KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Wednesday, 18 July 2012


Siku Musa alipokataa kuitwa Mwana wa Binti Farao
M. M. Mwanakijiji
Kwa imani, Musa alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. Akachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa kitambo kidogo tu. (Waeb. 11:24,25).
Mojawapo ya masimulizi ya vitabu vya dini za Kikristu na Kiislamu ambayo yanakubaliana sana na kulingana kwa kiasi kikubwa ni lile simulizi la Nabii Musa. Jinsi gani alizaliwa, wapi alizaliwa, kwanini alitelekezwa, na jinsi gani mama yake alipata nafasi ya kumnyonyesha kwa ruhusa na baraka ya nyumba ya Farao (Firauni – nitatumia maneno haya kwa kubadilishana) yote yanalingana sana.
Na pia jinsi ambavyo ilimlazimu Musa kuikimbia nyumba ya Farao na fahari zake zote, utajiri wake na elimu yote ambayo aliipata kule na kwenda kuunganika na Wanawaisraeli waliokuwa Utumwani kule Misri na kwa uamuzi wake huo kujiweka kuwa ni adui wa kudumu wa Farao.
Haya yote yanaonekana katika Agano la Kale la Biblia Takatifu na katika Kurani Tukufu. Hata hivyo, kwa namna ya pekee mwandishi wa kitabu cha Waebrania anatueleza kwa namna ya pekee kabisa ni kwa sababu gani Musa aliiacha nyumba ya Firauni. Mwandishi anasema “Kwa imani, Musa alipokuwa mtu mzima”.
Kwa maneno mengine, imani ya kile ambacho hakukijua kitatokea, imani ya kutegemea kuwa lililo jema liko mbele yake (hata kama dalili hazioneshi hivyo), imani ya kutambua kuwa ni Muumbaji tu ndiye mwenye uamuzi wa mwisho wa kila kitu kulifanya Musa kuchukua kile ambacho naweza kukiita kuwa ni “uamuzi wa mtu mzima”.
Mtu aliyepata elimu na ufundi wa kila namna katika jumba la Farao (fananisha na kuzaliwa kama mwana wa Malkia wa Uingereza!), akapata kila akitakacho, akaishi kwa raha zote za wakati na uwezekano hata wa kuwa mrithi wa Farao, halafu mtu huyo siku moja kwa sababu ya tatizo fulani anaamua kuachana na utajiri, enzi, na fahari yote hiyo basi yawezekana alichofanya ni uamuzi wa kijinga, wa kibinafsi, na wenye kutaka kupandikiza chuki kati yake na watawala!
Hata hivyo, mwandishi anasema huu ulikuwa ni uamuzi uliofanywa na “mtu mzima”. Tukumbuke kuwa wakati Musa anaamua kuiacha nyumba ya Farao na kwenda kukaa na wana wa Israeli alikuwa na kama miaka 40 hivi. Kwa maneno, maamuzi yote aliyoyafanya kabla ya uamuzi huo, yalikuwa ni maamuzi ya “kitoto”. Maamuzi aliyoyafanya akiwa na miaka 20, miaka 30 au 37 au hata 39 yalikuwa ni maamuzi ya kitoto. Ni pale alipoamua kuacha nyumba ya Firauni hapo ndipo alipofanya hatimaye uamuzi wa “mtu mzima”.
Kwa maneno mengine, uamuzi wa mtu mzima hufanyika pale mtu anapojitambua kuwa yeye ni nani, ana makusudi gani na yuko upande gani kati ya watawala na watawaliwa, kati ya watesaji na watesao, katika ya walionacho na wasionacho, na kati ya mabwana na watumwa!
Hata hivyo mwandishi wa Waebrania anaongeza jambo jingine ambalo lilinifanya nirudie simulizi hili na kuamua kuwashirikisha Watanzania wenzangu tunapotazamia makadirio ya bajeti ya Serikali na wizara zinazoendelea mjini Dodoma kwa mwaka huu wa fedha, mwandishi anasema “Kwa imani, Musa alipokuwa mtu mzima alikataa kuitwa mwana wa binti Farao”.
Neno la kushikilia hapa ni “kukataa”. Ukisoma Kurani na ukisoma Biblia hutaona mahali ambapo Musa “anakataa” kuitwa mwana wa binti Farao (au mwana wa Malkia). Kwanini basi mwandishi wa Waebrania amepata wazo hili kuwa Musa “alikataa”?
Tafakari yangu imenifanya niamini kuwa mwandishi alielewa hulka ya wanadamu kukubali mambo ili kuwafurahisha watu wengine au kuwapendezesha watu fulani fulani.
Baada ya matatizo yake ya kumuua yule Mmisri na kumfukia mchangani na kumtetea Myahudi, siri ile haikuwa siri tena pale alipojikuta kuna mtu alishuhudia jambo hilo na kujaribu kulitumia dhidi yake. “Je, unataka kuniua mimi kama ulivyomuua yule Mmisri?” aliulizwa Musa na akajua siri yake imefichuka na akaamua kukimbia.
Bila ya shaka Farao na wakuu wake wa vyombo vya usalama kama vile TAKUKURU, Polisi, JWTZ, Kamati ya Ulinzi na Usalama walianza kumtafuta Musa yuko wapi (hapa hata mimi mwenyewe nimecheka!) Walipoambiwa kisa kilichomfanya akimbie nina uhakika walitoa matangazo na kutuma wajumbe kuwa “yote yamesamehewa na arudi nyumbani, kwani yeye ni wa nyumba ya Farao”. Yawezekana ahadi nono zilitangazwa na chombeza za kila namna kutumika.
Ni katika kuelewa hilo mwandishi wa Waebrania anasema “Musa alikataa kuitwa mwana wa Binti Farao”. Pamoja na kuitwa na kukumbushwa jinsi alivyosoma kwa utajiri wa Farao, jinsi alivyonufaika biashara zake na shughuli zake mbalimbali na jinsi gani atapoteza urithi wake katika nyumba ya Firauni, Musa alikataa kurudi.
Mwandishi anaongeza kitu kingine ambacho ndiyo msingi wa uamuzi wa mtu mzima wa Musa. Anasema “akaona ni heri (tafsiri nyingine zinatumia neno “akachagua”) kupata mateso na watu wa Mungu, kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo kifupi”.
Ndugu zangu msingi wa Musa kukataa kuitwa mwana wa binti Firauni ni uamuzi wa kuchagua kuwa upande wa watu wa Mungu ambao wanateseka.
Ni uamuzi wa kuona kuwa fahari na furaha yote ya anasa ya nyumba ya Farao havitoshi kumtia kiza kwenye macho yake asione mateso ya watu wa Mungu. Kwamba, pamoja na utajiri wote, elimu, na urithi uliokuwa mbele yake, asingeweza kuishi kwa furaha ilhali anajua kuwa watu wa Mungu wanateseka.
Watanzania wenzangu, mnaweza kufikiria nazungumzia habari za dini. Kwa namna fulani inaweza kugusa dini lakini hayo nitawaachia wachungaji, mapadre, mashehe na walimu mbalimbali wa dini. Mimi nazungumzia haja na ulazima wa watoto wa Tanzania kukataa kuitwa wana na mabinti wa Utawala wa Kifisadi! Simzungumzii Musa wa Biblia wala Farao wa Misri; siwazungumzii wana Waisraeli wa Mashariki ya Kati. Nazungumzia mahusiano kati ya watawala na watawaliwa wa hapa Tanzania.
Siku mpya imeanza na jua la neema limeanza kurusha miale yake kutoka pwani ya Bahari ya Hindi hadi kingo za Ziwa Tanganyika. Kutoka katika katika ardhi nyevu ya Mlima Kilimanjaro hadi kwenye kingo zing’arazo za ziwa Nyasa. Kutoka katika mashamba ya Karafuu kule Pemba hadi mashamba ya minazi ya pembezoni mwa Unguja. Siku mpya imeanza! Watu wazima wameanza kuchukua uamuzi wa kiutu uzima. Wameanza kuachana na maamuzi ya kitoto!
Kuna watu kati yetu leo hii wameamua kukataa kwa hiari yao wenyewe kuendelea kuitwa wana na mabinti wa nyumba ya Farao. Wameona ni heri na kwa hakika wamechagua kuwa ni bora kupata mateso na Watanzania wanaohangaika mchana kutwa na kuhenyeka kila kukicha kuliko kuishi katika utajiri na ufahari ambao wameuzoea na umewanogea.
Si kwamba kati yao hawapo wenye siri zao za mambo mabaya, au ambao wamewahi kuvurunda huko nyuma. Si kwamba wote wanaosimama leo hii kuwapinga mafisadi ni watu walio wasafi kabisa na hawana doa. Tukitarajia hivyo, ina maana tunatarajia malaika! Wengine tunayafahamu mambo yao, tunafahamu madhaifu yao, tunafahamu migogoro yao n.k Hata Musa alijulikana jinsi alivyomuua mtu na kumfukia mchangani na Mungu akamhurumia huyo Musa na kumpa unabii!
Lakini hawa wote leo wameamua kufanya uamuzi wa mtu mzima. Uamuzi wa kuwachagua Watanzania wanyonge, kuwatetea na kuwapigania mbele ya Farao. Ni uamuzi wa hatari, ni uamuzi wa kuudhi na kwa namna fulani unatishia kabisa nyumba ya Farao. Ndugu zangu, Sauti zao zinatoka kwenye kilichosemwa mwanzo na mwandishi wa Waebrania, “kwa imani”.
Hawajui vita hii itaishaje, hawajui hatima ya mambo yao yatakuwaje, na hawajui ni nani atakuwa msaliti wao. Lakini kwa imani wameamua kukataa kuendelea kuitwa wana wa binti Farao.
Kampuni zao zitapigwa mikwara kila kukicha, na mashamba yao yatavamiwa mbele ya Polisi, watafanywa duni kwenye hotuba za viongozi na kudhalilishwa kwa kuiacha nyumba ya Farao! Lakini, kurudi humo hawarudi tena!
Yupo Farao wetu. Ni utawala wa kisiasa ambao msingi wake ni kujipendelea. Ni wanasiasa (wana familia ya Farao) ambao wamejikita katika kula na kufuja mali ya umma, huku wakiuza urithi wa watoto wetu kama vile ni mali ya wanasiasa hawa. Tangu Loliondo, Mkomazi, Yeada Chini, na leo kwenye mambo ya Benki Kuu, wana wa Farao wameendelea kutesa na kunesa katika magari yao ya vita.
Muda huu wote wametegemea wana familia wote kuwa pamoja. Wametegemea kuwa watoto wa Farao watasimama na Farao. Wametegemea utajiri walio nao kuweza kuwanyamazisha wale wote ambao wangeweza kuibuka na kupaza sauti kuwatetea wale wateswao. Wamekosea.
Watawala hawa wenye mvuto wa Farao na nguvu ya majeshi kama ya Misri ya kale ambao wanaweza kutikisa vinavyotikisika na kusogeza vinavyosogezeka, leo hii wanajikuta wamegeukwa na wale walionufaika na hazina za nyumba ya Farao.
Tunashuhudia wabunge mahiri wakisimama kinyume na nyumba ya Farao, tena wengine wakisimama wakijua kabisa kuwa kwa kufanya hivyo wanaweza kufichuliwa siri za uchafu wao na kuwa majina yao yataharibiwa. Wapo wanaosimama ambao wanajua kwa kufanya hivyo wanaweka majimbo yao chini ya Farao na wapanda farasi wake. Ndiyo! Nyumba ya Farao imegawanyika na Farao na wakuu wake matumbo yamepata joto.
Wapo wanaofuatwa na makuwadi wa Farao ili warudi nyumbani. Wapo wanaobembelezwa kwa ahadi motomoto na michango ya kushinda uchaguzi. Wapo ambao wameahidiwa mbingu hapa duniani endapo tu wataamua kurudi nyumbani “kwao”. Sitoshangaa wapo watakaorudi na watakaoamua kurudi nyumbani kwa Farao, hao wanachothibitisha ni kuwa hawakuwahi kuondoka!
Lakini wapo wale ambao pamoja na kubembelezwa na kuimbiwa nyimbo na kutafutiwa sababu ya kuacha kukemea ufisadi wa farao wataendelea na watasema “ni heri kupata mateso na watu wa Mungu”! Hawa wako tayari kupoteza majimbo yao, wako tayari kupoteza heshima zao, wapo tayari kuoneakana wamekomolewa kuliko kurudi na kujifurahisha katika ufisadi kwa “kitambo”.
Hawa ndugu zangu wamefanya uamuzi wa mtu mzima. Ni matumaini yangu na kwa hakika ni dua na sala yangu kuwa mkutano wa bajeti unaendelea utatupa watu wa nyumba ya Farao watakaomua kutoka kwa Farao milele! Natumaini mkutano huu utaligawa Bunge rasmi kwa kuwapa ujasiri wale wanaositasita na kuwapa shime wale ambao wameshaamua kuondoka lakini bado mizigo yao iko ndani! Ili wafanye ule uamuzi wa mtu mzima; wa kukataa kuitwa mwana wa Farao!
Natumaini mkutano huu utasababisha tuyazungumze yote yale yanayohusiana na ufisadi. Ni lazima Meremeta, Deep Green, Mwananchi, Kiwira, Dowans, na wengine yafikie tamati hata ikilazimu kurudi kwa wananchi tena! Imetosha kukaa katika nyumba ya Farao! Natumaini kusikisia Bungeni wabunge wakikataa kuitwa wana wa binti Farao! Kwamba hawako tayari tena kuburuzwa kwa sababu ya kufurahia dhambi kwa kitambo!
Watanzania wenzangu, tuwaunge mkono wale waliofanya uamuzi huo. Tuwaunge mkono kwa kuwatia shime, tuwatetee pasipo woga na tusimame upande wao tukiona wanaonewa. Farao ameshaanza kupoteza nguvu yake na huko tunakokwenda anaweza kutumia nguvu ya wapanda farasi wake.
Lakini kabla hatujafika huko ni lazima tujiulize kwanza sisi wenyewe. Je mimi bado ni mwana au binti wa Farao? Kama bado nitaendelea hadi lini kufurahia vinafasi vya biashara, ujiko na viongozi, kusamehewa kodi, kula na wakubwa n.k katika nyumba ya Farao? Je wakati umefika kwa mimi nami kutoka nyumba ya Farao na kupata mateso na watu wa Mungu kuliko kufurahia maisha ya kifisadi kwa kitambo?
Ukifikiria maswali hayo zingatia jambo jingine kuhusu kuelekea nchi yetu ya Ahadi ya Tanzania Mpya; Kutoka nyumba ya Farao ni rahisi kwa mtu mmoja, kuamua kuacha Misri kwa maelfu ya watu ni jambo jingine kabisa.

No comments:

Post a Comment