KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Monday, 9 July 2012

Mali za Taasisi ya Moyo (THI) ya Dkt. Massau zapigwa mnada; Jengo apewa mwekezaji


Picture: Tanzania Heart Institute iliyokuwa ya Dkt. Massau (Taasisi ya Moyo)
picha via Charaz.blogspot.com
Taasisi ya Moyo Tanzanania (THI), imefungwa rasmi na mali zake kupigwa mnada kwa amri ya Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, ili kulipa deni la Shilingi bilioni saba la pango la jengo linalomilikiwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Mnada huo ulifanyika jana katika hospitali hiyo na kusimamiwa na kampuni ya Erick Auction Mart, ambapo vifaa vyote vinavyomilikiwa na taasisi hiyo viliuzwa kwa wananchi ili kufidia deni la NSSF.

NIPASHE lilifika katika taasisi hiyo ambayo awali ilikuwa inatoa huduma ya matibabu ya moyo kwa Watanzania na watu wengine kutoka nje ya nchi, na kukuta msongamano wa watu waliofika kutaka kununua vitu hivyo.

Matangazo yaliyokuwepo kwenye majengo ya taasisi hiyo yalikuwa na taarifa ya kufungwa kwa hospitali hiyo na kueleza kwamba, tayari amepatikana mwekezaji mwingine anayetaka kutumia majengo hayo yaliyo barabara ya Tunisia karibu na viwanja vya Leaders Club wilayani Kinondoni.

Tangazo hilo lilisomeka kuwa: “Hospitali hii imefungwa kwa amri ya Mahakama, hakuna huduma inayotolewa hapa, jengo hili ni la NSSF limeshapata mwekezaji mpya.”

Katika hatua nyingine, walinzi waliokuwapo katika lango kuu la kuingilia katika taasisi hiyo, waliwazuia waandishi wa habari waliofika eneo hilo kupata taarifa za kina juu ya suala hilo.

Tofauti na minada mingine ya hadhara ambayo imekuwa ikiendeshwa na kampuni za minada, wanunuzi katika mnada huo walitakiwa kulipa Sh. 5,000 ili waingie ndani kushiriki mnada.

NIPASHE lilimtafuta Meneja Uhusiano wa NSSF, Eunice Chiume, ambapo alithibitisha kuwepo kwa mnada huo na kwamba wameamua kufanya hivyo ili kutimiza amri ya mahakama ya kupiga mnada vitu vyote ili kufidia deni.

NIPASHE lilimtafuta Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Ferdinand Massau kupata taarifa kamili ya tukio hilo na alisema hiyo ni habari ndefu  na inahitaji muda zaidi wa mazungumzo.

“Leo ni Jumapili, niko sehemu mbaya na siwezi kuizungumzia hali hiyo kwa sasa, ukitaka taarifa kamili nitafute kesho tuzungumze kiundani zaidi,” alisema kwa kifupi Dk. Massau.

---
NIPASHE


Source: http://www.wavuti.com/#ixzz208OcxfGY

No comments:

Post a Comment