KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Wednesday, 10 October 2012


MGIMWA ALISHAURI SHIRIKA LA FEDHA LA KIMATAIFA KUPUNGUZA MASHARTI YA MIKOPO INAYOKOPWA NA NCHI ZINAZOENDELEA.


Shirika la fedha la kimataifa (IMF) hujishughulisha na kutoa ushauri wa kisera kwa nchi wanachama na kutoa mikopo na misaada ya kifedha. Hayo yamesemwa na Mhe. Mgimwa jijini Tokyo- Japan. Akishiriki kikao cha kundi la Africa (African Group one Constituency),aidha, Mheshimiwa Mgimwa aliwasilisha hoja kwa niaba ya Magavana wa Afrika, na mbele ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IMF Bwana Shinowara, ya kulitaka shirika hilo kupunguza kiwango cha kigezo cha kukopa ili kuruhusu Nchi zinazoendelea kupata unafuu na kuziwezesha kukopa fedha za kufadhili kwa miundombinu ya Barabara, Reli na Bandari.
Mhe. Mgimwa alisema kuwa, mkutano huo uliangalia uhalisia na vigezo vinavyotolewa na Shirika la Fedha la kimataifa kuruhusu nchi wanachama kukopa tu katika ukomo wa sasa wa asilimia 35 na zaidi (Concesionality). Aliendelea kufafanua kwamba, jambo kubwa ni kuangalia jinsi ya  kuboresha taratibu  za kukopesha katika mikopo nafuu. Aidha, wajumbe wa mkutano wamekubaliana na haja ya kuwepo kwa utaratibu wa kuhakikisha kuwa nchi zote zinakuwa na madeni yanayohimilika”. Alisisitiza Mgimwa.
Wakijadiliana katika mkutano huo wajumbe hao wameshauri Shirika la fedha la kimataifa pamoja na taratibu zake, liangalie namna ya kulegeza masharti ya mikopo ili nchi wanachama ziweze kuboresha  miundombinu.
 “ IMF walau itizame aina ya miradi yenye chachu ya ukuwaji wa uchumi ambayo inaweza kutizamwa kwenye viwango vya ukopaji vya chini ya asilimia 35”.Aliongeza Mgimwa.
“Tunashukuru kuwa IMF imekuwa ikitupatia mikopo ya masharti nafuu, mikopo ile ya mapumziko ya miaka saba kabla ya kuanza kulipa na yenye riba ndogo sana na yenye masharti nafuu”. Mgimwa alisisitiza.
Akitolea mfano wa mradi wa gesi wa Tanzania, Mgimwa alisisitiza kuwa upatikanaji wa gesi utaongeza uzalishaji, ajira na viwanda. Kuongezeka kwa ajira kutaongeza kukua kwa pato la Taifa. Hii itasaidia kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa nchi ya Tanzania na hata  Afrika kwa ujumla.
Mikutano hiyo bado inaendelea hapa jijini Tokyo-Japan na nchi wanachama wanaendelea kuja kwa wingi.
Imetolewa na Msemaji Mkuu -Wizara ya fedha
Bi. Ingiahedi Mduma
Tokyo-Japan
9oktoba 2012

No comments:

Post a Comment