ya kuuvunja, gharama ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL ingekuwa Sh23,520,600,000 na hivyo Tanesco ingeliokolea taifa Sh6,282,900,000 kwa mwezi,” alisema. Alisema kutokana na ushahidi huo, wanaomtetea Mhando baada ya kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi, hawawezi kueleweka na jamii ya Watanzania wazalendo na wapinga ufisadi.

Mhando na kashfa nyingine
Katika hatua nyingine, Mnyika alisema Mhando ni Mkurugenzi na mwanahisa wa kampuni binafsi inayoitwa Santa Clara Supplies Co. Ltd ya Dar es Salaam. Alisema wakurugenzi wengine ni mkewe, Eva Martin William ambaye ni mkurugenzi mtendaji na watoto wao.

“Kwa mujibu wa taarifa ambazo kambi ya upinzani inazo, Desemba 20, 2011 Santa Clara Supplies iliingia mkataba na Tanesco na kukubaliwa kuwa mgavi wa vifaa vya ofisini vya shirika hilo la umma kwa gharama ya Sh884,550,000,” alisema na kuendelea:

“Mkataba huo ulisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji Mhando kwa niaba ya Tanesco na mkewe Eva Martin William kwa niaba ya Santa Clara Supplies. Aidha, barua ya Tanesco iliyoitaarifu Santa Clara Supplies kwamba imepatiwa zabuni hiyo, iliyoandikwa na tarehe 24 Novemba, 2011 ilisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco ambaye ni Mhando.”

Mnyika alieleza kuwa kitendo cha Mhando kuingia mkataba na kampuni yake akiwa mkurugenzi wa Tanesco, ni kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inayozuia viongozi kufanya uamuzi unaoingilia masilahi yao. Hata hivyo, Mnyika alionya kuwa hatua ya kumwajibisha Mhando isitumiwe kama kafara ya kuficha uzembe na udhaifu wa Serikali.

Alisema taarifa za utendaji wa Tanesco kuhusu mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta uliokuwa ukifanyika zilikuwa zikiwasilishwa kwenye vikao vya Wizara ya Nishati na Madini na hata vikao vya Baraza la Mawaziri.

Wabunge wang’aka
Wakichangia hotuba hiyo, wabunge walimpongeza Profesa Muhongo kwa kufanya kazi nzuri wengine wakisema baadhi yao wanafanya biashara na Tanesco.
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alisema kuna wabunge wamekuwa wakihongwa ili watetee ufisadi unaofanywa katika shirika hilo.

“Inawezekana Maswi (Eliakim, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini), ulikuwa academician (mwanataaluma), huwajui wanasiasa ila utatuzoea. Tunajua ulifuatwa na wabunge ili uwape hongo wapo humo tunawajua,” alisema na kuendelea:

Utawezaje kuisifu Tanesco wakati kwa muda mfupi wa kina Muhongo na Maswi tumegundua kwamba wanakusanya bilioni 80, mishahara bilioni 11 na wana bilioni 50 kila mwezi?”.
Alisema ni muhimu Sheria ya Uhujumu Uchumi ikarekebishwa ili mafisadi, wakiwamo wabunge washtakiwe kwa uhaini.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Diana Chilolo alisema kitendo alichokifanya Maswi ni kizuri kwa kuokoa fedha kiasi cha Sh3 bilioni ambazo zilikuwa zikipotea kutokana na ununuzi wa mafuta ya bei ghali kwa ajili ya mitambo ya IPTL.

Alisema Serikali ilikuwa ikitumia kiasi cha Sh18 bilioni kununulia mafuta hayo, lakini ikatumia Sh15 bilioni hivyo kuokoa kiasi cha Sh3 bilioni ambazo zinaweza kusaidia maeneo mengine ya nchi.
“Huyu mtendaji amefanya kazi nzuri kwa kuwa alilolifanya ni jambo la kizalendo, hivyo ni lazima tuwaangalie hawa watendaji wetu ambao wanafanya kazi nzuri,” alisema Chilolo.

Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka alisema Profesa Muhongo ana kazi kubwa ya kukabiliana na changamoto za sekta ya nishati na madini na kumtaka ajipange vizuri.

Alitaka wote watakaobainika kuhusika na ufisadi Tanesco wachukuliwe hatua inavyopaswa... “Hata wale walionunua mafuta kinyume cha sheria nao wachunguzwe ili waweze kushughulikiwa. Hivyo namwomba Waziri Mkuu na hata Rais, atusaidie katika hili.”

Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango alisema kitendo alichokifanya Maswi ni cha kizalendo na kwamba anahitaji kupongezwa na hata kitendo cha kuwachukulia hatua watendaji wake ni cha kizalendo kwa kuwa anaisaidia nchi.

“Maamuzi(uamuzi) aliyoyafanya waziri na katibu yake ni ya kizalendo hivyo tunahitaji kuwapongeza kama kambi ya upinzani ilivyofanya kwa kuchukua maoni ya kikao chetu cha chama na kuyaweka kwao,” alisema Kilango.

No comments:

Post a Comment