YANGA YAMALIZIA HASIRA KWA JKT RUVU, MTIBWA YAKALISHWA CHAMAZI
BAADA ya kuianza vibaya siku ya Jumamosi kwa uongozi kutangaza rasmi kumfukuza kazi kocha wao Mbelgiji Tom Saintfiet, hatimaye Yanga imezinduka kutoka katika mwanzo mbaya wa msimu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kutoa kisago kikali cha magoli 4-1 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.
Mshambuliaji mpya, Didier Kavumbagu, aliyejiunga na Yanga katika kipindi kilichoisha cha usajili akitokea katika klabu ya Atletico ya Burundi baada ya kuizamisha timu hiyo ya Jangwani magoli mawili katika michuano ya Kombe la Kagame, ameonyesha leo kuwa ameanza kufanya kazi iliyomleta baada ya kufunga magoli mawili katika ushindi huo uliohitajika kwa lazima.
Ilikuwa ni lazima Yanga ishinde leo ili kuweka hali sawa baada ya sare ya 0-0 ugenini Mbeya dhidi ya Prison katika mechi ya ufunguzi wa ligi na kipigo kishotarajiwa cha 3-0 kutoka kwa Mtibwa mjini Morogoro Jumatano kilichofanya miamba hao wa soka nchini kumfukuza kocha wao aliyewapa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, huku pia wakiisimamisha kazi sekretarieti nzima.
Kavumbagu ambaye alianzishwa kwa mara ya kwanza leo baada ya mechi zilizotangulia kuingia kutokea benchi na kuonekana hatari kwa mashuti yake makali, alifungua akaunti yake ya maagoli kwa klabu yake mpya huku mengine mawili yakifungwa na Simon Msuva na beki Nadir Haroub 'Cannavaro'.
Ushindi huo umeifanya Yanga, ambayo iliingia uwanjani leo ikiwa katika nafasi ya 13 katika msimamo wa timu 14 kutokana na kuwa na pointi moja, kufikisha pointi nne.
Washindi wa pili wa msimu uliopita, Azam walikwea kileleni mwa msimamo baada ya kufikisha pointi 7 kufuatia ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi katika mechi nyingine iliyochezwa leo. Goli la Azam lilifungwa na Kipre Tchetche katika dakika ya 25.
Mtibwa walicheza wakiwa pungufu kwa takribani kipindi cha pili chote baada ya Salvatory Ntembe kutolewa kwa kadi ya pili ya njano katika dakika ya 52.
Mabingwa Simba wenye pointi 6 kutokana na mechi mbili watacheza kesho kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya Ruvu Shooting.
Mjini Arusha, JKT Oljoro wameifunga Polisi Moro goli 1-0 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kufikisha pointi 5, huku mkoani Tanga, wenyeji Coastal Union wakishikiliwa katika sare ya 0-0 dhidi ya Toto African ya Mwanza.
Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa; Yanga: Yaw Berko, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nizar Khalfan/ Shamte Ally, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbangu/ Jerry Tegete, Hamisi Kiiza na Simon Msuva.
JKT Ruvu: Said Mohamed, Kessy Mapande, Stanley Nkomola, Damas Makwaya, Charles Timoth, Ally Khan, Haroun Adolf, Said Ahmed ‘Ortega’/ Jimmy Shoji, Omar Changa/ Furaha Tembo, Hussein Bunu na Sostenes Manyasi/ Credo Mwaipopo.
No comments:
Post a Comment