KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Sunday, 22 July 2012


RIPOTI MAALUMU: Silaha zabadilishwa kwa gunia la mahindi 
Sunday, 22 July 2012 00:12

Na Mwandishi Wetu
WAKATI vitendo vya uhalifu vikizidi kuongezeka sehemu mbalimbali nchini, sasa silaha kutoka nchi jirani zinadaiwa kuingia kwa wingi na kuuzwa mitaani na baadhi yake kubadilishwa na mahindi, Mwananchi Jumapili limegundua.

Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa, kutokana na kushamiri kwa biashara hiyo ya silaha nchini, bunduki moja aina ya Short Machine Gun (SMG) sasa inauzwa kati ya Sh300,000 hadi Sh500,000, huku bunduki aina ya AK 47 ikiuzwa kwa Sh700,000 hadi Sh1 milioni.
Wakati vijiji kadhaa mkoani Tabora vilipokumbwa na uhaba wa chakula, bunduki aina ya SMG  katika Kijiji cha Usinge wilayani Urambo  zilibadilishwa kwa gunia moja la mahindi, huku AK 47 ilibadilishwa kwa magunia mawili ya mahindi.
 Gazeti hili huko nyuma liliwahi kuripoti kuuzwa kwa bastola holela mitaani katika miji mikubwa ikiwamo Arusha, Mwanza, Moshi ambapo silaha hiyo ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh800,000 hadi shilingi milioni moja.
Uchunguzi wa muda mrefu uliofanywa na Mwananchi Jumapili katika mikoa mbalimbali iliyopo mipakani umebaini kuwa, mtandao huo wa uingizaji silaha ni mkubwa na unawashirikisha matajiri na baadhi ya askari polisi wasiokuwa waaminifu.

Silaha hizo huingizwa nchini kupitia mkoani Kigoma, mpakani mwa  Rwanda, Kenya, na Burundi kwa kutumia njia mbalimbali ikiwamo, magari, pikipiki na boti kupitia Ziwa Victoria pamoja na  baiskeli ambapo bunduki hizo hufungwa kama mzigo ya kawaida.

Chanzo kimoja cha uhakika kililiambia Mwananchi Jumapili kuwa eneo la Usinge ndiyo kituo kikuu cha kupokelea silaha kutoka Burundi na Rwanda ambazo husambazwa mikoa mbalimbali nchini.

Mawakala

Mmoja wa watu ambao wamewahi kufanya biashara alisema kuwa mawakala wa silaha hizo wapo katika mikoa ya Kigoma na Tabora na kwamba ni wafanyabiashara, huku baadhi wakidaiwa kuwa watu wenye asili ya kabila la Kitutsi.

Lakini kwa Usinge alimtaja mfanyabiashara mmoja ambaye pia hukopesha fedha kwa riba (jina tunalo) ambaye inadaiwa kuwa biashara hiyo haramu anayoifanya inajulikana na mamlaka mbalimbali za juu serikalini.
Habari hizo zilieleza kuwa mfanyabiashara huyo amekuwa akinunua SMG kati ya Sh300,000 hadi Sh500,000, na kwamba huzisafirisha kwa kutumia mtandao wake hadi mikoa ya Kanda ya Ziwa na huziuza kati ya Sh800,000 hadi Sh1,000,000.
Mbali na kutumia silaha hizo kwa ujambazi pia huzitumia kufanya uwindaji wa tembo  kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
Habari hizo zinaeleza kuwa baada ya kuyapata meno hayo ya tembo  na kukatwa vipande, husafirisha  kwa kusaidiwa na maofisa wa maliasili na askari polisi wasiokuwa waaminifu.
Askari hao inadaiwa wanatumiwa na wafanyabiashara wakubwa kuuza meno ambapo huwalinda watu hao wanapokuwa wanasafirisha  nyara hizo huku wakiwa wamevalia sare zao za kazi.
Zinafafanua kwamba wanaposafirisha bidhaa hizo, huyaweka meno katika magunia ya mkaa kutokea Wilaya za Serengeti, Bunda, Bariadi, Maswa hadi Mwanza ambapo mtandao wa watumishi wa umma wasiokuwa waaminifu huipokea mizigo hiyo na kuisafirisha kwenda kwa mawakala wa biashara hiyo.
Kwa mujibu wa vyanzo huru vya habari, silaha hizo hupokewa Mwanza ambapo huuzwa kwa wingi wilayani Serengeti kwa ajili ya kufanyia uhalifu na uwindaji wa wanyama pori.
“Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (Tanapa) kwa kutumia wapelelezi wao wamejitahidi kutoa taarifa Polisi lakini wanaokamatwa baada ya muda huachiwa…,  Polisi ni chanzo kikubwa hapa,” zilieleza habari hizo.
Silaha kutokea Somalia
Inadaiwa kuwa silaha hizo zinazotokea Somalia, huingizwa nchini kwa njia ya panya kupitia Kenya kwa kutumia punda ambao huwa wanakokota mikokoteni iliyopakiwa magunia ya mahindi au karanga ambayo ndani yake huwa na silaha hizo.

Tanapa wasaka mtandao
Tangu kuuawa kwa Tembo ‘George’ maarufu kama tembo wa JK, Tanapa inadaiwa kutumia gharama kubwa kuusaka mtandao huo bila mafanikio.

Mmoja wa maofisa wa shirika hilo kwa sababu za kiusalama jina limehifadhiwa aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa anajua taarifa zote za upatikanaji wa silaha wanazozikamata.
“Kuna mambo ambayo yanatusumbua sana maana wenzetu (polisi) wanatangaza kuwa wamekamata silaha, lakini baadaye waliokamatwa huachiwa baada ya kutoa fedha,” alisema  ofisa huyo na kuongeza:
“Kama rushwa itaendelea hali ya usalama kwa mikoa ya Kanda ya Wiwa itakuwa mbaya maana silaha ni nyingi na zilizokamatwa ni kidogo kuliko zilizopo.”
Ofisa huyo alikwenda mbali zaidi kwa kufafanua kwamba baadhi ya watuhumiwa wanaouza na kusafirisha silaha hizo wana uhusiano na baadhi ya maofisa wa polisi ambao huvujisha siri kila inapofanyika operesheni ya kuwakamata watu hao.
“Matatizo yote yanachangiwana maofisa wa polisi ambao hawana mpango wa kumaliza tatizo hili hatari,  nchi itageuka dampo la silaha za kivita, vyombo vya usalama vinatakiwa kuwachunguza maofisa wanaotuhumiwa, tena wachunguzwe mpaka mali zao kwani baadhi yao  wanadaiwa kujengewa nyumba,” kilibainisha chanzo hicho.
 Kamanda Simon Sirro

Kamanda wa operesheni Tanzania, Saimoni Siro aliyeendesha msako wa watuhumiwa wa ujambazi waliohusika na mauaji ya mtalii na Meneja Msaidizi wa Kambi ya Ikoma Bush na kupora vitu mbalimbali  alikiri hivi karibuni kuwa, uingizaji wa silaha za kivita unazidi kushika kasi.

"Uhalifu wa kutumia silaha unazidi kushika kasi, wengine wanahusika na ujangili katika hifadhi na wengine kwenye matukio kama haya ya uhalifu lakini tunakabiliana nao kuhakikisha wahusika wanakamatwa, nashukuru hata wazee wamekerwa na hali hii na wanatoa ushirikiano mzuri maana nimeitwa hadi kikao cha wazee wakanieleza nao mikakati yao," alisema.
RPC Mara
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Robert Boaz na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa huo, Emmanuel Lukula kwa nyakati tofauti waliliambia Mwananchi Jumapili juu ya ongezeko la silaha za kivita mkoani humo na kueleza kuwa hali hiyo inatishia usalama wa raia na mali zao, ikiwemo uwindaji haramu.

Kamanda Boaz alisema kwa kipindi cha Januari 2011 hadi Mei 2012,  bunduki  25 zimekamatwa na nyingine kusalimishwa kwa hiari ambapo kati ya hizo SMG ni 19 na Riffle 8.
Risasi zilizokamatwa ni 686 za SMG na 630 za Riffle na short gun zikiwa 56.
“Ni kweli silaha za kivita zinaingizwa nchini kutoka nchi jirani na  idadi hiyo ni kubwa na bado zipo nyingine  hazijakamatwa ila bado tunaendelea na uchunguzi kwa kuwa inaonyesha zinaingizwa kwa ajili ya kufanya uhalifu,” alisema Kamanda Boaz.

Aliongeza, “Lakini wapo wanaonunua na kudai kwamba wanazitumia  kwa ajili ya kulinda mifugo yao, lakini silaha za kivita  hairuhusiwi kumilikiwa na mtu,” alisema.Alipoulizwa kama askari nao wanahusika katika vitendo hivyo Boaz alisema,  “Ndiyo nasikia kutoka kwako, ila sina uhakika.”

Akizungumzia matukio yaliyotokea Mei mwaka huu alisema zilikamatwa bunduki nne aina ya SMG pamoja na risasi 436 ambazo ziliingizwa na watu kutoka Urambo na Kigoma na kwamba, mbili kati za  silaha hizo zilikuwa zimeishaingia wilayani Serengeti kwa mkazi mmoja wa Kijiji cha Bisarara ambaye awali alitoa risasi 228 na baada ya kubanwa akatoa nyingine.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa amenunua SMG mbili na baada ya kukamatwa alitaja mtandao wake ambao mmoja wa wenzake alikamatwa mjini Magumu na mwingine Bunda.

RPC Kagera
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Salewi alikiri kuingizwa kwa silaha hizo nchini  kutoka nchi za Uganda na Rwanda na kufafanua kwamba, huingizwa kupitia njia za panya na kwamba ni vigumu kuwadhibiti watu hao.
“Ni kweli silaha zinaingizwa kwa njia ya mabasi na  boti. Eneo la mpaka wa nchi ni kubwa hivyo kuwakamata ni kazi ila juhudi zinafanyika” alisema.

Alisema silaha hizo zinatumika katika uhalifu na kuongeza, “Kwa kushirikiana na wananchi  tumekamata SMG  na AK 47 pamoja na watu wanaopeleka silaha hizo mikoa mbalimbali, wananchi wasikubali kukaa kimya wakati wakiwafahamu watu hawa.”  

RPC Shinyanga
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,  Athumani Diwani aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa silaha hizo zinatoka nchi za Rwanda na Burundi na kwamba wanaoziingiza wanapitia mkoani Kigoma.

“Tuna changamoto kubwa kwa kuwa kasi hiyo hasa kwa mwaka jana ilikuwa kubwa, wanaingia na silaha za kivita,” alisema Diwani.
Alisema kuwa taarifa za polisi kuhusika katika matukio hayo wamezipata na wanazifanyia kazi.

RPC Kigoma
Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma Kamishna Msaidizi, Frasser Kashai aliliambia gazeti hili kwamba sababu kubwa ya kushamiri kwa vitendo vya uingizaji silaha inatokana na udhibiti mdogo katika maeneo ya mipaka ya nchi na kwamba jambo hilo linavisumbua vyombo vya ulinzi na usalama.

 “Burundi licha ya kuwa ni nchi ndogo, wameathiriwa na migogoro, jambo linalowafanya waingie nchini kutafuta hifadhi, lakini wanaingia na silaha na kufanya uhalifu huku wakisaidiwa kuhifadhiwa na wananchi,” alisema Kashai.

Alisema kuwa bunduki aina ya SMG na AK 47 ndizo zinazotumika katika uhalifu na uwindaji wa wanyama.

”Wanakuja na nia mbalimbali lakini wakiona hali siyo nzuri wanaingia katika hifadhi. Hivi sasa tunashirikiana na Tanapa kufanya msako. Tunawaomba wananchi washirikiane na Jeshi la Polisi ili kukomesha vitendo hivi,” alisema Kashai.

RPC Tabora 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora (ACP) Anthony Rutha alisema watu hao wanaingiza bunduki kwa kuzipitisha porini na kwamba huingizwa na wakimbizi ambao hurudi nchini kwa maelezo ya kuja kusalimia ndugu na jamaa.

“Kambi ya Ulyanhulu inatusumbua sana kwa kuwa pale zinaingizwa silaha kali kama SMG na AK 47 na kituo chao kikubwa ni Urambo, Sikonge na hasa Usinge ambako kunatisha zaidi kutokana na kuzungukwa na mapori,” alisema.

Hata hivyo alisema kwa sasa Usinge kumetulia baada ya kituo cha polisi kufunguliwa mapema mwaka huu.

“Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Mwanza, Mara,Tabora, Shinyanga, Kigoma na Kagera ziliomba kibali  ofisi ya Waziri Mkuu ili tufanye operesheni za pamoja lakini hatujawahi kujibiwa, bila kufanya hivyo hali itakuwa mbaya.” alisema Rutha.

Rutha alisema mpaka sasa amepata taarifa kuwa baadhi ya askari wilayani Kibondo  wanahusika katika matukio hayo na kwamba jambo hilo linachunguzwa.

RPC Mwanza
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow alisema kuwa silaha hizo zinaingizwa kutoka nchi jirani za Rwanda na Burundi.

 “Kwa jinsi mazingira yalivyo watu hawa wanaingia nchini kwa kutumia njia za majini, barabara pamoja na njia zisizo halali jambo linalofanya vikosi vya ulinzi kushindwa kuwadhibiti watu hawa,” alisema.
 via http://www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment