KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Monday, 23 July 2012



Chuji aache akili iitume miguu yake

Kenneth Mwaisabula

WIKI mbili zilizopita, makala zangu zilijikita kwenye suala zima la makocha wa nchi hii.
Ingawa niliahidi kuwa leo hii ningetoa zaidi maoni ya wadau walioniandikia, lakini kutokana na uwepo wa michuano ya Kombe la Kagame, upepo unanifanya nijielekeza huko.
Leo, nitajaribu kumzungumzia Kiungo Athuman Iddy ‘Chuji’ kwa jinsi ninavyomwona akifanya vitu vyake katika michuano hiyo iliyofikia hatua ya robo fainali.
Nimepata kuwaona viungo wengi ndani ya nchi ambao kamwe siwezi kuwasahau, nimepata kuwashuhudia Sunday Manara ‘Computer,’ Nico Njohole, Ramadhan Lenny, Hamis Tobias Gagarhino, Method Mogela ‘Fundi,’ Mtemi Ramadhan, Aluu Ally, Hussen Amani Masha, Ally Maumba, Machael Paul “Nailon,” Hasara Kasimu “Baba Kivumbi’ na Halfan Ngasa.
Hata ungeniamsha usingizini, nitakweleza hao walikuwa mafundi wa kweli dimbani.
Kizazi hicho kimepotea na kupunguza hata mshawasha wa baadhi ya wapenzi na mashabiki kwenda uwanjani.
Lakini, si kweli kama samaki wote wakioza ni wote, hivyo hata katika kizazi cha leo, kuna nyota kadhaa ambao wanafanya vitu vya uhakika.
Nikiri kuwa kati ya hao wachache, Haruna Moshi ‘Boban’na Chuji, ni miongoni mwao, ingawa leo nitajielekeza zaidi kwa Chuji.
Niseme Chuji ni mtambo wa aina yake na ndiyo maana akili yangu huwa inakataa na kuhoji ni vigezo gani vinavyomweka nje ya kikosi cha timu ya soka ya taifa, Taifa Stars.
Baada ya kutafakari kwa kirefu, nadhani tatizo lake ni akili ya kiungo huyo kutofanana na miguuni yake.
Miaka miwili iliyopita, kupitia moja ya makala zangu niliwahi kuandika nikisema, wakati wa Chuji kucheza nyumbani, ulishapita isipokuwa soka ya kulipwa.
Chuji sasa angekuwa Ulaya akigombana na baridi kali ya mwaka mzima, ubaguzi wa rangi na vita ya namba.
Nilifarijika baada ya Chuji kuisoma makala na kunipigia simu na kuniambia Mzazi nipe mwezi mmoja tu utanisikia nashukuru kwa ushauri, lazima niondoke.
Hivi karibuni, nimeshuhudia Chuji akifanya mambo yale yale nabaki nimeduwaa, nadhani Chuji ana kila sababu ya kuzifanya akili zake zifanye kazi ya kuiambia miguu yake, nikiamini itamtii.
Chuji ni aina ya wachezaji wenye kila kitu miguuni mwao kiasi cha kuitwa nyota wa kiwango cha kimataifa.
Kwa lugha nyingine ya kitaalamu zaidi, tungesema ana B zote 3, hivi Chuji utampanga namba ipi asiweze kucheza?
Ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi ndefu na fupi kwa uhakika, ana nguvu ya miguu kwa kupiga na kukaba, ana uwezo wa kufunga na kuzuia; unataka nini kwa mchezaji wa aina yake?
Tatizo ninaloliona kwa Chuji ni akili yake kuamua: “Sasa nataka kucheza mpira.”
Lakini pia huenda watu waliomzunguka si washauri wazuri kwake.
Chuji anatakiwa apange muda maalum kwa kazi moja tu ya mazoezi, ajiepushe na mambo ya nje ya uwanja kama vile ulevi ambao sina hakika kama anatumia, uasherati ambao pia sina hakika kama kajikita sana.
Aidha, atapaswa kuwa na muda mwingi wa kupumzika kuliko kushinda katika majumba ya starehe akiponda maisha, nidhamu ya uwanjani ndio njia pekee itakayomtoa hapo alipo na kwenda zake ughaibuni kula bata wake.
Usajili wa Yanga msimu huu utamfanya Chuji kama kweli anataka kucheza mpira akaonekana kweli kwani pale katika dimba la kati atapangiwa na wataalamu wenzake kama vile Rashid Gumbo ‘Chidi’ Haruna Nyozimana ‘Fabregus’ pia wapo kina Nizzar Halfan, Frank Dumayo, Simon Msuva. Hapo utamtaka Chuji ubaya lakini tatizo langu kwake ni je akili yake iko tayari kucheza mpira?
Maana miguu yake haina matatizo inamsubiri aitume kazi kupitia akili yake ya kichwani.
Huenda Chuji akawa hajijui kama anajua, lakini mbaya zaidi hajui kama ujana ni maji ya moto, kina Ally Mayai, Edibily Lunyamila, Fikiri Magoso ukikutana nao wanalia wanatamani warudishe umri nyuma, waikute awamu hii ya kwako ya utandawazi ambayo unacheza leo dunia nzima inakuona, unataka nini tena?
Soka la leo Chuji ni zaidi ya soka, unaweza leo ukalala maskini kesho ukaamka tajiri na dunia ikawa inakusema, inakutaja, inakuabudu.
Mbwana Samata kacheza mechi hazikuzidi kumi ndani ya Simba leo anazungumziwa na mataifa yote duniani hilo ndio soka, anakula fadhila ya akili yake kuiambia miguu yake ifanye akili inavyotaka ndio maana nasema soka ni zaidi ya soka.
Chuji atambue kuwa yote kwa yote hakuna kazi mbaya duniani kama kucheza mpira maana ukifika miaka 35 unaambiwa mzee kaa pembeni, hivyo ni wakati wako sasa kucheza na umri na kupigana na wakati na ninaamini wakati uliobaki kwako ni mdogo mno hivyo pigana leo ili kesho upumzike angalau vizuri kidogo.
Michuano ya Kagame sio tu itampa mwanga Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen, kujionea vipaji, pia ni fursa ya kuonekana kupitia Super Sports.
Nasisitiza kuwa nimewaona viungo wengi wanaocheza nafasi ya kiungo, lakini kwangu Chuji ni mmoja kati viungo bora waliopita katika macho yangu.
Niliutambua uwezo wake zaidi ya miaka 13 nyuma alipokuwa akicheza Polisi Dodoma ambayo ilipocheza na Yanga, hata kama ilifungwa 3-2, ilikuwa ni shughuli nzito.
Nadhani mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Yanga, Aaron Nyanda, atamkumbuka maana ndiye aliyekuwa anakabana naye wakati huo.
Ni mchezaji mwenye kiwango bora, mara zote akili yake ikiamua mashabiki wanamkubali lakini akili yake ikikataa, ndio basi tena.
Kwa vile sasa naona dalili zote za akili yake kukubali kucheza mpira, basi nami namwambia akili hiyo iendelee dunia itamtambua bado ni kiungo asiye na mfano.
Akili yako Chuji sasa ipeleke katika miguu yako.

No comments:

Post a Comment