Ngwilizi aonya wanaozungumzia kashfa ya majaji
Brigedia Jenerali (Mstaafu) Hassan Ngwilizi,
Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Brigedia Jenerali (Mstaafu) Hassan Ngwilizi, ameonya watu kutozungumzia masuala yanayochunguzwa na kamati yake hususani la kashfa ya majaji iliyoibuliwa wakati wa mkutano wa Nane wa Bunge.
Ngwilizi akizungumza na waandishi wa habari jana alisema ambalo linachunguzwa na Bunge ni kinyume cha Katiba Ibara ya 100 na ile ya 89 (1), inalipa Bunge mamlaka ya kujiwekea utaratibu wa kushughulikia masuala yake bila kuingiliwa.
Alisema kuripoti au kuzungumza jambo linalochunguzwa na kamati hiyo ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 31 (1) (f) cha Sheria Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, Sura ya 296.
Alieleza kushangazwa na malumbano ya hivi karibuni katika vyombo vya habari kuhusu kinachoendelea ndani ya kamati yake na kueleza kuwa ni kinyume cha Katiba, sheria na kanuni za Bunge zinaweka mamlaka na kinga kwa mhimili huo kutoingiliwa.
Alisema kutokana na unyeti wa suala hilo, hairuhusiwi kwa taasisi au mtu yeyote kulizungumza nje ya Bunge kwa kuwa linajadiliwa na kamati yake.
"Hivyo basi, Kamati inashauri watendaji wa Serikali, Mahakama na taasisi nyingine zote, kuacha kuzungumzia suala la uteuzi wa majaji kama ambavyo limewasilishwa Bungeni...inavishauri vyombo vya habari kuacha kuzungumzia suala hili mpaka pale ambapo uamuzi wa Kamati utakapotolewa Bungeni," alisema.
Ngwilizi alisema badala yake, taasisi au mtu yeyote ambaye ana maoni kuhusiana na suala hilo anaweza kuyawasilisha kwa Katibu wa Bunge ili yafanyiwe kazi na kamati yake.
"Kamati inaelewa unyeti wa suala hili kwa pande zote ambazo zinahusika na inapenda kuwahakikishia umma wa Watanzania kuwa ushauri wa Kamati kwa Bunge utazingatia ukweli, uwazi na uwajibikaji bila kupendelea au kuonea mtu yeyote," alisema Ngwilizi.
Katika mkutano wa Bunge uliopita, Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alisema Kambi ya Upinzani inazotaarifa kuwa baadhi ya majaji wa Mahakama Kuu walioteuliwa hawakuwa na sifa huku wengine wakiwa hawajawahi kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Alisema baadhi yao wameteuliwa kushika wadhifa huo wakiwa wameshastaafu au wanakaribia kustaafu jambo ambalo ni kinyume cha Katiba.
Hotuba ya Lissu ambaye ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni na mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), iliibua mvutano mkali kutoka kwa wabunge hali iliyomlazimu Spika wa Bunge, Anne Makinda kulifikisha kwenye Kamati ya Ngwilizi kwa ajili ya uchunguzi.
No comments:
Post a Comment