KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Thursday, 18 October 2012


Simon Group na mkakati wa kufuta adha ya usafiri Dar

ROBERT SIMON KISENA

Joseph Senga
SHIRIKA la Usafiri Dar es Salaam (UDA), licha ya kukumbwa na misukosuko na matatizo ya ufisadi hadi kukaribia kufa, sasa limerejeshewa uhai kupitia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Kampuni ya Simon Group Ltd.
Katika mahojiano na Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group, Robert Kisena, anasema mikakati ya shirika hilo ni kuleta ukombozi wa usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.
Kisena anakwenda mbali zaidi na kusema baada ya kupunguza kama na kumaliza adha hiyo kwa jijini Dar es Salaam, watajielekeza mikoani na nje ya nchi.
Kisena anasema chini ya mkakati huo kampuni yake imepanga kuleta mabasi 300 hadi kufika Machi, 2013, yatakayogharimu dola milioni 26 za Marekani.
Kisena anasema katika utekelezaji wa awali wa mpango huo wa mabasi 300, wataanza na mabasi 30 yatakayogharimu sh bil. 2.064 na 15 kati ya hayo, yameshazinduliwa na kuanza kazi Dar es Salaam.
Bila shaka, uwepo wa magari mengi ya UDA kwa mujibu wa Kisena, kutaongeza idadi ya mabasi katika njia mbalimbali, hivyo kupunguza adha ya usafiri kama si kumaliza kabisa.
Ukija kwenye uwekezaji wenyewe, Kisena anasema lengo ni shirika hilo kurejea kwenye enzi zake kabla ya kuanza kuporomoka kiuchumi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ufisadi.
Kisena anasema wachache walifanya vitendo vya kuhujumu shirika hilo bila kujali athari zake katika sekta ya usafirishaji na uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa.
Kwa mujibu wa Kisena, kwa kutambua ukubwa wa tatizo la usafiri kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, ndiyo maana kampuni hiyo imefanya uwezekezaji mkubwa.
“Mkakati wetu ni kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri wa abiria kwa Jiji la Dar es Salaam kwa kutoa huduma bora kupitia mradi wetu wa mabasi 300 kwa jiji hilo na mikoani,” anasema Kisena.
Anaongeza kuwa mbali ya ubora wa usafiri wa mabasi ya kawaida ya uuma, pia kutakuwa na mabasi ya daraja la juu (Executive Class), kwa lengo la kuboresha zaidi huduma hiyo.
Akifafanua juu ya mabasi hayo maalumu ambayo yatakuwa na bei tofauti na yale ya kawaida, Kisena anasema yatakuwa na huduma za ziada kama magazeti na vinywaji baridi.
Kisena anasema lengo la kuweka usafiri wa aina hii ni kuwapunguzia gharama wananchi wa Dar es Salaam wanaomiliki magari ili wavutike kutumia mabasi hayo maalumu na kuacha magari yao.
Anasema kwa hesabu walizofanya, baaadhi ya wamiliki wa magari wamekuwa wakitumia hadi sh 1,000,000 kwa mwezi kwa ajili ya mafuta na matengenezo ya magari, lakini kwa kutumia mabasi maalumu ya UDA, ataweza kutumia sh 120,000 hadi 150,000.
Mbali ya hilo, pia kampuni hiyo imekuja na mkakati mwingine wa kuwakomboa wanafunzi ambao ni kama wamekuwa hawana mtetezi pale wanapokwenda na kurudi shule.
Kisena anasema kwa muda mrefu wanafunzi wamekuwa wakinyanyaswa na makondakta hivyo kuchelewa kufika shule tu, pia wakati mwingine wameshinda kituoni kwa kukataliwa.
Kisena anasema kwa kuliona hilo, kampuni yake inakuja na ukombozi wa wanafunzi kwa kutenga mabasi maalumu kwa ajili yao kati ya hayo 300.
“Wanafunzi wamekuwa wakipata shida sana kwa kunyanyaswa na makondakta, hivyo kampuni yetu imekuja na ukombozi kwani tumetenga mabasi 20 kati ya 300 kwa ajili yao,” anasema.
Anasema mabasi hayo yatapelekwa katika maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam, hivyo kutopigana vikumbo na makondakta kila waendapo na kurudi shule.
“Ukiona namna mwanafunzi anavyonyanyaswa na makondakta wa daladala, utawaonea huruma, hivyo tumejipanga kuwaondolea adha hiyo ya kunyanyaswa kwa namna mbalimbali kama kutukanwa, kusukumwa na kuumizwa,” anasisistiza.
Kisema anasema mbali ya wanafunzi, mradi huo umekwenda mbali zaidi na kuwasaidia wanawake ambao nao wamekuwa wakipigwa vikumbo na wanaume katika kugombea magari.
Kwa kuliona hili, kati ya mabasi hayo 300, mengine yatakuwa maalumu kwa ajili ya wanawake tu yatakayoitwa ‘malaika’ kuwaondolea adha mbalimbali ambazo wamekuwa wakizipata ikiwemo udhalilishaji wa kijinsia.
Anasema lengo ni kuhakikisha wanawake wanaondokana na adha hiyo kwani hata kama watalazimika kugombea au kubanana, iwe wao kwa wao, si dhidi ya wanaume kama ambavyo imekuwa ikitokea.
Kisena anasema uamuzi wa kampuni yake kuwekeza kwenye Shirika hilo la UDA, ni kutaka kulipa uhai zaidi na kuwa mkombozi wa kada ya kipato cha chini na kati.
Anasema licha ya umuhimu wake, lakini shirika hilo limekuwa likisuasua kiuchumi hivyo kushindwa kutoa huduma kwa kiwango kilichokuwa kimetarajiwa kutokana na kukabiliwa na changamoto nyingi kiuendeshaji, ukiwemo ufisadi.
Kuhusu tatizo la wapiga debe, Kisena anasema uboreshaji wa huduma chini ya mabasi ya UDA, ni pamoja na kumwondolea msafiri adha zitokanazo na wapiga debe.
Anasema mradi huo ambao kwa kiasi kikubwa unaratibiwa na Kampuni ya Simon Group, kutakuwa na mabasi ya kwenda nje ya Dar es Salaam na ikiwezekana hata nje ya nchi.
Kisena anasema jambo hilo si geni kwani lilishawahi kufanywa na UDA wakati huo likiwa na uwezo mkubwa kiuchumi kama ilivyokuwa kwa iliyokuwa Kampuni ya Mabasi ya Taifa (Kamata).
Anasema chini ya mikakati hiyo, anaamini wataweza kupunguza tatizo la usafiri wa abiria, si kwa Jiji la Dar es Salaam tu, pia kwa Watanzania wote.
Zaidi ya usafiri wa abiria, kampuni hiyo pia imepanga kuwa na mabasi ambayo yatakuwa yakikodishwa na makampuni na taasisi mbalimbali zitakazotaka ili kubana matumizi.
Kisema anasema mradi huo ni wenye manufaa makubwa kwa wananchi kwani mbali ya kuwa suluhisho la adha ya usafiri kwani hadi kukamilika kwake utatoa ajira mpya za moja kwa moja 900.
Anasema kwa upande mwingine, uwekezaji wa Simon Group katika Uda, ni kuunga mkono juhudi za serikali kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kujenga uchumi.
“Naamini kwa uwekezaji huu uliogharimu fedha nyingi kwa shirika hili, ni fahari kwa Watanzania kwani kwa kiasi kikubwa utasimamiwa na wazalendo wenyewe, tutafanikiwa,” anasema kwa kujiamni Kisena.
Kisena anasema kitendo cha kushindwa kwa waliokuwa wakipiga vita mradi huo kwa masilahi yao kwa vile walikuwa wakilinyonya shirika, sasa hawana nafasi tena.
“Ni vema wakakaa pembeni kuupa nafasi uongozi utakaosimikwa kusimamia uwekezaji huu uliotukuka, pengine usio na mfano kwa taifa la Tanzania,” anasisitiza Kisena.
Kwa mipango, mikakati, dhamira na uthubutu wa Kampuni hii ya Simon Group katika kupunguza adha ya usafiri jijini Dar es Salaam, kuna haja wadau na wananchi kwa ujumla wakaunga mkono juhudi hizi.

No comments:

Post a Comment