TAMKO LA WAZIRI MKUU KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA KIMATAIFA YA UPUNGUZAJI WA ATHARI ZA MAAFA DUNIANI LEO.
Ndugu Wananchi, leo tarehe 12 Oktoba, 2012 ni Siku ya Kimataifa ya Upunguzaji wa Athari za Maafa(International Day for Disaster Reduction). Siku hii huadhimishwa tarehe 13 Oktoba ya kila mwaka.
Hata hivyo, kwa mwaka huu Sekretariati ya Kupunguza Athari za Maafa ya Umoja wa Mataifa, imeelekeza kuwa siku hii iadhimishwe leo siku ya Ijumaa Oktoba 12, 2012. Kama ilivyo kwa miaka yote tangu siku hiyo ilipoanzishwa katika miaka ya 1990, Sekretarieti hiyo hutoa Kaulimbiu ya mwaka husika. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema, “WANAWAKE NA WASICHANA – NGUVU ISIYOONEKANA KATIKA KINGA DHIDI YA MAAFA” (WOMEN AND GIRLS –THE INVISIBLE FORCE OF RESILIENCE).
Siku ya Kimataifa ya Upunguzaji wa Athari za Maafa kwa mwaka huu imewalenga Wanawake na Wasichana kwa lengo la kutambua na kukubali mchango unaotolewa katika jamii na mamilioni ya Wanawake na Wasichana katika kukabili athari za maafa na Mabadiliko ya tabia nchi na hivyo kuleta manufaa katika shughuli za maendeleo na uwekezaji.
Ndugu Wananchi, mtakubaliana na mimi kwamba mafanikio makubwa yatokanayo na nguvu za wanawake na wasischana hayatambuliwi kwenye shughuli za maafa na katika kufanya maamuzi kutokana na kutokutambua mchango wao katika jamii. Kwa kulitambua hili ndiyo maana ujumbe wa mwaka huu unasisitiza kutambua ushiriki wa wanawake na wasichana katika kulinda na kujenga jamii kabla na baada ya Maafa.
Ndugu Wananchi, lengo kubwa la kaulimbiu ya mwaka huu ni kuamsha uelewa wa wananchi katika masuala yafuatayo:-
i. Jamii kutambua mchango wa Wanawake na Wasichana kabla, wakati na baada ya Maafa;
ii. Kuainisha uwezo wa Wanawake na Wasichana unaokwamishwa kwa kutokushirikishwa katika shughuli za upunguzaji wa athari za maafa na katika kutoa maamuzi kwenye ngazi za uongozi pamoja na mipango ya progamu na uelewa mdogo wa jamii juu ya usawa wa jinsia;
iii. Kuondokana na mtazamo kwamba daima wanawake na wasichana ndiyo waathirika wakubwa wa maafa; na
iv. Kudhihirisha vielelezo vya shughuli na jitihada zinazofanywa na Wanawake na Wasichana katika kukabiliana na maafa.
Ndugu Wananchi, napenda nielezee hatua chache zilizochukuliwa na Serikali yetu kuwezesha ushiriki wa wanawake katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na shughuli za upunguzaji athari za maafa katika ngazi za kisiasa na kutoa maamuzi kwa kuwapa fursa ya moja kwa moja katika kusimamia Ofisi za Umma zikiwamo Wizara, Taasisi na Idara pamoja na kutambua umuhimu wao katika uandaaji wa sera, mikakati na mipango ya kiuchumi.
Ushiriki wa wanawake katika ngazi za uongozi wa kisiasa mathalan, Wabunge Wanawake wameongezeka kutoka asilimia 11 mwaka 1990 hadi kufikia asilimia 36 mwaka 2011. Kwa upande wa Mawaziri waliongezeka kutoka asilimia 12 mwaka 1990 hadi kufikia asilimia 27.5 mwaka 2011. Aidha, kwa mara ya kwanza mwaka 2010 katika historia ya nchi yetu aliteuliwa Mwanawake kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano waTanzania. Kwa upande wa Wakuu wa Mikoa wameongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 29 mwaka 2012 wakati Wakuu wa Wilaya wameongezeka kutoka Asilimia 19 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 32 mwaka 2012. Kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004, Wakuu wa Mikoa na Wilaya ndiyo Wenyeviti wa Kamati za Maafa katika ngazi zao.
Katika ngazi ya uongozi wa kiutendaji, Majaji wanawake wameongezeka kutoka asilimia 6 mwaka 1990 hadi kufikia asilimia 35 mwaka 2011. Wakurungezi wa Halmashauri wameongezeka pia kutoka asilimia 6 mwaka 1991 hadi kufikia asilimia 26 mwaka 2011. Tukizingatia Sera yetu ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004, Wakurugenzi hao ndiyo Makatibu wa Kamati za Maafa za Wilaya zao ambazo zina majukumu ya kusimamia masuala ya maafa katika maeneoyao.
Ndugu Wananchi, ili kuamsha uelewa wa jamii kutambua na kukubali umuhimu wa wanawake na wasichana katika kukabili na kupunguza athari za maafa na mabadiliko ya tabia nchi, Serikali imewezesha uingizaji wa masuala ya jinsia katika Sera na Mikakati ya maendeleo. Lengo la hatua hii ni kufikia usawa wa jinsia kwa kuanzisha jumla ya Madawati ya Jinsia 188 katika Wizara 26, Wakala za Serikali Saba, Sekretariati za Mikoa 21, Halmashauri 133 na Idara inayojitegemea moja.
Aidha, Serikali imewajengea uwezo wanawake kupitia mafunzo ya fani mbalimbali yaliyofadhiliwa na Mfuko wa Mafunzo kwa Wanawake Tanzania (TFTW). Jumla ya wanawake 445 waliwezeshwa kupata mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika fani za sheria, uongozi na utawala, mipango, sayansi na teknolojia, ushauri nasaha, ujasiriamali na jinsia.
Vilevile, kwa kuzingatia kuwa wanawake walikuwa wameachwa nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na wanaume, serikali imefanikiwa kutekeleza hatua mbalimbali za kuwawezesha wanawake kiuchumi. Hatua hizo ni pamoja na kuanzisha na kuendesha Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake mnamo mwaka 1993 kwa lengo la kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake kupitia Halmashauri za Wilaya. Hadi sasa kiasi cha Shilingi 2,005,234,000/- kimekopeshwa kwa wanawake 40,105 katika Halmashauri zote 134 nchini. Aidha, katika kuwajengea wanawake na wanaume uwezo, Benki ya WanawakeTanzaniahadi kufikia tarehe 31 Mei, 2011 ilitoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wateja wake kabla ya kuwapatia mikopo wajasiriamali 5,246 wakiwemo wanawake 4,358 na wanaume 888.
Ndugu Wananchi, Taarifa ya Dunia ya Tathmini ya Upunguzaji Athari za Maafa ya Mwaka 2011 (Global Assessment Report on Disaster Risk Reduction (GAR) 2011), inabainisha kuwa nchi nyingi duniani ikiwemoTanzania zinakubaliana kuwa kukosekana kwa utaalamu wa kuingiza masuala ya jinsia katika mipango ya maendeleo imekuwa ni kikwazo kikubwa cha kinga dhidi ya maafa. Ripoti hii imeonesha kuwa asilimia 26 ya nchi ikiwemo nchi yetu ndizo zilizotoa taarifa ya umuhimu wa kujikita katika masuala ya jinsiakama chachu ya maendeleo.
Ndugu Wananchi, kuna vipengele vitatu katika kampeni hii ambavyo ningependa Wizara, Taasisi na Idara za Serikali pamoja na Wadau wote wa Maendeleo kwa kushirikiana na wananchi wavizingatie ili nguvu ya wanawake katika kinga dhidi ya maafa ionekane. Vipengele hivi vinatokana na ujumbe muhimu wa Siku ya Kimataifa ya Upunguzaji Athari za Maafa 2012 ambavyo ni:
- Wanawake na Wasichana Wawezeshwe kwa Usalama wa Kesho Wanawake na Wasichana wawezeshwe katika kuchangia kuleta maendeleo endelevu kwa kupunguza athari za maafa, hususani katika utunzaji wa mazingira na usimamizi wa mali asili, utawala na mipango ya matumizi ya ardhi na miji pamoja mipango ya kiuchumi na kijamii ambayo ndiyo mihimili ya kinga ya maafa.
- Wananawake na Wasichana Nguvu Kuu ya Mabadiliko
Ilijitihada za upunguzaji wa athari za maafa ziweze kuleta matokeo mazuri ni vyema jamii iwashirikishe Wanawake na Wasichana katika uandaaji na utekeleji wa sera, mipango na mikakati ya kinga dhidi ya maafa.
Asilimia 52 ya watu Duniani ni Wanawake na Wasichana, kwa upande waTanzaniani asilimia 51 ambao ni miongoni mwa waathirika wa maafa. Hapa nchini inakadiriwa kwamba wanawake hasa wa Vijijini wanatoa Asilimia 80 ya wafanyakazi katika kazi hasa za mashambani na hivyo kutoa Asilimia 60 ya chakula kinachozalishwa.
Hivyo uzoefu, ujuzi na uelewa wao ni muhimusanakatika mikakati na shughuli za Upunguzaji wa Athari za Maafa na kuhimili mabadiliko ya tabia nchi. Mchango ya Wanawake na Wasichana utakuwa na matokeo mazuri iwapo watashirikishwa katika hatua zote za menejimenti ya maafa.
- Jamii yenye Kinga Dhidi ya Maafa ni Jamii Inayojali Jinsia
- Kutokuwa na Usawa wa Jinsia ni Udhaifu – Kuimarisha Usawa wa Jinsia ni Kuimarisha Kinga Dhidi ya Maafa
Kutokuwa na usawa wa jinsia unawaweka wanawake, watoto na jamii nzima katika hatari pindi majanga ya asili yanapotokea. Kwa hali hiyo tujenge na kuboresha kinga dhidi ya maafa kwa kutoa elimu kwa uwiano sawa wa jinsia.
-Itambulike Kuwa Uwiano Sawa wa Jinsia Unaanzishwa na Elimu Wanawake na Watoto lazima washiriki katika kufahamu jinsi ya kujiandaa, kukabili na kupunguza athari za maafa katika jamii. Hili litawezekana kwa kuwaelimisha wavulana na wasichana katika rika zote. Wanaume na wavulana wakihusika wataweza kuondoa vikwazo vinavyowazuia wanawake na wasichana kushiriki katika mzingo mzima wa upunguzaji athari za maafa.
-Wanawake na Wasichana ni Njia Bora ya Kutoa Taarifa Njia sahihi ya mawasiliano ni ile inayohusisha pande mbili kwa kushirikisha sauti za Wanawake na Wanaume katika kujiandaa, kukabili na kupunguza athari za maafa. Hivyo, jamii itaweza kuwa na uwezo wa kujikinga dhidi ya maafa na kupata maendeleo endelevu.
Ndugu Wananchi, pamoja na mambo yote haya kama tutaongeza mkazo katika kutambua mchango unaotolewa na Wanawake na Wasichana kwa kuwashirikisha katika kuandaa na kutekeleza shughuli za Upunguzaji wa Athari za Maafa na kutoa maamuzi kwenye ngazi za uongozi pamoja na mipango ya progamu, sera na mikakati tunaweza kuiona nguvu ya wanawake katika kinga dhidi ya maafa. Natoa wito kwa Viongozi wote katika Wizara, Idara, Taasisi zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri ziendelee kuzingatia masuala ya jinsia katika Sera na Mikakati na Mipango yao ya maendeleo kwa lengo la kufikia usawa wa jinsia ili nguvu ya Wanawake na Wasichana katika kinga dhidi ya maafa ionekana dhahiri kwa jamii. Ikumbukwe kuwa, jukumu la kupunguza athari za maafa ni la jinsia zote. Kila mmoja pale alipo atimize wajibu wake.
ASANTENI SANA
Mhe. Mizengo P. Pinda (Mb)
WAZIRI MKUU
No comments:
Post a Comment