KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Wednesday, 25 July 2012


Hongera Bw. na Bi. Slaa, haki ya maisha binafsi imetamalaki!

M. M. Mwanakijiji

NAWEZA kusema pasipo shaka yoyote kuwa hakuna watu ambao maisha yao ya nyumbani au chumbani yameingiliwa na watu wa nje katika miaka ya karibuni kama ilivyokuwa kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA ambaye pia ni mgombea aliyepita wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Willibrod Slaa.
Yeye pamoja na Bi. Josephine Mushumbusi wamepitishwa si tu kwenye tanuru la moto bali moto ulikuwa ni tanuru lao kwa sababu moja tu kubwa njia waliyopitia kuweza kuingia katika maisha ya ndoa ilikuwa imejaa vizuizi, vikwazo na mambo ambayo mtu mwingine yeyote yangetosha kabisa kumfanya asiendelee kutafuta faraja hiyo ya moyo katika ndoa.
Kwa yeyote aliyefuatilia kampeni za uchaguzi mkuu wa urais za mwaka 2010 anaweza kukumbuka vizuri jinsi taarifa za Dk. Slaa kuwa na Bi. Mushumbusi zilivyofanywa kuwa taarifa za kisiasa; zikizungumziwa na wanasiasa na kutumiwa kama silaha ya siasa.
Viranja wa maadili walisimama kubeza kwa kila namna na kwa kila nafasi uamuzi huowakikejeli uamuzi wa mioyo ya watu hawa wawili kuwa pamoja.
Sababu kubwa na bila ya shaka ya msingi sana ni kuwa wote wawili Dk. Slaa na Bi. Mushumbusi walikuwa wametoka kuachana na wenza wao ambao walikuwa wazazi wenza vile vile.
Hata hivyo katika hali ya ajabu sana na kwa kipimo kikali sana suala hili halikuachwa kwa wenza wao au wazazi wenza wao kulalamikia hili au kutafuta suluhu kuokoa mahusiano yao. Wanasiasa kutoka chama tawala, makuwadi wa mafisadi na hata wengine wa nje walijaribu kutolea maoni kwanini Dk. Slaa na Mushumbusi hawakupaswa kuwa pamoja.
Wapo ambao walikuwa wanazungumza kwa ukali kabisa wakisema kuwa kama hawa wawili wameamua kuwa pamoja ingewezekana vipi kwa Dk. Slaa kuweza kuja kuwa Rais. Na kwa watu wengine bila ya shaka walishawishiwa hivyo na kuona kuwa kweli Dk. Slaa hafai kuwa rais kwa sababu ameamua kuwa na Bi. Mushumbusi. Katika haya yote wale wasiohusika walikuwa na sauti kali zaidi, ya kebehi zaidi na wakiwa na uchungu wa mambo yasiyo yao.
Ni hapa ambapo Dk. Slaa alibezwa siyo tu kama mwanasiasa bali pia kwa vile aliamua kuacha daraja ya ukuhani katika Kanisa Katoliki na kuamua kufuata taratibu zote za kuacha.
Wengine walijaribu toka wakati ule na zaidi hata kwenye uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki kutumia hili kama kete yao ya kisiasa. Kila jina na kila tusi baya lilirushiwa kwa wapenzi hawa wawili kiasi kwamba ilikuwa ni jambo la aibu hata kufikiria jinsi maisha yao yanaingiliwa na watu wasiohusika; watu ambao kama vibao vingegeuzwa wasingethubutu kusimama.
Mimi ni mmoja wa wale ambao tunaamini kabisa kuwa kuna mambo ambayo ni ya mtu binafsi na ni lazima yaheshimiwe hivyo. Katiba yetu hii pamoja na upungufu wake mwingi imeweka kama moja ya tunu kulinda haki za maisha ya mtu binafsi kulindwa; wenyewe wanaita haki ya faragha (right to privacy).
Katika haki hii ya faragha manake ni kuwa serikali na watu wengine wanapaswa kuwa nje ya mazungumzo ya mtu, mahusiano yake binafsi na mambo ya nyumbani kwake kwa kadiri inavyowezekana. Isipokuwa pale ambapo labda kuna tetesi ya uhalifu au ushahidi wa uhalifu kutoweka ndio watu wa nje wanaweza kuingilia kati na serikali vile vile. Kwa mfano, mbakaji hawezi kudai “haki ya faragha” lakini watu wawili ambao hawana kizuizi cha sheria kuwa pamoja wanayo haki ya kulinda faragha yao.
Haki hii ya faragha inalindwa zaidi mtu anapokuwa nyumbani kwake wengine wanasema nyumbani kwa mtu ni mahali pake patakatifu. Mtu huwezi kwenda nyumbani kwa mtu na kuingia ndani bila kubisha hodi au kukaribishwa.
Hata rais hawezi kujipeleka nyumbani kwa mtu na kujiingiza ndani ati kwa vile ana vimulimuli! Polisi hawawezi na hawapaswi kuingia ndani ya nyumba ya mtu bila kibali, sababu au ruhusa ya kisheria kufanya hivyo. Mwananchi akiamua kumtwanga polisi aliyeingia nyumbani kwa nguvu naamini analindwa kikatiba kama polisi yule hakujitambulisha wala kuelezea kwanini anataka kuingia nyumbani kwa mtu na hasa kama hana waranti ya kumruhusu kufanya hivyo.
Hili ni kweli kwamba mtu akiwa nyumbani kwake anayo kinga ya kikatiba ya kuishi na kufurahia maisha yake binafsi. Tumeona kwenye magazeti kadha wa kadha jinsi ambayo watu wanaingiliwa hadi nyumbani kwao au wakiwa wameamua kutoka kwenye faradha ambayo haki ya faradha inadhaniwa (right to privacy is presumed). Kwa mfano, mtu akiamua kwenda safari na akapanga kwenye chumba basi pale chumbani kwake haki ya faragha inamlinda.
Haya ninayasema kwa sababu ninaamini haki ya faradha kwa Dk. Slaa na Mushumbusi ilifika mahali kwamba inatishiwa na wanasiasa wengine na hata viongozi wa serikali. Lakini sasa baada ya ndugu zetu hawa wawili kuingia katika ndoa haki hiyo siyo tu imetamalaki sasa inatakiwa kuwanyamazisha wale wote ambao walikuwa na ‘kiherehere’ cha kutaka kuvunja mahusiano ya watu hawa. Mioyo miwili ikipendana ni vigumu sana kutenganishwa.
Mambo haya ndio ninayaita “siasa za moyo”! Kwamba katika siasa za moyo kura ikishapigwa si rahisi kuchakachua. Mtu unaweza usipende watu wawili wawe pamoja, unaweza usifurahia kuwaona pamoja na kwa hakika kuwa kwao pamoja kunaweza kukukera wewe hadi kwenye mifupa.
Lakini kama watu hao hawana zuio la kuwa pamoja basi wewe inabidi ule jiwe na uyaache mambo yao yawe. Wakishindwana wenyewe wewe halikuhusu. Ni vizuri niseme kuwa kuna mambo ambayo mtu unaweza kufurahia kama ungeona yanatokea kwa namna fulani ili uone kama njozi inavyokuwa kweli lakini katika maisha halisi vitu wakati mwingine haviwi tutakavyo sisi. Wakati mwingine watu wapendanao hulipa gharama kubwa sana ili kuwa pamoja.
Ni nani ambaye hajawahi kusikia kisa cha msichana aliyewakaidi wazazi wake (matajiri) ili kuwa na mwanamume ambaye si tajiri kihivyo?
Ni wangapi tumewahi kusikia visa vya vijana wa dini tofauti ambao wameamua kuwa pamoja licha ya mapingamizi ya wazee au familia zao? Nani hajui kuwa kisa cha Malkia Elizabeth wa pili kuja kuwa malkia ni kwa sababu baba yake alimridhi kaka yake ambaye aliamua kuachilia kiti cha ufalme ili kuwa na mwanamke wa Kimarekani.
Tumeshasikia visa vya watoto wa matajiri huko Saudia ambao walitokea kupenda vijana wa Kimagharibi na wengine hata kukataa kurudi kwao Saudia (kuna kisa kinachoendelea sasa hivi cha binti wa mmoja wa watawala wa Saudia).
Hata hapa nyumbani wapo watu ambao wamekuwa pamoja tena wengine kwa maisha marefu (ninawafahamu baadhi ya wazee) baada ya familia zao awali kuwapinga. Na Dk. Slaa na Mushumbusi kwa hakika sio watu wa wanza ambao wamewahi kuwa na wenza/wazazi wenza na baadaye wakaamua kutoka katika maisha hayo kwa sababu zozote ambazo zilikuwa halali katika mioyo yao na kuanza mahusiano mapya.
Haya yote yanatufundisha mengi; kuna mafunzo katika yote haya. Ni matumaini yangu kwa watu wengi yote haya yanakuwa ni “muda wa kufundishika”. Unaweza ukachagua cha kujifunza kwa kweli; lakini kwa mwenye hekima yote mazuri na mabaya yamo ndani.
Ni kwa sababu hiyo binafsi nawapa pongezi na kuwatakia maisha marefu Bw. na Bi. Slaa. Ninawaombea baraka na fanaka zaidi katika maisha haya mapya na ni matumaini yangu waliokuwa na ya kusema sasa watafungwa vinywa vyao milele! Tuwaache ndugu zetu hawa wajaribu kutuliza mioyo yao na kulea familia zao.
Na mambo mengine ambayo hayajamalizika tutawapa muda tukiheshimu faragha ya familia zao waweze kuyatatua. Sidhani kama kuna yeyote kati yetu ambaye angependa kuingiliwa faragha ya maisha yake ya mapenzi namna hii na kujadiliwa majukwaani kama walivyofanyiwa haya.
Jamani, isije kufikiria viongozi wengine au watu wengine hawajulikani mambo yao. Kweli kabisa tukiamua siku moja tukifyatuka kuanza kuandika mambo ya viongozi hawa hawa wanaosimama kuhubiri “uzuri” wao watatukimbia. Tuandike ya wabunge wenye ndoa zao ambao wametelekeza na watoto vile vile watasimama? Tukiandika ya viongozi na wengine wa ngazi za juu tu ambao wana “visichana vyao” kwenye mashule yetu ya bweni humu mnadhani watasimama? Kweli kabisa tukifyatuka na kuelezea hizi “ziara” za huku na kule na wapambe wanaoenda na viongozi mngejua wanatanua vipi nao mbona ni kashfa za aina yake? Tena wengine hawa wanatumia hadi maofisi ya serikali kufanya uchafu wao! Siyo kwamba watu hawaoni au hawajui.
Nilipoandika kitabu changu cha “MAJERUHI WA MAPENZI” upande mmoja ni kuelezea kwa namna fulani suala hili la mapenzi katika maudhui yake mbalimbali. Ukiwakuta watu wanaogopa mapenzi ujue wana sababu, na ukikuta wengine hawatulii nao wana sababu na ukikuta mtu ameacha mapenzi na kutafuta upweke wa moyo nako kuna sababu.
Katika kitabu hiki tunakutana na vijana wawili ambao wanakutana huku kila mmoja akiwa na lundo la mizigo ya majeraha na makovu ya mapenzi. Kwa kila kipimo vijana hawa (Erica Tossi na Dk. Shedrack) hawana nafasi ya kuweza kudumu katika mapenzi hasa kwa vile wote wanaingia wakiwa wameumizwa kila aina ya vionjo.
Simulizi hili kwa kiasi kikubwa linatokana na baadhi ya matukio ya kweli ambayo yamewahi kutokea. Lakini lina lengo kubwa sana la kumfanya mtu afikiri zaidi katika masuala haya. Kila uamuzi ambao mtu anachukua una matokeo yake na mojawapo ndio haya ya watu kuwa majeruhi wa mapenzi.
Kitabu hiki kinapatikana kwa bei ya sh 18,000 tu. Hivyo, si kitabu cha watu ambao hawapendi kujisomea. Kina kurasa nyingi (si chini ya 250) na hivyo kitabu hiki si cha wavivu wa kusoma, yaani watu ambao wakiona ukurasa mmoja wanaona ni “maneno meeeeengi”. Na kwa hakika si kitabu cha watu ambao wanapenda vya chee. Kina gharama na hivyo kwa yeyote anayetaka kukisoma ni lazima awe mtu ambaye anapenda kujisomea si mvivu wa kusoma kwa hakika si mtu bahili.
Bahati mbaya sana kitabu hiki kwa makusudi kabisa hakipatikani kwenye maduka makubwa ya vitabu. Kwa sababu mbili kwanza ni kwa sababu tumetoa nakala chache sana kwenye toleo hili la kwanza kutokana na gharama kubwa za kuchapisha nchini. Lakini pili ni kwa sababu tumetoa nakala kubwa (Big Paperback). Karatasi zake ni za kiwango cha juu na maandishi yake ni makubwa kwa mtu yeyote kuweza kusoma bila kuhitaji miwani. Lakini pia ni kwa ajili ya watu wazima kina maudhui ya watu wazima hivyo siyo kitabu cha kumtuma mtoto wa shule ya msingi kuanza kukisoma.
Watu watakaokipata kwa haraka sasa hivi ni wa Dar-es-Salaam, Mwanza, Mbeya na Songea na vile vile watu wa Dodoma. Kwa wakazi wa Dar wanaweza kukipata Mlimani City kwenye duka la Modern Day Boutique ambalo linapatikana kwa namba 0718966885 na vile vile kwenye duka la Trustmark Investment liliko kona ya Ally Hassan Mwinyi na Kawawa maeneo ya Kinondoni mkabala na nyumba za polisi za Oysterbay. Duka hili linapatikana kwa namba 0716791177.
Kwa wakazi wa Mwanza wanaweza kupata kwa kupiga simu 0762404820, wakati wale wa Mbeya wanaweza kupiga simu namba 0752055160 huku wa kule Songea wanaweza kupiga nambari 0754952119. Kote huko ni muhimu kupiga kujua kama bado wanazo nakala kwani siwezi kuahidi kuwa kila atakayetaka nakala anaweza kupata.
Ni matumaini yangu kitabu hiki kwa namna moja kitasaidia watu wengine kuweza kuona vile vile changamoto za mioyo ya watu na jinsi gani kumhukumu mwingine kwa maamuzi yake siyo tu ni kujipa uwezo wa kimungu lakini pia ni kujiona bora zaidi kuliko wengine.
Natumaini kitakuwa ni burudani kwa wasafiri, faraja kwa wapendanao, onyo kwa wengine, na chanzo cha kujisahau kidogo mtu na matatizo yake na kuingia katika ulimwengu wa Erica na Shedrack. Kama mmoja wa wasomaji alivyosema ni “Riwaya ya Mwaka”.
Kila la kheri kwa wasomaji wa gazeti hili na hasa pia wasomaji wa kitabu hiki ambacho ni mwanzo wa riwaya kadhaa za mapenzi, siasa, vitisho na ushujaa kutoka kwa wenu mtiifu. Na kila la heri Dk. Slaa na Bi. Josephine Slaa!

No comments:

Post a Comment