Lissu, Wenje waibana serikali migogoro ya ardhi
Maoni
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema kitendo cha serikali kujigeuza kuwadi, wakala na dalali wa wawekezaji kwa kutumia nguvu kuwanyang’anya wananchi ardhi na rasilimali zake na kuwauzia watu hao, kinajenga mazingira hatari ya umwagaji damu katika siku za usoni nchini.
Wakati Lissu akitoa onyo hilo kali, Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje, ameibana serikali bungeni akiitaka ieleze hatua itakazowachukulia maofisa wake waliotoa vibali vya ujenzi wa nyumba zilizobomolewa jijini Dar es Salaam Jumanne wiki hii.
Walisema hayo kwa nyakati tofauti jana wakati wakichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, iliyowasilishwa na Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Anna Tibaijuka, bungeni, juzi.
Lissu alisema kesi zinazoongoza kwa wingi katika mfumo wa mahakama zote nchini, ni zile zinazohusu migogoro ya ardhi na kwamba kuna kesi zisizopungua 6,000 katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi zinazohusu migogoro ya ardhi.
Hata hivyo, alisema ipo migogoro mingine ya ardhi ambayo haipelekwi mahakamani kwa sababu mahakama sasa imekuwa mithili ya gulio la kununulia haki.
Alisema hali hiyo imewafanya wananchi kupoteza imani na mfumo wa mahakama wa kutatua migogoro ya ardhi na hivyo, kulazimika kujichukulia sheria mikononi.
Lissu alisema migogoro, ambayo imekuwa ikisababisha mapinduzi na vita vya kutafuta ukombozi katika baadhi ya nchi barani Afrika, ukiangalia chini yake, mingi ni ile inayohusu ardhi.
“Kwa kufanya hivyo, tunaundiwa vita kwa sababu wananchi wamechoka,” alisema Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzania Bungeni.
Kauli ya Lissu ya “ukuwadi” ilimfanya Mbunge wa Mpendae (CCM), Salim Hassan Turky, kusimama na kuomba Mwongozo wa Spika akieleza kuwa neno hilo halistahili kutumika bungeni, kwani hututumika katika mazingira mabaya ya kumtafutia mwanaume mwanamke.
Akitoa Mwongozo wa Spika, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema licha ya yeye kutofahamu vyema mtaalamu wa lugha ya Kiswahili kama ilivyo kwa Mbunge wa Uzini (CCM), Muhammed Seif Khatib na Mbunge wa Bukombe (Chadema), Profesa Kulikoyela Kahigi, alisema udalali ni kazi rasmi inayotambulika na ni ya halali, lakini “ukuwadi” si rasmi, ingawa wapo.
Wakati Lissu akisema hayo, Wenje alihoji ilikokuwa serikali wakati wamiliki wa nyumba zilizobomolewa jijini Dar es Salaam Jumanne wiki hii wakijenga nyumba hizo.
Nyumba hizo zilibomolewa katika operesheni iliyoendeshwa na Wizara ya Maliasiali na Utalii, Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa madai ya kujengwa kwenye viwanja zaidi 100 vilivyopo ndani ya hifadhi ya misitu ya mikoko kwenye fukwe za bahari na mito, kinyume cha sheria.
“Hawa waliotoa vibali mnawachukulia hatua gani? Mnabomoa maghorofa yao mnapiga makofi. Mnasubiri jengo linajengwa halafu mnabomoa? Mnaendeshaje nchi kwa kuvizianaviziana, kulipizana kisasi?” alihoji Wenje.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment