YANGA YALITEKA BUNGE DODOMA
Makamu Mwenyekiti wa Yanga,
Clement Sanga wa pili kulia akiwa na kocha Mkuu wa timu hiyo, Tom
Saintfiet.
Wachezaji wa
Yanga wakiwa Bungeni mjini Dodoma.
Na Danson
Kaijage, Dodoma
MABINGWA wa
soka Afrika Mashariki na Kati, ‘Kagame Cup’ Yanga ya jijini Dar es Salaam, leo
wamepokewa kwa shangwe na wabunge wanazi wa timu hiyo, lakini wakikumbana na
kebehi za watani zao, Simba kwa kuwaonesha alama ya vidole vitano walipofanya
ziara ya kulitambulisha kombe hilo bungeni.
Licha ya
kupokewa kwa kishindo, baadhi ya wale wa Simba nao waliibuka na kuwakebehi kwa
kuonesha vidole vitano juu, wakimaanisha kipigo cha 5-0, ilichopokea katika
mechi ya kufunga msimu wa Ligi Kuu Bara, msimu uliopita.
Hali hiyo
ilitokea wakati Spika, Anne
Makinda alipokuwa akitambulisha wageni waliohudhuria bungeni kwa ajili ya
kuangalia shughuli zinazoendelea.
Baadhi ya
wabunge walionekana kuonesha mikono yao ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samwel Sitta na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,
Sophia Simba.
Wengine ni
Mbunge wa Tabora mjini, Aden Rage, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na
Mbunge wa Viti Maalum, Diana Chilolo.
Akitangaza
ujio huo wa Yanga, Makinda alisema: “Mimi siku zote huwa natangaza watu ambao
wanaleta vitu vizuri bungeni. Hawa Yanga ni wageni mashuhuri kutokana na kuleta
vitu vizuri.
“Lakini,
mimi nikisema hivi, baadhi ya wabunge wanasema mimi ni mpenzi wa Yanga, kitu
ambacho si kweli…Yanga wameleta ubingwa, ndiyo maana nimewatangaza,” alisema
Spika Makinda.
Wakati
Makinda akitoa kauli hiyo, baadhi ya wabunge waliangua kicheko,
ambapo pia aliongeza: “Namuona Mh. Spika aliyepita (Samwel Sitta), ananiangalia
lakini huo ndiyo ukweli.”
Kikosi
hicho cha Yanga, kiliambatana na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya klabu hiyo,
Fatuma Karume, Francis Kifukwe.
Kwa upande
wa uongozi, ni Mwenyekiti Yusuph Manji na Makamu wake Clement Sanga walioingia
madarakani Julai 15, kupitia uchaguzi mdogo.


No comments:
Post a Comment