Mtayarishaji wa Vipindi ambae pia ni Mtangazaji wa Zenji F.M Mustapha Mussa akimuuliza swali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  kuhusiana na masuala mbali mbali ya Maendeleo, Kijamii na Kisiasa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiahidi kuendelea kuitumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa wakati akihojiwa na Zenji F.M Hapo Nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Licha ya kuwepo kwa Uhuru wa kutosha wa Kuabudu na kupata Habari Miongoni mwa Jamii kufuatia kutanuka kwa Demokrasia  Nchini, lakini bado Wananchi wanapaswa kuzingatia kwa makini utumiaji wa fursa hiyo katika kulinda umoja na Mshikamano uliopo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameeleza hayo Nyumbani Kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, wakati akizungumza na Kituo cha Matangazo ya Redio cha Zenji F.M kuhusiana na masuala mbali mbali ya Kijamii, Kisiasa, Maendeleo, Kiuchumi likiwemo pia  suala kubwa  la Amani ya Nchi.
Balozi Seif amesema Zanzibar imepita katika majaribu mengi ya kukosa utulivu na amani hasa katika mivutano ya Kisiasa ndani ya mfumo wa vyama vingi na kuibuka kwa migogoro ya matokeo  ya uchaguzi iliyopelekea kudumaa kwa Maendeleo na Ustawi wa Jamii.
Ameshauri Uhuru huo wa kuabudu utumiwe vizuri ili kuepuka upotoshaji unaoweza kuleta athari na hatimaye kuvurugika kwa amani ambayo huchukuwa muda mrefu kuirejesha.
Balozi Seif amefahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayofuata Muundo wa Umoja wa Kitaifa, imesaidia kwa kiasi kikubwa kuleta utulivu wa Kisiasa uliokosekana kwa kipindi kirefu hali iliyochangia kuongezeka kwa wawekezaji kuweka vitega uchumi vyao Zanzibar.
Amewakebehi baadhi ya Watu wanaodhani kwamba yeye hauungi mkono muundo wa Serikali iliyopo hivi sasa wa Umoja wa Kitaifa, jambo ambalo alikuwa na fursa na haki ya kujiuzulu kama alikuwa hakubaliani na Muundo huo.
Akizungumzia mchakato wa Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Seif amesema Wananchi lazima watumie kwa makini fursa hiyo ya kutoa Maoni yao kwa vile muundo wa katiba ipi inahitajika na Wananchi hao limo ndani ya uamuzi na mamlaka yao.
Akigusia tuhuma alizobebeshwa za kuhusishwa na vurugu za Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Bububu, Balozi Seif ameelezea kusikitishwa kwake na tabia ya baadhi ya Vyombo vya Habari kutumia kalamu zao kumvurugia Heshima yake.
Amesema yeye kama Kiongozi daima hataweza kwenda kinyume na Maadili ya Uongozi kwa vile tayari ameshakubali kubeba dhima hiyo kwa kula Kiapo cha  kuwatumikia Wananchi wote akiwa kama Kiongozi Mkuu wa Shughuli za Serikali.