17/07/2012
Hotuba kali ya Tundu Lissu ya kukosoa uteuzi wa majaji dhaifu uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete, imeelezwa kwamba ina baraka zote za baadhi ya viongozi waandamizi wa Mhimili wa Mahakama, gazeti la JAMHURI limeelezwa.
Chanzo cha habari cha kuaminika kimesema hotuba hiyo imepokewa kwa furaha kubwa na viongozi wa mhimili huo, wanaotambua wazi udhaifu wa baadhi ya wateule hao.
Kuna habari za uhakika kwamba Lissu, mmoja wa mawakili machachari nchini, alipata maelezo ya kina na ya uhakika kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Mhimili wa Mahakama nchini, na ndiyo maana akawa na msimamo wa kutetea kile alichokizungumza bungeni.
Duru za uchunguzi zimebaini kuwa kwa nyakati tofauti, Lissu amekuwa akikutana na viongozi hao jijini Dar es Salaam, na kwa karibuni kabisa walikutana Dodoma ikiwa ni siku chache kabla ya Lissu kuwasilisha hotuba hiyo iliyopokewa kwa nderemo na wakosoaji wa uteuzi wa majaji.
Imeelezwa kwamba Lissu alionekana kuwa ndiye pekee anayeweza kuwasilisha ujumbe huo mahsusi kwa jamii na kwa Rais Kikwete, kupitia njia ya hotuba yake bungeni.
“Viongozi (majaji) waliona hakuna mbunge wa CCM anayeweza kuthubutu kulisema hilo. Mtu pekee aliyeonekana kufaa kuifanya kazi hiyo ni Lissu na Kambi nzima ya Upinzani kutokana na ukweli kwamba wapinzani huwa hawabanwi na 'nidhamu ya woga' bungeni,” kimesema chanzo chetu.
Katika hatua nyingine, imebainika kuwa hotuba hiyo haikuvuja hata kwa wabunge wengine wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Lissu alifanya hivyo ili kuondoa uwezekano wa kupunguzwa kwa makali ya hotuba hiyo kama ilivyomtokea mwaka jana.
Wakati fulani Spika alipendekeza hotuba za wasemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wawe wanawasilisha hotuba zao kwa Spika kabla ya kusomwa bungeni ili kuondoa “maneno makali”. Hoja hiyo ilipingwa vikali na upande wa upinzani.
via gazeti la JAMHURI
No comments:
Post a Comment