• Wabunge wala rushwa kuanikwa hadharani
na Edson Kamukara, Dodoma
TUHUMA za rushwa zilizotolewa na baadhi ya wabunge dhidi ya wenzao katika
Wizara ya Nishati na Madini, zimemfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuridhia
kuvunjwa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Hatua hiyo inatokana na baadhi ya wajumbe wake kukumbwa na tuhuma za kupokea
hongo kutoka kwa baadhi ya kampuni za mafuta ili kuficha ufisadi wa vigogo ndani
ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Mbali na kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Bukene, Seleman Zedi (CCM),
pia Makinda ameahidi kuchukua uamuzi kama huo
kwa kamati nyingine zitakazobainika wajumbe wake walihusika katika sakata
hilo.
Licha ya kutozitaja kwa majina kamati hizo lakini wabunge wengi walionekana
kuzitaja Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) inayoongozwa na Mbunge wa
Vunjo, Augustine Mrema (TLP) na ile ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) iliyo
chini ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA).
Wabunge wanadai kuwa LAAC imekuwa na tuhuma nyingi za wajumbe wake kuomba
rushwa kwa wakurugenzi wa halmashauri wakati ile ya (POAC), inaelezwa kuwa
baadhi ya wajumbe wake walionekama kufanya juhudi za kumkingia kifua aliyekuwa
Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, William
Mhando.
Spika Makinda alifikia uamuzi huo jana bungeni kutokana na hoja
iliyowasilishwa na Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM) na kuungwa mkono na
wabunge takariban wote, akitaka kamati hiyo ivunjwe, vile vile wabunge
waliohusika kwenye sakata hilo wachunguzwe na kuchukuliwa hatua.
“Mheshimiwa Spika, naomba kutumia kanuni ya 53 (2) pamoja na 55 (3)(f)...
katika michango ya wabunge wengi kwenye wizara hii walitoa tuhuma nzito kwa
baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini na wabunge
wengine kuwa walipokea rushwa ili kuipigia debe TANESCO.
Kwa kuwa tuhuma hizi ni nzito na zinatudhalilisha wabunge na Bunge lako
tukufu, naomba utumie mamlaka yako kwa mujibu wa kanuni ya 5 (1) kuivunja Kamati
ya Nishati na Madini na zile zilizopata kutuhumiwa halafu uiagize Kamati ya
Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge tuhuma za wabunge zichunguzwe na wachukuliwe
hatua...naomba kutoa hoja,” alisema Kawawa.
Baada ya kutoa hoja hiyo, Spika Makinda alisimama na kukiri kuwa hoja hiyo
imeungwa mkono na iko wazi, akibainisha kuwa si kwa jambo hilo tu bali kwa siku
zilivyokuwa zikienda mienendo ya baadhi ya wabunge ilikuwa ikilidhalilisha
Bunge.
“Nimeiomba Kamati ya Maadili ituandalie kanuni za maadili (code of ethics)
ili wabunge watakaopatikana na makosa wachukuliwe hatua kwa kutumia kanuni
hizo...lakini hata wale wanaowatuma na kuwahonga, pia tunataka wachukuliwe
hatua.
“Unakuta mbunge anatoka jasho humu ndani akizungumza kumbe ametumwa na watu
huko nje ili kutetea masilahi yao baada ya kupewa fedha,” alisema Makinda.
Alisema kwa sasa serikali iko kwenye kipindi cha mpito katika kutatua kero za
wananchi, hivyo Bunge kama chombo kinachoheshimika kinapaswa kuishauri serikali
na si kutumika kwa masilahi ya watu binafsi.
“Natumia pia mamlaka yangu kuivunja Kamati ya Nishati na Madini na zile zote
zinazotuhumiwa, ikibainika nazo nitazivunja,” alisema Makinda na kushangiliwa na
wabunge.
Hata hivyo kabla ya kufikia uamuzi huo, wabunge wengi walifanya juhudi za
kumshinikiza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kuwataja kwa
majina wale waliohongwa na kuwatisha watendaji wa wizara bila mafanikio.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), Kangi Lugora wa Mwibara
(CCM), John Shibuda wa Maswa Mashariki (CHADEMA) na Ali
Keissy wa Nkasi ni miongoni mwa wabunge wengi walioshinikiza majina hayo kutajwa
wakidai hatua ya kuwaficha ni kuendelea kuwadhalilisha wabunge wote.
Nao wabunge, Pudenciana Kikwembe, Vicky
Kamata, Josephat Kandege, Said Zuber wa Fuoni (CCM) na Naomi Kaihula (CHADEMA),
walipendekeza watuhumiwa hao wafilisiwe, huku Zuber akitaka wanyongwe au kupigwa
risasi na vifaa vitakavyotumika kuwaua wavigharamie wao.
Hotuba ya Nishati
Hata hivyo idadi kubwa ya wabunge waliochangia bajeti hiyo walionekana
kutekwa na sakata la TANESCO na kusahau kuchangia masuala muhimu ikiwamo
uchimbaji wa urani pamoja na gesi asilia.
Hotuba ya mwaka huu imekuwa tofauti na ya mwaka uliotangulia ambapo wabunge
wengi waliisulubu serikali kwa kushindwa kutoa fedha za kutosha kwa wizara hiyo
hasa kwa TANESCO ambayo ilidaiwa haina fedha za kuiwezesha kuzalisha umeme wa
kutosha.
No comments:
Post a Comment