UCHAGUZI MDOGO WA MADIWANI KUFANYIKA OKTOBA MWAKA HUU.
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Jullius Mallaba akizungumzia maandalizi ya uchaguzi mdogo wa madiwani kata 29 Tanzania.(Picha na Geofrey Mwakibete wa MO BLOG).
Na Veronica Kazimoto- MAELEZO
Uchaguzi mdogo wa Madiwani katika kata ishirini na tisa na halimashauri ishirini na saba Tanzania bara utafanyika tarehe 28 Oktoba, mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na viongozi wa siasa ngazi ya Taifa leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi Julius Mallaba amesema maandalizi ya uchaguzi huo yameanza rasmi ili kuhakikisha kwamba kila raia mwenye sifa anapata fursa ya kushiriki na kuchagua kiongozi anayemtaka.
Amezitaja Kata na Harimashauri hizo kuwa ni pamoja na Bangata (Halmashauri ya Wilaya ya Arusha), Darajambili (Halmashauri ya Manispaa ya Arusha), Msalato (Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma), Mpwapwa (Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa), Magomeni (Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Lwezera (Halmashauri ya Wilaya ya Geita) na Bugarama (Halmashauri ya Wilaya ya Kahama).
Nyingine ni Mwawaza ambayo iko Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Vugiri (Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe), Tamota (Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto), Makata (Halmashauri ya Wilaya ya Liwale), Mnero Miembeni (Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea), Mlangali (Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa), Luwumbu (Halmashauri ya Wilaya ya Makete), na Mpepai (Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga).
Zimetajwa pia Kata za Mletele (Halmashauri ya Wilaya ya Songea), Ipole na Kiloleli (Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge), Miyenze (Halmashauri ya Wilaya ya Tabora), Karitu (Halmashauri ya Wilaya ya Nzega), Mpapa na Myovizi (Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi), Lubili (Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi), Kilema Kusini (Halmashauri ya Wilaya ya Moshi), Nanjara/ Reha (Halmashauri ya Wilaya ya Rombo), Mtibwa (Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero), Mahenge (Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga), Likokona (Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu) na Kitangari (Halmashauri ya Wilaya ya Newala).
Katika mkutano huo Mallaba ametangaza ratiba ya uchaguzi mdogo wa madiwani kuwa uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 2 oktoba, 2012, kampeni za uchaguzi zitaanza oktoba 3 hadi oktoba 27, 2012 na fomu za uteuzi kwa wagombea na wasimamizi wa uchaguzi zimeanza kutolewa.
Aidha Mallaba amefafanua kuwa tayari tume imeshateua watendaji watakaosimamia chaguzi hizo na inaendelea na maandalizi mengine ambayo ni pamoja na mafunzo kwa watendaji, uchapishaji na ununuzi wa vifaa vya uchaguzi, uchapishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, utoaji wa elimu ya mpiga kura na uudaji wa kamati za maadili.
amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itahakikisha kwamba chaguzi hizi zinafanyika kwa uwazi, uhuru na haki kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kujenga demokrasia na kuimarisha utawala bora.
Julius Mallaba ameviomba vyama vyote vya siasa vitavyoshiriki katika uchaguzi huo kuzingatia sheria na maadili ili kuepusha malumbano yanayoweza kujitokeza.
No comments:
Post a Comment