Nishati na Madini yawagawa wabunge |
Monday, 23 July 2012 20:59 |
KATIBU MKUU AZILIPUA KAMPUNI ZA MAFUTA, ASEMA HAKUNA MGAWO WA UMEME
Mwandishi Wetu
WAKATI baadhi ya wabunge wakitaka kuwachukulia hatua Waziri wa Nishati na Madini, Pofesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakimu Maswi kwa madai ya kuiuka sheria ya Ununuzi wa Umma, mtendaji mkuu huyo wa wizara ametupa kombora la ufisadi dhidi ya baadhi ya kampuni za mafuta nchini.Wanaowatuhumu akina Muhongo na Maswi wanadai kuwa, walikiuka sheria ya ununuzi wa umma kwa kuipa zabuni Kampuni ya Puma Energy ya kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL na kuziweka kando kampuni zilizokuwa zimechaguliwa kupitia mchakato halali wa zabuni ya Tanesco.
Suala hilo linahusishwa na kusimamishwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando kwamba alichukuliwa hatua baada ya kukataa kutii maelekezo ya Wizara.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa kumekuwa na mgawanyiko miongoni mwa wabunge, ambao unaanzia kwenye Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo hadi sasa hawajaafiki uamuzi wa kuwachukulia hatua viongozi hao.
“Ni kama tumeshindwa kuelewana huko kwenye Kamati, lakini wabunge ndio tumekuwa tukilalamikia ufisadi Tanesco, sasa tunawashangaa wenzetu ambao wameanza kuiandama tena Serikali kwa kuchukua hatua,” alisema mmoja wa wabunge wa CCM.
Mjumbe mwingine ambaye pia ni Mbunge wa CCM alisema kuwa, Muhongo na Maswi walikiuka sheria.
“Tutakuwa tunakosea, tukiruhusu hawa watu wavunje sheria na halafu eti tuwaachie,” alsema mbunge huyo.
Nje ya Kamati hiyo, wabunge bila kujali itikadi zao nao wamegawanyika huku wengine wakitaka viongozi hao wachukuliwe hatua kuhusiana na suala hilo na wengine walisema: “Hakuna kosa walilofanya, waachwe waendelee na kazi.”
Chanzo cha mgawanyiko huo ni sababu zilizotolewa na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini kwamba waliwapa Tanesco fedha za kununua mafuta mazito ili kuiepusha nchi na mgawo wa umeme, lakini wakaelekeza mafuta hayo yanunuliwe Kampuni ya Purma ambako bei ya lita moja ni Sh1,460.
Kwa kufanya hivyo uongozi wa Wizara unadaiwa kuokoa kiasi cha Sh3 bilioni ambazo zingetumika kama mafuta yangenunuliwa katika kampuni zilizokuwa zimeshinda zabuni kupitia mchakato wa Tanesco.
Ndani ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, baadhi ya wajumbe walinukuliwa wakisema kuwa hata kama Muhongo na Maswi walikuwa na nia njema ya kuokoa fedha za umma, lakini waondolee kwa kukiuka sheria.
Hata hivyo, hatua hiyo inapingwa na baadhi ya wajumbe wanaosema uamuzi waliofanya (Muhongo na Maswi) unapaswa kupongezwa, kwani ni mwanzo wa kumaliza ufisadi ulioota mizizi ndani ya Tanesco na Wizarani kwa ujumla.
Maswi afunguka
Maswi katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, aliwatupia kombora baadhi ya wamiliki wa kampuni za mafuta akisema zimekuwa zikifanya vitendo vya ufisadi na kutaka Watanzania wazalendo kuunga mkono juhudi za wizara yake za kupambana na hali hiyo.
Maswi alifafanua kwamba, baadhi ya kampuni (majina tunayo) zimekuwa zikinunua mafuta kwa bei rahisi kutoka Puma Energy na kisha kuiuzia IPTL kwa bei ya juu na kupata mabilioni ya shilingi.
Mtendaji mkuu huyo wa wizara alisema haiwezekani kwa akili ya kawaida Serikali iache kusimamia fedha za umma kwa kuhakikisha mafuta yananunuliwa kwa bei nafuu moja kwa moja toka Puma Energy badala ya kununua kwa mtu wa kati ambaye anaongeza bei ya mafuta hayo.
Akitoa mfano wa ufisadi unaofanywa na baadhi ya kampuni, Maswi alisema kuwa, Januari mwaka huu kampuni moja kati ya zilizopata zabuni ya kupeleka mafuta Tanesco, (jina tunalo) ilinunua mafuta kutoka kwa Puma Energy kwa bei ya Sh 1,068 kwa lita moja ya ujazo, kisha ikaenda kuuzia IPTL kwa Sh1,860.
“Kwa hiyo, haya mambo Watanzania wanapaswa kuyafahamu. Na ninyi waandishi msaidie kuandika mambo yenye maslahi kwa taifa. Mimi nitasimamia maslahi ya taifa, hatuwezi kuacha kununua mafuta kwa bei rahisi halafu tununue kwa bei ya juu. Shilingi moja tu kwa mfano, katika maisha ya Mtanzania ni kubwa. Si mnaona mkipandishiwa bei ya dizeli na petroli mnavyolalamika!” alisema.
Akizungumzia tuhuma za kukiuka sheria kwa kuipa zabuni PUMA Energy, Maswi alisema mchakato wote ulifanyika na kukamilika kabla hajateuliwa kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
“Ikumbukwe kuwa niliteuliwa kuja Wizara ya Nishati na Madini, tarehe 22 Julai, 2011 siku ya Ijumaa na nilianza kazi kama Kaimu Katibu Mkuu Julai 25, 2011 siku ya Jumatatu. Kabla ya kuanza kazi niliwaeleza wenzangu utendaji wangu na ninavyopenda twende kwa kufuata utaratibu,” alifafanua Maswi.
Alifafanua kwamba mwishoni mwa mwaka 2010/11 kulikuwa na mgawo mkubwa umeme nchini, na Serikali kulazimika kuingilia kati kuhakikisha mgawo huo unaondolewa na kuitaka IPTL kuwasha mitambo yake katika kiwango cha megawati 100.
“Aliyefanya hivyo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco na siyo Wizara. Ikumbukwe pia kipindi hicho IPTL ilikuwa inasimamiwa na Wakala wa Vizazi na Vifo (Rita) kwa kuwa kulikuwa na amri ya kufilisi (under liquidation process).” alisema Maswi
Aliongeza kwamba, Tanesco ilifanya hivyo kwa barua Kumb. Na. SMSC/MSC/IPTL ya Juni 10, 2011 ambapo kampuni hiyo ilitakiwa kuanza kufua umeme hadi Desemba 2011 na kuondoa mgawo wa umeme.
“Aidha, Tanesco walipeleka barua RITA wakitaka mafuta ya kuendesha mitambo yapatikane. Ieleweke kuwa ili kuendesha IPTL kwa siku moja tunahitaji MT500,” alifahamisha Maswi.
Mgawo wa umeme
Kuhusu mgawo wa umeme, Maswi alisema kumekuwa na upotoshaji wa makusudi kuhusu suala hilo.
Alifafanua kwamba, kwa jinsi Serikali na Tanesco walivyojipanga kuanzia sasa hadi Desemba, hakutakuwa na mgawo wowote wa umeme.
Maswi alisema uwezo wa juu wa ufuaji wa umeme (installed capacity) kwa sasa ni Megawati 1,375.74, ingawa, wastani wa uwezo halisi (available capacity) ni Megawati 873.
“Kwa upande mwingine, wastani wa mahitaji ya umeme kwa sasa ni kati ya Megawati 650 hadi 720,” alifafanua Maswi.
Alisema kutokana na hali halisi Serikali na Tanesco wamejipanga kuhakikisha hakuna mgawo wa umeme kuanzia sasa hadi Desemba.
Akitoa mchanganuo wa uzalishaji umeme, Maswi alisema nguvu za maji itazalisha megawati 120 hadi 151 (wastani wa megawati 132).
Mitambo ya gesi asili, itakuwa ikizalisha wastani wa Mewagawati 348 na mitambo ya mafuta itazalisha megawati 240.
|
No comments:
Post a Comment