KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Saturday, 22 September 2012


 
SHULE ya Msingi Bokorani, Mtoni-Mtongani, wilayani Temeke, Dar es Salaam hivi karibuni imekumbwa na matukio ya ajabu ya kupotea wanafunzi wanapotoka shule katika mazingira ya kutatanisha.

Kwa kipindi cha wiki mbili katika mwezi mmoja, imeripotiwa kupotea kwa wanafunzi watatu wa madarasa tofauti, wote wa kike na matukio hayo yamehusishwa na masuala ya kishirikina.

Tukio la kwanza lilitokea Juni 19 mwaka huu baada ya mwanafunzi wa darasa la kwanza Zawia Mohammed (7) (pichani) kupotea alipotoka shule na mpaka mwishoni mwa wiki, hakuwa amepatikana.

Taarifa zinaeleza kuwa, katika kipindi cha wiki mbili baada ya Zawia kupotea, wanafunzi wengine wa kike wawili ambao majina yao hayakuweza kupatikana, wa darasa la tano na la sita, walipotea katika mazingira kama hayo.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Abdallah Mshana akizungumza na gazeti hili hivi karibuni kuhusu matukio hayo alikiri kutokea katika shule yake mwezi Juni na kubainisha kuwa wanafunzi wawili kati ya hao watatu, walipatikana.

Alisema tukio la kwanza lilimhusu mwanafunzi wa darasa la kwanza, Zawia Mohamed mwenye umri wa miaka saba, na aliripotiwa kupotea Juni 19 mwaka huu na taarifa ilifikishwa kwake Juni 22, “Siku ya tukio nilikuwa kwenye mkutano Halmashauri, siku moja baadaye walimu wakanieleza kuhusu tukio hilo na kesho yake baba wa mtoto alikuja kutoa taarifa na kuuliza kama amepatikana,” alisema Mwalimu Mshana.

Mshana alisema taarifa alizopewa na baba wa mtoto huyo zinadai kuwa, alipotoka shule, alikutana na mtu nje ya geti la shule karibu na barabara kuu ya Kilwa na mtu huyo alimvusha barabara na hajaonekana tena, “Tulichukua hatua sisi na wazazi wake kwenda Ofisi za Serikali za Mitaa kutoa taarifa na tukiwa pale uongozi wa Serikali ulipiga simu Polisi Kituo kidogo cha Mtongani, juhudi za kumtafuta bado zinaendelea”.

Katika hali ya kushangaa, Mshana alisema katika kipindi cha wiki mbili baada ya Zawia kupotea, walipotea wanafunzi wawili wa kike na baada ya kutafutwa kwa siku kadhaa, walipatikana isipokuwa Zawia.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, David Misime alithibitisha kupotea kwa mtoto huyo na kueleza kuwa taarifa ilifika Polisi Juni 20 mwaka huu na wanaendelea kumtafuta, “Ni kweli mtoto huyo alipotea na tunaomba wazazi waendelee kuwasiliana na sisi ,” alisema.

via HabariLeo


No comments:

Post a Comment