Dk Limbu:Maji yanatishia ubunge wake |
MBUNGE wa Magu (CCM), Dk Festus Limbu, amesema endapo maji hayatafika katika jimbo lake hadi mwaka 2015 basi hataweza kutetea kiti chake cha ubunge katika uchaguzi huo.Alisema wapigakura wake wamemwambia kuwa iwapo hawatapata maji hadi kufikia kipindi hicho, basi hawatampigia kura. “Nimeambiwa hivyo na wananchi wangu, wasipopata maji hawanipi kura na mimi sipo tayari kupoteza ubunge wangu kabisa. Kwa kweli kwa bajeti hii ilivyo, sioni dalili ya kupata maji mwaka 2015.” alisema Limbu. Alisema tatizo la maji katika jimbo lake ni kubwa na kwamba uhaba huo umesababisha baadhi ya wananchi kuliwa na mamba wakienda kutafuta maji katika mito.“Wanafunzi hawasomi, wanawake hawalali kwa sababu ya maji, imekuwa ni maji tu hakuna shughuli nyingine.” alisema. Mbunge huyo alisema kuwa sheria ya kuufanya Msitu wa Sakaya kuwa Hifadhi ya Taifa umesababisha mto uliotegemewa na wananchi wa jimbo lake kufungwa na wao kupigwa marufuku kuutumia. “Msitu wa Sakaya una vijiji vinane, vyote vinategemea mto huo. Lakini kwa kuwa hifadhi hiyo imeanzishwa kisheria, basi msitu unajaliwa kuliko watu.” alisema Limbu. Aliitaka Serikali kuwaandalia wananchi mazingira rafiki kabla ya kuwachukulia rasilimali zao kwani bila ya kufanya hivyo, wananchi watataabika kwa sababu waliutegemea mto huo.Alisema kuwa ni vyema ikiwa Serikali itawaruhusu wanakijiji wanaoishi kando kando ya Hifadhi ya Sakaya kutumia mto huo kwa ajili ya maji na mifugo. Aliongeza kwa kuitaka Serikali iandae fedha kwa ajili ya kujenga malambo na visima vya maji ya kutumia kabla ya kuwanyima fursa ya kutuma rasilimali iliyopo katika himaya yao |
No comments:
Post a Comment