KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Friday, 14 September 2012


MKE WA RAIS WA ZANZIBAR AWATAKA WANANCHI KUSHIIRIKIANA NA POLISI KUKOMESHA DAWA ZA KULEVYA.


Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein,akifungua pazia kama ishara ya uzinduzi wa Kituo cha Polisi cha Fumba Mkoa Mjini Magharibi,(kulia) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdalla Mwinyi Khamis,na Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa.[Picha na Ramadhan Othman Ikulu.]
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, akikata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Kituo cha Polisi cha Fumba Mkoa Mjini Magharibi,(kulia) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdalla Mwinyi Khamis,na Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa.[Picha na Ramadhan Othman Ikulu.]
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein,akipata maelezo kutoka kwa Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa,alipokitembelea Kituo cha Polisi cha Fumba Mkoa Mjini Magharibi,baada ya kufanya ufunguzi rasmi wa kituo hicho kilichojengwa na jeshi hilo,(katikati) Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Pili Balozi Seif Iddi.[Picha na Ramadhan Othman Ikulu.]
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, amewataka wananchi kushiirikiana na Jeshi la Polisi Visiwani humo katika kuwafichua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu mwambao wa pwani ya visiwa hivyo ukiwemo uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya.
Mama Mwanamwema, ametoa wito huo leo mjini Zanzibar, wakati akizindua kituo kipya cha Polisi cha Fumba kilichojengwa kwa nguvu za wananchi na Wawekezaji katika wilaya ya Magharibi Zanzibar.
Mke huyo wa Rais wa Zanzibar amesema kuwa kujengwa kwa kituo hicho ni kazi moja lakini kazi ya kuwafichua wahalifu ni kazi ya pili ambayo inawategemea sana wananchi ambao ndiyo wanaoishi pamoja nao.
Amesema kituo hicho kitasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukomesha vitendo vya kihalifu vikiwemo vya magendo, wizi wa mifugo, usafirishaji na usambazaji wa madawa hayo ya kulevya ambayo yamekuwa yakiathiri afya za vijana wa visiwa hivi na Tanzania kwa ujumla.
Amemtaka kila mwananchi kuhakikisha kuwa anamfichua na kumtolea taarifa Polisi mhalifu yeyote ili achukuliwe hatua ikiwa ni pamoja na kukamatwa na kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
“Ndugu Wananchi, ninamategemeo makubwa kuwa kituo hiki cha Polisi kitasaidia sana katika kupambana na matukio ya kihalifu”. Alisema Mama Shein.
Alisema taarifa zilizopo ni kuwa maeneo haya yanachangamoto ya uhalifu wa aina mbalimbali, Wafugaji hapo salama na mifugo yao na wakulima nao hawapo  salama na mazao yao.
Awali akimkaribisha Mke wa Rais, Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, alisema kuwa, kwa kiasi kikubwa, ujenzi wa kituo hicho umechangiwa na baadhi ya wafanyabishara yakiwemo Mabenki, Shirika la Umeme na wawekezaji wa kigeni.
Amesema Jeshi la Polisi limesaidia kuweka mafundi wa ujenzi na kugharimia baadhi ya mahitaji muhimu kwa lengo la kufanikisha ujenzi huo na kuwasogezea huduma za kipolisi wakazi wa eneo hilo ambalo kwa muda mrefu lilikuwa halina kituo cha Polisi.
Nao baadhi ya wananchi wamepongeza juhudi binafsi zilizochukuliwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, katika kuwashawishi wawekezaji wa kigeni na mabenki kuchangia ujenzi wa kituo hicho.
Miongoni mwa Makampuni yaliyochangia katika ujenzi huo ni Benki ya Wananchi wa Zanzibar BPZ na Shirika la umeme Zanzibar ZECO.
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Mke wa makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mama Pili Seif Iddi pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Bw. Abdallah Mwinyi na Makamaba wa Polisi wa mkoa wa Mjini na makao makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar.

No comments:

Post a Comment