WAJASIRIAMALI NCHINI WATAKIWA KUPATA MAFUNZO YA USIMAMIZI WA BIASHARA NA UJASIRIAMALI.
Meneja wa NMB, Tawi la Singida Mjini Christine Mwangomo akigawa cheti cha ushiriki kwa mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya msingi juu ya usimamizi wa biashara na ujasiriamali, kwa wateja wa benki hiyo.
Wajasiriamali wakifuatilia mada iliyotolewa na Clement Kihitula(hayupo pichani) juu ya kutambua gharama na kupanga bei.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakisikiliza kwa makini mada juu ya kutambua gharama na kupanga bei ili kuepuka hasara katika Usimamizi wa Biashara na Ujasiriamali.
Washiriki wa mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika ukumbi wa hoteli ya Aque mjini Singida.
Na Nathaniel Limu.
Wajasiriamali nchini wametakiwa kupata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa masuala ya biashara ili waweze kupata mafanikio zaidi katika kazi zao na kuhimili marejesho ya mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha.
Rai hiyo ilitolewa mjini Singida, wakati wa mafunzo ya msingi ya biashara, yaliyoendeshwa na benki ya NMB, Tawi la Singida na kushirikisha wajasiriamali zaidi ya 80, wanachama wa klabu ya benki hiyo mjini Singida.
Mafunzo hayo ya siku moja juu ya usimamizi wa biashara na ujasiriamali ambayo washiriki wote walipatiwa vyeti, yamefadhiliwa na benki ya NMB, kwa kushirikiana na klabu ya wateja wa benki hiyo Tawi la Singida mjini.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo Clement Kihitula kutoka mkoani Arusha, amesema wajasiriamali iwapo watapatiwa elimu ya msingi ya biashara, wanaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo, kutokana na kuwa na uelewa wa kutosha katika kuendesha kazi zao.
Amesema kwa kukosa elimu hiyo, baadhi yao hujikuta wakihusisha masuala ya kazi na familia zao, hali ambayo huathiri mtaji baada ya fedha kutumika katika kuhudumia mahitaji ya ndani ya nyumba, badala ya kuimarisha ajira (biashara).
Kutokana na hali hiyo, Kihitula amewataka wajasiriamali nchini kuhakikisha wanatenganisha ajira na huduma, na kuchukulia biashara zao sawa na ajira zingine serikalini au mahali pengine, ambako mtumishi hulipwa mshahara wake kwa wiki au mwezi, kulingana na hali halisi ya uzalishaji.
Kwa upande wake Meneja wa NMB, Tawi la Singida Mjini Christine Mwangomo, amesema pamoja na tawi hilo kuzidiwa na wateja, lakini hatua za makusudi zimeanza kuchukuliwa ikiwemo kuboresha madirisha ya kutoa na kuweka fedha, pia kuongeza mashine za kuchukulia fedha nje, ili kupunguza malalamiko.
Aidha Mwangomo amesema, ili kuondoa kero zaidi, benki hiyo inatarajia kujenga jengo jipya kubwa, katika eneo la viwanja vya utamaduni mjini Singida, ambalo litatosheleza mahitaji na huduma muhimu, kwa wateja wake wote.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Elizabeth Masawe na Omari Sombi wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata na kuahidi kuimarisha biashara zao, ili kuepuka utendaji kazi wa mazoea, kutokana na mbinu mbalimbali walizopewa.
No comments:
Post a Comment