Kusini yatumika kujibu propaganda za udini, ukanda Chadema |
Wednesday, 11 July 2012 10:25 |
Geofrey Nyang’oro
HARAKATI za kisiasa za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mikoa ya kusini – Lindi na Mtwara zimeibua mambo mengi, kubwa likiwa ni kujibu hoja za udini, ukanda zinatolewa dhidi yake Ziara hiyo ya mwezi uliopita ilibatizwa majina mengi, wengine waliita ‘Operesheni Sangara’, ‘movement For Change’ (Vuguvugu la mabadiliko) au ‘Oparesheni Okoa mikoa ya Kusini. Pamoja kutumia fursa hiyo kufungua matawi, kusimika viongozi, kuongeza wanachama na kujibu hoja hizo, viongozi wa Chadema, walikuwa na kauli moja, kwamba dhamira yao kuu ni kuondoa CCM madarakani.
Chadema imefanya mikutano katika mikoa hiyo baada ya kupita kipindi cha miaka sita tangu walipofanya ziara katika mikoa hiyo mwaka 2004.
Walikwenda katika mikoa hiyo ambayo kwa kipindi kirefu ilibaki kuwa ngome kuu ya CCM na Chama cha Wananachi (CUF).
Hoja kuu zilizokibeba chama hicho katika mikutano yake ni majibu ya propaganda ya udini, ukabila na ukanda, umasikini na ushirikiano baina ya CCM na CUF.
Hoja ya udini
Katika mikutanio hiyo propaganda za udini, ukabila na ukanda dhidi ya chama hicho zilifafanuliwa huku chama hicho kiliitupia lawama CCM kuwa ndio walioandaa propaganda hiyo kwa lengo la kuwaondoa wananchi kwenye hoja za msingi zinazohusu maisha yao ya kila siku.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa anasema hoja kama hiyo imewahi kutumika kuiangamiza CUF pindi alipokuwa chama cha upinzani chenye nguvu hapa nchini.
“Mwalimu Nyerere alisema, ukiona mtu anazungumzia ubaguzi wa aina yoyote,….udini, ukabila na ukanda kwenye majukwa ya siasa amefilisika kisiasa, leo tumekuja kuwafumbua macho ili nanyi muweze kufanya uamuzi kwa kuchambua na kuelewa vema juu ya hoja hizo,” Dk Slaa alisema mara kwa mara katika mkutano yake.
Dk Slaa anawataka wakazi wa mikoa hiyo kupuuza hoja hizo kwa kuwa zimelenga kuwasahaurisha na matatizo yanayowakabili, likiwamo la mifumo mibovu ya ununuzi wa korosho, kuhamishwa kwa rasilimali inayotoka katika mikoa hiyo ya gesi, na umaskini unaopandikizwa na sera mbovu za CCM.
Katibu Mkuu alisema Chadema siyo chama cha kidini kama ambavyo wao wameelezwa, na kufafanua kuwa chama hicho ni cha siasa, chenye nia njema ya kuwasaidi wananchi kunufaika na rasimali zao.
“Chadema ilifanya uchaguzi mwaka 2009, kabla hata ya propaganda hizo za udini, ukabila na ukanda hazijaanza kutumiwa na CCM, katika uchaguzi ule viongozi sita wa juu, Waislamu ni wanne na Wakristu ni wawili tu, tena madhehebu tofauti, kama ingekuwa na udini chama hicho kingeitwa dini gani?”anahoji Dk Slaa na kuongeza;
“Hii ni propaganda ambayo CCM baada ya kukosa hoja ya kupambana na Chadema, CCM kukosa majibu ya utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi yenye kaulimbiu ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’.
Anasema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa hoja inayotumiwa na chama tawala ya udini na ukabila siyo mpya na ilitumika pia wakati wa ukoloni.
“Mwingereza wakati wa kupigania uhuru alitumia hoja hiyo, na wakati huo aliwarubuni mashekhe wa kiisilamu kuwa Nyerere ametumwa na maaskofu wa Kanisa Katoliki kudai uhuru na kuwataka wasiunge mkono, lakini mashekhe wa wakati huo walichambua na kutupilia mbali propaganda hizo na ndiyo sababu uhuru ulipatikana,” anasema .
Pia anasema propaganda kama hiyo imewahi kutumiwa na CCM dhidi ya CUF wakati ilipokuwa chama cha upinzani chenye nguvu wakidai chama hicho ni chama cha kiisilamu, hali iliyopoteza heshima ya chama mbele ya jamii.
Kuhusu umaskini
Dk Slaa anasema umaskini chanzo chake ni uongozi mbovu wa CCM na kusistiza njia pekee ya kuondokana nao ni kuiondoa madarakani.
Anasema Tanzania imejaliwa kuwa na rasimali nyingi yakiwemo madini, gesi, maeneo ya utalii na bahari lakini imeshindwa kuinuka kutokana CCM kukosa njia mbadala ya kuwasaidia wananchi.
Anasema mikoa ya kusini ina utajiri mkubwa wa gesi, mazao ya korosho, mihogo na bahari ambayo kama Serikali ingetumia kwa manufaa ya wananchi taifa lingeondokana na umasikini.
“Serikali ingekuwa na nia ya kuwaendeleza wananchi wa Mtwara isingeuza kiwanda cha kubangulia korosho na badala yake ingekiendeleza kwa manufaa ya wananchi wake,”anasema Dk Slaa na kuongeza;
“kiwanda kile kilitoa ajira,kiliongeza ubora wa zao la korosha na kuwapatia faida wakulima,”anasema.
Moto wa chama
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe katika mikutano yake kadhaa, wilayani Masasi mkaoni Mtwara alisema moto uliowashwa na chama chake katika Operesheni Sangara utaendelea nchi nzima, na kuapa kama CCM itapona mwaka 2015 atajiuzulu siasa.
Anasema CCM imepoteza mwelekeo uliowekwa na waasisi wake, chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere wa kuzingatia usawa, udugu na kuacha msingi wake wa kutetea wakulima wanyonge na wafanyakazi.
“Wajibu wa Serikali kokote duniani ni moja tu, kuwezesha watu wake kutoka katika hali ngumu za maisha na kuwapeleka kwenye heri, leo CCM wameligawa Taifa katika vipande, wanauza rasilimali za nchi na kuwadidimiza watu wa kipato cha chini, wengi wao wakiwa ni wakulima,” anasema Mbowe na kuongeza; kazi tuliyonayo ni moja – kuunganisha nguvu kuiondoa CCM madarakani.
“Ndugu zangu ngojeni niwaulize swali, wakati wa utawala wa Mwinyi na Mkapa (marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa), ni kipindi gani maisha yalikuwa mazuri?” Wananchi wakajibu ‘kipindi cha Mwinyi’.
“Miaka 10 ya uongozi wa Mkapa na miaka saba ya Kikwete, ni kipindi gani maisha yamekuwa magumu zaidi?" Wakajibu ‘Kikwete’; Je, 2015 wanakuja tena kutuomba kura huyo atakayekuja si ndiyo itakuwa mbaya zaidi,”anasema Mbowe na kuongeza kuwa Chadema haiwezi kukubali, na harakati za kushawishi wananchi kuondoa CCM madakarani zitaendelea hadi mwaka 2015.
“CCM ya Mwalimu Nyerere ilijali wakulima na wafanyakazi wa kipato cha chini, ilijenga mshikamano baina ya Watanzania wote bila kujali ukabila,”anasema Mbowe na kuongeza;
“Tanzania ina makabila zaidi ya 120, lakini tuliishi kama mtu na ndugu yake, leo taifa limegawanyika vipande huku maadili ya uongozi yakiporomoka,” anasema.
Uhusiano wa CCM, CUF
Chadema walitumia uhusiano ulipo kwa sasa baina ya CCM na CUF uliounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kuwa chama hicho cha upinzani kimesaliti upinzani na wananchi wake.
Kauli hiyo ambayo pia ilitumiwa na viongozi wote wa Chadema waliofanya mikutano katika mikoa na wilaya zote za Lindi, pia ilituiliwa na makazo na mwenyekiti wa Mbowe.
Akihutubia mkutano uliofanyika Lindi Mjini katika Uwanja wa Lulu, Kiongozi huyo anasema ushirikiano huo ni wa viongozi wa juu wa CUF, Katibu Mkuu Seif Sharif Hamad na Mwenyekiti wake Profesa Ibrahimu Lipumba.
Mbowe anasema uhusiano huo umedhoofisha nguvu na uwezo wa wabunge wa CUF wa kuwasaidia wananchi.
“Tuligawana maeneo lengo likiwa kuishambulia CCM ili kuitoa madarakani, lakini wenzetu (CUF) wametusaliti wameshikana mikono na kuungana na CCM na sasa wanatushambulia sisi,”anasema Mbowe.
Anasema kwa sasa chama cheke kimeweka mkakati na hakitalala, kitashambulia vyama vyote, CCM, CUF na washirika wake hadi kitapoiondoa CCM madarakani.
|
No comments:
Post a Comment