KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Friday, 13 July 2012


 Wakati mchakato wa uchaguzi wa viongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukiendelea katika ngazi za matawi, kata huku wilaya pamoja na mkoa ukitazamiwa kuanzia mwezi ujao, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho kupitia mkoa wa Mbeya, Profesa Mark Mwandosya, ameandika kitabu kueleza uoza wa uchaguzi unavyofanywa ndani ya chama hicho.

Katika kitabu alichokipa jina la Sauti ya Umma ni Sauti ya Demokrasia, Profesa Mwandosya ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais kazi maalum, ameeleza jinsi alivyofanywa fitna, hujuma na kila aina ya mizengwe wakati wa mchakato wa uchaguzi kama huu unaoendelea sasa kwa mwaka 2007 mkoani Mbeya.

Katika kitabu hicho chenye sura 15 ndani ya kurasa 177, Profesa Mwandosya anataja wazi kuwa mamlaka za kiserikali na chama zilihusika moja moja kutoa maelekezo ili asishinde kiti cha NEC kupitia mkoa wa Mbeya na anawataja kwa majina wahusika wakuu, wakiwamo waliokuwa wanauongoza mkoa wa Mbeya, kiserikali na kichama, na walifanya hivyo wakisaidiwa na rasilimali za serikali na chama pia.

Sura ambazo zimo ndani ya kitabu hicho ni Utangulizi ukurasa wa 1-11; Uchaguzi wa Mwakilishi wa Mbeya Katika Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ikianzia ukurasa wa 12-20; Baada ya Chimwaga kuanzia ukurasa wa 21-28;  
Picture

Matumizi ya Chama kwa Sababu Binafsi kuanzia ukurasa wa 28 -39; Makatibu ‘Wapangwa na Kujipanga Tayari kwa Kampeni ikianzia ukursa wa 40-49 na Kifo cha Mzee Andangile Mwakasendo kuanzia ukurasa wa 50 -93.

Nyingine ni Jumuiya za Chama na Uchaguzi wa Mbeya ukurasa wa 94 – 100; Uteuzi wa Wagombea Nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rungwe kuanzia ukurasa wa 101 – 108 na Makundi Ndani ya Chama kuanzia ukurasa wa 109-112.

Pia zipo za Mwenendo wa Uchaguzi wa Wilaya ya Mbeya Mjini ukurasa wa 113-121;  Wiki ya Mwisho Kuelekea Uchaguzi ukurasa wa 122-146;  Siku ya Uchaguzi Tarehe 11 Septemba 2007;

Matukio Baada ya Uchaguzi kuanzia ukurasa wa 156-158; Yaliyosemwa na Vyombo vya Habari ukurasa 159-165 na mwisho ni sura ya Hitimisho kuanzia ukurasa wa 166-177.

Bila kusema moja kwa moja, Profesa Mwandosya ambaye amekuwa mgonjwa kitandani kwa muda mrefu sasa, akitibiwa India na hapa nchini, anazungumzia vurugu za kwenye uchaguzi ndani ya chama na uwezekano wa serikali kushindwa kutimiza majukumu yake sawasawa.

“… chama kikisimamia vilivyo katiba na taratibu zake, wanachama wakiishi katika misingi na wakiongozwa na imani ya chama chao basi hata serikali inayoongozwa na chama hicho huwa imara na makini. Upande wa pili wa sarafu ni kwamba chama kisipoheshimu katiba yake na miongozo yake, basi si rahisi kusimamia vilivyo serikali,” anasema katika kitabu hicho.

Profesa Mwandosya bila kuficha hisia zake katika kitabu hicho, ametangaza wazi kuwa ameamua kukiandika ili kuacha kumbukumbu kwa yeyote ambaye angependa kufuatilia siasa za vyama ajue, anataja mlolongo wa majina ya watendaji wa CCM wakiwamo makatibu wa wilaya, mkoa na uongozi wa mkoa ambao walijipanga kumshughulikia kisiasa hadi akaamua kulalamika kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kutokana na njama dhidi yake.

Anakwenda mbali zaidi na kutaja majina ya waliokuwa watu wake wa karibu sana katika kambi ya kuwania uchaguzi wa urais mwaka 2005 kuwa walimgeuka wakiwamo ambao walikuwa wanamuona kama baba na ambao kwa ujumla familia zao zilikuwa marafiki wakubwa.

Kwa sababu ya kushindwa kuwapata watu hao kwa sasa hatutataja majina yao.

“Katika kipindi chote cha 2006 na miezi saba ya 2007 kulikuwa na juhudi kubwa zilizoelekezwa katika kuharibu au kuchafua jina la Profesa, ambazo zilikuwa na mpangilio fulani (Character assassination), “ anasema katika kitabu hicho.

“Pale ofisini kwa Bwana…, ofisi ya CCM siku zote kulikuwa na msaafu wa Kikristo, Biblia Takatifu. Siku alipomwita … alikitumia vibaya kitabu kitakatifu. Kwani baada ya ‘kumsomea’ maagizo na maelekezo, na kumpa vitisho, alimtaka ashike Biblia Takatifu kama ishara ya kukubaliana na ombi lao. Kwa kifupi alikuwa anamwapisha mwanaCCM kwa kutumia Biblia,” anasema katika kitabu ambacho amenukuu shuhuda za watu mbalimbali aliozungumza nao na kumthibitishia matukio na mipango iliyokuwa imeandaliwa dhidi yake.

Katika kitabu hicho ambacho bado kuzinduliwa rasmi, Profesa Mwandosya pia anazungumzia tukio la kutokea mtafaruku kwenye msiba wa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Rungwe na jinsi magazeti yalivyoandika.

Ndani ya kitabu hicho, Profesa Mwandosya anathibitisha habari nyingi ambazo ziliandikwa kwenye magazeti ikiwa ni pamoja na ile iliyosema kuwa alimwandikia Rais Kikwete waraka maalum akielezea jinsi demokrasia na maadili ya chama yalikuwa yanakiukwa na watendaji wa chama na serikali katika mkoa wake, ameinukuu barua  hiyo yenye mpangilio wa aya kwa namba kuanzia namba moja hadi 12.

Aya ya mwisho ya barua yake inasema: “Niwie radhi kwa haya kwani kama Mwenyekiti una majukumu mengi na mazito. Lakini nimona nikuletee haya, sio kama malalamiko, bali kama taarifa tu ya yale yanayoendelea, na hasa kukiukwa kwa taratibu na maadili ya uongozi ambayo yanaweza kuleta ufa na mfarakano baina ya wanachama.” 

 Katika kitabu hicho Profesa Mwandosya anasema wazi kuwa anajua kuwa atawaudhi baadhi ya watu aliowataja na vitendo vyao vibaya: “Si nia yangu kumfurahisha mtu au chombo chochote. Nikifanya hivyo nitakuwa nimekiuka misingi ya ualimu na ufahamu. Yaliyomo katika kitabu hiki ni matukio yaliyotokea, sio bahati mbaya bali yalipangwa.”

Hata hivyo, anashauri kuwa kuna mafunzo katika yaliyotokea na ameyaainisha kuwa ni umuhimu wa ufafanuzi wa itikadi ya chama; kuboresha mchakato wa uteuzi na kuomba kura katika uchaguzi ndani ya Chama; usimamizi wa zoezi la uchaguzi na wajibu wa watendaji wa chama na serikali, na athari za matumizi makubwa ya fedha bila udhibiti wa kutosha katika uchaguzi wa ndani ya chama.

NIPASHE jana ilimtafuta Profesa Mwandosya kuzngumzia kitabu chake, lakini simu yake ilikuwa haipokelewi na hata ujumbe wa sms nao haukujibiwa.

---
via gazeti la NIPASHE


No comments:

Post a Comment