KARIBUNI

Pata habari za kila siku, burudani,matangazo, na mengineyo mengi pia unaweza kuacha maoni yako kuhusu tovuti hii.

Tuesday, 18 September 2012


BALOZI SEIF AAHIDI SERIKALI KUWASAIDIA VIJANA WANAOJIREKEBISHA NA KUACHA KUTUMIA MADAWA YA KULEVYA.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Baskeli Kijana Mlemavu Badri Ameir Issa ambayo itamsaidia katika harakati zake za Kimaisha. Msaada huo amekabidhiwa katika Nyumba ya kurekebishia Tabia iliyopo Nyarugusu Shehia ya Pangawe Wilaya ya Magharibi. Kushoto ni Mlezi Mkuu wa Nyumba hizo Bibi Fatma Sukwa.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Viongozi pamoja na Vijana wanaoishi katika Nyumba za kurekebisha Tabia kwa watu waliokuwa wakitumia dawa za kulevya { Sober House } zilizopo Nyarugusu Wilaya ya Magharibi.
Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi  vyakula Mshauri Mkuu wa Nyumba saba za kurekebishia Tabia Unguja na Pemba  Bibi Fatma Sukwa  kwa ajili ya kusaidia Vijana wa nyumba hizo. Wa kwanza kushoto ni mlezi wa Nyumba ya kurekebishia watu waliotumia dawa za kulevya ya  Mtaa wa Nyarugusu Shehia ya Pangawe Bw. Badru Nassor Ali.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuwasaidia Vijana waliotengemaa baada ya kuacha matumizi ya dawa za kulevya kwa kuwapatia mtaji endapo vijana hao wataamaua kubuni na hatimae kuanzisha miradi ya kujiimarisha Kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Viongozi na baadhi ya Vijana waliomo katika nyumba saba za kurekebishia tabia Unguja kwa watu waliokuwa  wakitumia  dawa za kulevya, katika moja ya nyumba hizo iliyopo Mtaa wa Nyarugusu Shehia ya Pangawe Wilaya ya Magharibi.
Balozi Seif amesema Serikali kupitia Wizara inayosimamia masuala ya Ajira ina mpango wa kuwawezesha Wananchi hasa Vijana kujiendesha kimaisha  katika dhana nzima ya kuwajengea mazingira ya kuchapa kazi kwa vile Vijana ndio nguvu kazi kubwa inayotegemewa na Taifa.
Amesema kazi kubwa inaendelea kufanywa kupitia Taasisi, Jumuiya Washirika wa Maendeleo kwa kushirikiana na Serikali  ya kubadilisha tabia kwa Watu na hasa Vijana kuacha kuendelea kutumia dawa za kulevya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameshauri kuwa ipo haja kwa Jamii kwa kushirikiana na Serikali Kuu pamoja na washirika wa Maendeleo kutafuta mbinu za kuwajengea mazingira bora Vijana walioacha matumizi ya dawa hizo ili wajiepushe kurejea katika magenge ya kihuni.
Mapema Mlezi Mkuu wa Nyumba saba za kurekebishia Watu wanaotumia dawa za kulevya Zanzibar Bibi Fatma Sukwa alisema asilimia  42% ya watu waliopitia katika Nyumba hizo wameacha matumizi ya Dawa za kulevya katika kipindi cha miaka mitatu.
Bibi Fatma alifafanua kwamba asilimia 48% ya Vijana waliopitia Nyumba hizo wamerejea kutumia dawa za kulevya baada ya kutengwa na Familia zao, asilimia 1% hadi sasa hawajuilikani taarifa zao tokea waondoke katika Nyumba hizo.
Mshauri huyo Mkuu wa Nyumba za kurekebishia tabia kwa watu waliotumia dawa za kulevya ameitahadharisha Jamii kuelewa kwamba dawa za kulevya ni ugonjwa kama magonjwa mengine yanayo wazunguka wanadamu.
Kwa upande wake Mshauri wa kuacha dawa za kulevya na kubadilisha tabia katika nyumba saba za kurekebishia tabia za Unguja na Pemba Bw. Ahmed Islam ameema Jamii inapaswa kuacha tabia ya kuwanyooshea vidole Vijana walioathirika kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.
Bw. Ahmed Islamu amempongeza na kumshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa msaada wake ambao ni faraja kwao ukionyesha kuyathamini makundi hayo ya Vijana.

No comments:

Post a Comment